Wachezaji Djigui Diarra, Stephene Aziz Ki na Khalid Aucho wameripoti kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC.
Young Africans na Azam FC zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa kumi na mbili na nusu jioni mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa Jumatatu (Oktoba 23).
Nyota hao walikuwepo katika majukumu ya timu zao za taifa, michezo ya tarehe za Fifa wote hao walimaliza mechi zao juzi Jumatano (Oktoba 18).
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Muargentina Miguel Gamondi tangu mapema alifanya mawasiliano na wachezaji hao kwa kuwapa taarifa za kuripoti kambini juzi Alhamisi (Oktoba 19).
Gamondi amesema kuwa wachezaji hadi kufikia juzi Alhamis (Oktoba 19) mchana walikuwepo njiani wakirejea nchini tayari kwa ajili ya kuiwahi kambi ya pamoja na wenzao.
Amengeza kuwa wachezaji waliokuwepo katika kambi ya Taifa Stars, wenyewe tangu Jumanne wameripoti kambini ambao ni Metacha Mnata, Dickson Job, Bakari Mewamnyeto, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya na Nickson Kibabage.
“Diarra, Aziz Ki na Aucho wamemaliza mechi zao za mwisho za kirafiki juzi Jumatano wakitoka kutumikia timu zao za taifa, Niliwaambia kuwa warudi hapa Alhamisi kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam FC.
“Niwapongeze kwa kufuata maagizo yangu, na Alhamisi usiku wachezaji wote waliripoti kambini kujiandaa na mchezo huo mgumu ambao tunahitaji pointi tatu.
“Kurejea kwao mapema na kuingia kambini, kutanipa nafasi ya kuwaongezea mbinu za ushindi kuelekea mchezo huo uliopaniwa na wapinzani wetu,” alisema Gamondi.