Home Habari za michezo ROBERTINHO AMKINGIA KIFUA NGOMA

ROBERTINHO AMKINGIA KIFUA NGOMA

Habari za Simba

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameweka heshima kwenye soka la Tanzani hadi sasa akiiongoza timu hiyo kwenye mechi 16 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza mchezo wowote, huku akikiri kukunwa na kiwango kinachoonyeshwa na kiungo Fabrice Ngoma akisema anakuja mdogo mdogo.

Ngoma ni miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa kwenye dirisha lililofungwa Agosti 31 akitokea Al Hilal ya Sudan na amekuwa akitumiwa mara kwa mara na Kocha Robertinho sambamba na Mzamiru Yassin au Sadio Kanoute na kocha huyo Mbrazili amesema nyota huyo ameanza kurudi kwenye utamu wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Robertinho alisema tofauti na wakati anafika kwa sasa Ngoma ameimarika na kuwa sehemu kubwa ya utulivu wa kikosi chake kikiwa kimeshinda mechi tano za kwanza kwenye ligi.

Kocha huyo alisema Ngoma amekuwa muhimu kuifanya timu kucheza bila presha ambapo utulivu wake eneo la katikati ya uwanja umekuwa na mchango mkubwa.

“Wakati anafika alihitaji kuzoea kidogo, lakini sasa nadhani mnamuona anaonyesha ubora wake mkubwa, ni mtu muhimu kwetu pale katikati ya uwanja,”alisema Robertiunho.

“Nataka timu icheze bila presha na hili limefanikiwa, isingekuwa rahisi kucheza hivi kama tungekosa mtu mwenye utulivu kama Fabrice anajua afanye kipi kwa wakati gani awe wapi ili kuipa timu utulivu.”

Aidha Robertinho aliongeza kuwa kiungo huyo Mkongomani amemkosha zaidi kutokana na ubora wake wa kusambaza mipira kwa kupiga pasi za aina mbili.

“Napenda anavyojua kupiga pasi ndefu zinazotufanya tuharakishe kufika lango la wapinzani lakini pia anajua kupiga pasi fupi, nadhani kama ataendelea hivi Simba itazidi kuimarika.”

Simba inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 15 baada ya michezo mitano, ikishinda michezo yote mitano ya kwanza.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA SIMBA SAFARINI KUELEKEA MOROCCO...WATUMIA MBINU HII KUWACHANGANYA WAARABU