Home Habari za michezo FT: GEITA 0-3 YANGA…..AZIZI KI AWAONYESHA ‘VIPOFU’ NJIA…

FT: GEITA 0-3 YANGA…..AZIZI KI AWAONYESHA ‘VIPOFU’ NJIA…

Geita vs Yanga

SHOO imerudi tena baada ya Yanga jioni hii kuendeleza ubabe dhidi ya Geita Gold kwa kuifumua mabao 3-0 katika pambano tamu la Ligi Kuu Bara lililopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa.

Yanga imeibuka na ushindi huo ambao unakuwa wa tano mfululizo katika Ligi Kuu dhidi ya Geita kwa mabao yaliyofungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 44 akitumia vyema pasi ya Yao Kouassi, Stephane Aziz KI aliyefunga la pili dakika ya 45 akimalizia krosi ya Maxi Nzengeli, huku la tatu likipachikwa wavuni na Maxi Nzengeli dakika ya 67.

Wachezaji hao watatu walionyesha kiwango bora na mwendelezo mzuri msimu huu, wapiga shoo ya maana na kung’ara kwenye mchezo huo wakifunga mabao na kutoa assisti za mabao kwa wenzao.

Mtanange huo umekuwa wa upande mmoja Yanga ikitawala kwa dakika zote 90 wakati Geita Gold ikijihami kwa kujilinda, ambapo kipindi cha pili wenyeji waliwatoa Tariq Seif, Tariq Simba, Brown Mwankemwa na George Sangija na kuwaingiza Seleman Ibrahim, Yusuph Athuman, Yusuph Mhilu na Abeid Athuman.

Awali nahodha wa timu hiyo, Elias Maguri alitolewa dakika tu ya mchezo baada ya kuumia aliporuka juu akichuana na Bakar Mwamnyeto na alipoenda kutibiwa hakurudi tena.

Yanga iliwapumzisha Clement Mzize, Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Kouassi Yao na Mudathir Yahya huku nafasi zao zikichukuliwa na Hafiz Konkoni, Denis Nkane, Kenedy Musonda, Nickson Kibabage na Gift Fredy.

Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 12 baada ya kucheza mechi tano ikikamata nafasi ya pili, huku Simba inayocheza kesho ikikamata nafasi ya tatu na alama 12 wakati Azam FC ikiwa kileleni kwa pointi 13.

Hizi ni dondoo za mchezo huo

Nahodha wa Geita Gold, Elias Maguri ameshindwa kumaliza mchezo huo baada ya kupata majeraha na kushindwa kuendelea kufuatia kugongana na Bakari Mwamnyeto wa Yanga dakika ya 15, ambapo nafasi yake imechukuliwa na Valentino Mashaka.

Huu ni mchezo wa saba timu hizo kukutana katika mashindano yote, zikiwemo mechi mbili za Kombe la Shirikisho la Azam na tano za Ligi kuu Bara.

Katika mechi hizoza Ligi, Yanga imeshinda zote ikifunga jumla ya mabao tisa na kuruhusu moja pekee.

Katika mechi saba za mashindano yote, Yanga imepata kadi tano za njano huku Geita Gold ikipata kadi 17 za njano na nyekundu moja.

Huu ni mchezo wa tatu wa Ligi Kuu timu hizo kukutana katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, ambapo katika mechi hizo Yanga imeshinda zote na kufunga mabao matano.

Geita haijafunga bao lolote katika mechi tatu za ligi ambazo imecheza na Yanga katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza ikiruhusu mabao matano.

Pacome Zouazoua amefunga mabao ya kwanza ya timu yake katika mechi mbili mfululizo, ambapo alifunga dhidi ya Ihefu dakika ya 4 na amefunga tena leo mbele ya Geita Gold dakika ya 44, huku bao hilo likiwa ni la tatu kwenye ligi msimu huu.

Baada ya kipigo cha leo, Geita Gold imepoteza mchezo wa tatu wa ligi mfululizo ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar, 2-1 na KMC na 3-0 dhidi ya Yanga.

Geita Gold inakamata nafasi ya 12 kwenye msimamo ikiwa na pointi nne katika mechi tano, huku ikicheza mechi tano, ikishinda moja, sare moja na kupoteza tatu ikifunga mabao mawili na kuruhusu sita.

Mvua ya ghafla imenyesha jijini hapa kuanzia saa 10:42 jioni na kukatika dakika ya 45 wakati ambao Yanga imefunga mabao mawili ya haraka.

SOMA NA HII  WAKATI WATU WAKIMSIFIA KWA KUFUNGA...TAMBWE APINDISHA MDOMO KISHA AKASEMA HAYA KWA MAYELE...