Home Habari za michezo BAADA YA KONKAN KUPEWA MECHI 4 YANGA, GAMONDI NAE AWEKA WAZI MSIMAMO...

BAADA YA KONKAN KUPEWA MECHI 4 YANGA, GAMONDI NAE AWEKA WAZI MSIMAMO WAKE

Habari za Yanga SC

Kikosi cha Yanga kinajifua kwa mazoezi makali ajili ya pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC litakalopigwa Oktoba 25, huku kocha wa timu hiyo, Manuel Gamondi amedaiwa kuwapa mechi nne mastaa wasiopungua watano akiwamo straika Hafiz Konkoni kabla ya kufanya maamuzi magumu.

Yanga inajifua kwenye kambi yake ya Avin Town, Kigamboni Dar es Salaam, huku baadhi ya wachezaji wakiwa kwenye timu za taifa zinazojiandaa kwa mechi za kirafiki za kimataifa.

Hata hivyo, habari kutoka kwenye kambi hiyo ya Yanga zinasema kuwa Kocha Gamondi amekaa na baadhi ya wachezaji ambao wameshindwa kuonyesha kitu licha ya kupewa nafasi ya kuitumikia timu hiyo kabla ya kufanya uamuzi kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba.

Taarifa hizo zinasema, Gamondi amegeuka mbogo na kuwawakia wachezaji wasiojituma huku akiwapa mechi nne za kujitafakari kabla ya panga halijawapitia kwenye dirisha dogo.

Gamondi aliyetua Yanga kuchukua nafasi ya Nassredine Nabi aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco, amekuwa akitoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha uwezo, lakini amegundua kuna wachezaji wanategea na wengine hawastahili kuwepo Yanga kwa sasa.

Ukimuondoa kipa Aboutwalib Mshery, ambaye ndiye pekee hajapata walau dakika tano za kucheza kwenye mechi za mashindano tangu arejee kutoka majeruhi, lakini waliosalia wote wamepata nafasi na kucheza kuonyesha walichonacho.

Chanzo hicho cha kuaminika kutoka kambi ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti, Gamondi tayari ana majina ya mastaa wasiopungua wanne wakiwemo washambuliaji, Hafiz Konkoni, Crispin Ngushi na beki kutoka Uganda, Gift Fred aliofanya nao mazungumzo ya mmoja mmoja kuwataka waongeze bidii.

Katika mazungumzo hayo, inaelezwa kocha huyo kutoka Argentina amewaeleza, atakuwa akiwapanga katika muda tofauti kwenye mechi nne zijazo za mashindano zikiwa za Ligi Kuu ili kuangalia maendeleo yao na watakaochemsha basi wajue panga linawahusu.

Hafiz alisajiliwa hivi karibuni kutoka Ghana kuziba nafasi ya Fiston Mayele aliyesajiliwa Pyramids baada ya kutwaa Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu akifunga mabao 17 sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba na kutupia mengine saba katika Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ikifika fainali na kulikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria, lakini bado hajaonyesha makeke akiwa na bao moja tu la ligi na jingine la mechi za CAF.

“Usimuone anacheka, huyu kocha huku kambini ni mkali sana. Hataki watu wazembee pia anapenda wote wawe na usawa,” kilieleza chanzo hicho kilichoongeza;

“Tayari amewaonya wasiofanya vizuri, anaweza kuwatema kwenye dirisha dogo lijalo kwani ana mpango wa kusajili straika mpya na wachezaji wengine kama wawili hivi.”

Mapema Gamondi alikaririwa na Mwanaspoti, anataka wachezaji walio tayari kuipambania Yanga na kufikia malengo.

“Kila mchezaji ana umuhimu ndani ya timu lakini nataka kuona wote wanakuwa sawa na kupambania malengo ambayo tumejiwekea kwa kadiri wawezavyo,” alisema Gamondi aliyeipeleka Yanga hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 25.

Mechi tano za ligi zijazo ambazo huenda Gamondi atakuwa akifanya mabadiliko ya wachezaji kwa kumpa kila mmoja nafasi ili kuwapima wachezaji hao waliwatega ni ile ya Azam itakayopigwa Oktoba 25,kisha, Singida Big Stars, Simba, Coastal Union na Mashujaa, mbali na mechi za Ligi ya Mabingwa zinazoanza Novemba 25.

SOMA NA HII  KIPA LA SIMBA 'LAJITIA KITANZI' MBEYA CITY...ISHU NZIMA IKO HIVI....