Home Habari za michezo AHMED ALLY:- SIMBA ITAUFUTA UFALME WA AL AHLY AFRIKA…KAZI INAANZA IJUMAA…

AHMED ALLY:- SIMBA ITAUFUTA UFALME WA AL AHLY AFRIKA…KAZI INAANZA IJUMAA…

Habari za Simba

UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa safari hii lengo lao ni kuiondoa kwenye mashindano Al Ahly ya Misri kwenye michuano ya kimataifa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka mingi.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema lengo na mikakati ya safari hii watacheza nayo kwenye michuano ya Afrika Football League (AFL) Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ni kuiondoa kwenye mashindano na si kuwafunga tu hapa nchini kama ambavyo wamekuwa wakifanya mara zote.

“Hata Al Ahly wanaifahamu Simba na hawataona kitu kipya tukawafunga hapa nyumbani kwa sababu tuliwahi kufanya hivyo, safari hii tumejipanga kutaka kuwatoa kwenye mashindano hayo kwa kuwafunga hapa na kwao kwenye mchezo wa marudiano,” alisema Ahmed.

Aliongeza kuwa benchi la ufundi linaloongozwa na Roberto Oliveira (Robertinho) anaendelea kukisuka kikosi na ameanza kutengeneza dawa ya kuwaondoa Al Ahly katika mashindano hayo.

“Kikosi kipo kambini kwa wachezaji ambao hawako kwenye majukumu ya Taifa, wale majeruhi tayari wanaendelea vizuri akiwemo beki yetu, Henock Inonga ambaye yuko kwenye majukumu ya timu ya Taifa, Manula (Aishi) amerejea vizuri kwenye mazoezi,” alisema .

Simba imeifunga Al Ahly mara zote inapokutana nayo hapa nchini, tatizo linakuwa inapokwenda ugenini nchini Misri.

Mwaka 1984, Simba iliifunga Al Ahly mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ikiwa ni Kombe la Washindi Barani Afrika (sasa Kombe la Shirikisho), kwa mabao ya Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ na Mtemi Ramadhani, lakini ikapoteza kwa mabao 2-0 ilipokwenda Cairo na kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2.

Zilikutana tena 2019 zikiwa kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ikipigika nchini Misri mabao 5-0, lakini ikashinda nyumbani bao 1-0 la Meddie Kagere, na 2021 Simba iliichapa tena Al Ahly nchini bao 1-0 lililowekwa wavuni na Luis Miquissone katika mechi ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ikifungwa tena ugenini bao 1-0.

SOMA NA HII  KIUNGO SIMBA AZURURA NA MKATABA MITAANI...MWENYEWE AWEKA MASHARTI YA KUUSAINI....