Home Habari za michezo KISA ‘PANGA PANGUA’ ZA BODI YA LIGI…GAMONDI ASHINDWA KUJIZUIA YANGA…MSIMAMO WAKE HUU...

KISA ‘PANGA PANGUA’ ZA BODI YA LIGI…GAMONDI ASHINDWA KUJIZUIA YANGA…MSIMAMO WAKE HUU HAPA..

Habari za Yanga SC

Bodi ya Ligi (TPLB) wikiendi iliyopita ilifanya mabadiliko madogo ya ratiba za Ligi Kuu Bara kwa kulirudisha nyuma pambano la Yanga na Azam lililokuwa lipigwe Oktoba 25 na kulipanga lichezwe wikiendi hii, jambo lililomfurahisha kocha Miguel Gamondi aliyesema ndivyo alivyokuwa anataka.

Gamondi aliyeiongoza timu hiyo kwenye jumla ya mechi 11 za mashindano na kupoteza mbili tu ikiwamo moja ya fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na ile ya Ligi kuu Bara mbele ya Ihefu, amesema kurejesha kwa mechi nyuma ni nafuu kwani wachezaji walikuwa wanakaa muda mrefu bila mechi ya ushindani.

Kocha huyo alisema pia anaamini hadi mechi ipigwe Jumamosi, tayari nyota wa timu hiyo waliopo timu za taifa watakuwa wamesharejea na kumrahisishia kazi ya kuzisaka pointi tatu nyingine na kujiweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi hiyo inayoongozwa na Simba yenye pointi 15, tatu zaidi na ilizonazo Yanga.

Gamondi  alisema badiliko hilo la Bodi ya Ligi imekuwa faraja kwake na hana wasiwasi kwa wachezaji wake waliopo timu za taifa, kwani watarudi wakiwa moto zaidi.

“Nimefurahishwa na mabadiliko ya ratiba, kwani awali nilikuwa naumiza kichwa namna ya kupata mechi ya kirafiki ili kuwajenga kimwili na kiushindani wachezaji ambao wamekaa nje ya uwanja kwa muda bila kucheza,” alisema kocha huyo raia wa Argentina na kuongeza;

“Djigui Diarra, Stephane Aziz Ki na Khalid Aucho wanacheza mechi za mwisho za kirafiki wakitumikia timu za taifa, Oktoba 18 nimewaamuru warudi siku inayofuata ili kujiandaa na mchezo huo na Azam kwani ni mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa.”

Juu ya nafasi ya kuwatumia kwenye mchezo ambao Yanga ni wenyeji, Gamondi alisema ana imani nao kwani ni wachezaji waliopewa kipaumbele na timu hizo kwa kucheza dakika nyingi kwenye mechi ya kwanza hivyo anatarajia kuona wakiwa bora na fiti zaidi.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo alisema wachezaji wanaingia kambini isipokuwa waliopo timu za taifa wakiwamo wale wa Taifa Stars na amekuwa akiwakazania kujiweka fiti zaidi kwani bdo kuna safari ndefu kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa, Yanga ikiwa imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa.

“Ni wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wameitwa timu zao za taifa, hilo haliondoi mimi kuendelea kuwaandaa wachezaji waliopo na wao pia wana mchango kwenye timu. Yanga haimtegemei mchezaji mmoja, wanategemeana wote hivyo kurudi kwao ni mwanzo mzuri wa kuwaandaa tayari kwa mechi iliyopo mbele kwani hautokuwa rahisi. Azam ni moja ya timu ambazo hazijapoteza mechi,” alisema Gamondi.

Kocha huyo pia alikiri anatambua ugumu wa ratiba iliyo mbele yao, hivyo atahakikisha anawaandaa wachezaji wote kwenye ubora ili kupeana nafasi ya kucheza na wengine kupumzika kulingana na aina ya mashindano waliyonayo.

Ratiba inaonyesha kwamba Yanga ikimalizana na Azam Oktoba 22, itakuwa na kibarua kingine Oktoba 26 dhidi ya Singida Bi Stars kabla ya Novemba 5 kuvaana na Simba halafu itaenda Tanga kucheza na Coastal Union Novemba 8.

SOMA NA HII  FT: YANGA SC 4-1 SINGIDA BIG STAR....MAYELE AFANYA YAKE...KAGERE AENDELEA KUWACHOVYA YANGA...