Home Habari za michezo AFCON 2023….TANZANIA KUFUNGUA DIMBA NA MOROCCO…KUMALIZA KAZI NA KINA MAYELE…

AFCON 2023….TANZANIA KUFUNGUA DIMBA NA MOROCCO…KUMALIZA KAZI NA KINA MAYELE…

Taifa Stars

TIMU ya taifa ‘Taifa Stars’ itafungua Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast mwakani kwa kucheza na Morocco, Januari 17 katika Uwanja wa Laurent Pokou, San Pedro.

Mchezo huo utafungua mechi za kundi F lililo pia na Zambia na DR Congo na umepangwa kuanza saa 2:00 usiku.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) juzi jioni, mchezo wa pili wa Stars utakuwa Januari 21 dhidi ya Zambia na itahitimisha hatua ya makundi na DR Congo Januari 24.

Stars imekuwa haina historia nzuri na mechi ya kwanza ya makundi katika fainali za Afcon ambapo mara mbili ilizoshiriki ilipoteza mechi ya ufunguzi.

Mara ya kwanza ilikuwa 1980 zilipofanyika Nigeria ambapo ilipoteza mechi ya kwanza ya kundi kwa mabao 3-1 kutoka kwa Nigeria. Pia mechi ya kwanza ya makundi ilipoteza 2019 zilipofanyika Misri dhidi ya Senegal kwa mabao 2-0.

Lakini dhidi ya Morocco, Stars sio tu itakuwa inasaka historia ya ushindi katika mechi ya kwanza ya kundi, bali itakuwa ikitafuta ushindi wa kwanza wa fainali za Afcon kwani haikuwahi kushinda mchezo wowote.

Katika mara mbili ambazo imeshiriki imecheza mechi sita za makundi, imetoka sare moja tu huku ikifungwa michezo mitano.

Kocha msaidizi wa Stars, Hemed Morocco alisema hawana hofu kwa ratiba hiyo na wanachokifikiria ni kujiandaa vizuri ili waandike historia katika Afcon mwakani.

“Makundi yakishapangwa maana yake utacheza dhidi ya kila timu ambayo ipo kwenye kundi jambo ambalo hata sisi tulishajiandaa nalo. Kinachohitajika ni maandalizi ya uhakika ambayo yatatuwezesha kupata matokeo mazuri katika mechi zote tatu za kundi ili tuingie katika hatua inayofuata,” alisema.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUWA NA KUWANGO KIKUBWA...NABI APITISHA 'TIKI YA KIJANI KWA SAIDO'...UONGOZI WATOA NENO...