Home Habari za michezo GAMONDI AFUNGUKA HAYA MALIPO UBINGWA PAWEKWA WAZI

GAMONDI AFUNGUKA HAYA MALIPO UBINGWA PAWEKWA WAZI

Kikosi cha Yanga juzi hakikulala jijini Mbeya, kwani mara baada ya kupoteza mabao 2-1 mbele ya wenyeji wa Ihefu, ikiwa ni mara ya pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara, ilipaa kurudi Dar es Salaam na jioni ya jana wakatua Mwanza. Kocha wao ametumia dakika saba tu kuwatuliza wachezaji.

Yanga ilikumbana na kipigo hicho cha pili mfululizo ugenini mbele ya Ihefu, baada ya awali kufungwa mwishoni mwa mwaka jana kwenye Ligi Kuu ya msimu uliopita na juzi ikarudia tena kufungwa idadi ile ile ya mabao na kupoteza kwa mara ya kwanza mechi za ligi kwa msimu huu na kushtua mashabiki wa klabu hiyo.

Kocha Miguel Gamondi kwa kutambua kuwa hata wachezaji walipata mshtuko kwa kipigo hicho ikicheza kwa mara ya kwanza ugenini katika Ligi ilimfanya aitishe kikao cha dharura na wachezaji kisha kuzungumza nao akiwasisitizia, wameshapoteza mechi, lakini hawajapoteza taji kwani mechi bado zipo.

Gamondi amekiri hawakucheza kwa ubora anaoujua, lakini hataki wabaki kwenye huzuni na kwamba wainuke kwani hatma ya ubingwa upo kwenye mechi 26 zilizobaki.

Gamondi amesema anajua ni wapi wamekosea kwenye mchezo huo wa juzi na sasa watakuwa na siku moja pekee ya kesho kufanya marekebisho kabla ya kushuka uwanja wa ugenini tena kucheza na Geita Gold kesho Jumamosi.

Mechi hiyo ya raundi ya tano itapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza huku rekodi zikiibeba Yanga mbele ya wenyeji wao hao ambao hadi sasa wamekusanya pointi nne ikiwa nafasi ya 10.

Amesema kikosi hicho bado kipo kwenye njia kuu ya malengo na kwamba ubingwa walionao watautetea kwa kuzitumia mechi 26 zilizobaki ambazo alitaka kila mchezaji kujipanga vema na kuepuka makosa ambayo yanaweza kuwatibulia mipango.

“Nimewaambia wachezaji waachane na matokeo ya mechi ya juzi, imeshapita tunatakiwa kuangalia tumefanya makosa gani na tutayasahihisha vipi,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Hatuna muda wa kutosha kusema tutapata wakati mzuri wa kufanya marekebisho makubwa, tutakuwa na siku ya kesho pekee (leo) kuangalia kipi tutakifanya. Tuna mechi 26 ambazo tunatakiwa kuzitumia kutafuta ushindi ili tubaki kwenye malengo yetu ya kuchukua tena ubingwa, hatutaweza kufanikiwa hapo kama tutaendelea kuangalia mechi ambayo tumeshaipoteza.”

MUSONDA FRESHI

Pia kocha huyo alifichua kilichomfanya asimtumie straika Mzambia, Kennedy Musonda ambaye hakucheza mchezo wa juzi dhidi ya Ihefu ikisema alipata maumivu kwenye mazoezi ya mwisho kabla ya kuwavaa Ihefu lakini tayari ameshakuwa sawa.

“Musonda alipata maumivu hakuweza kuwa tayari kwa mchezo nadhani maendeleo yake yako vizuri kuna uwezekano tukamtumia kwenye mechi ijayo tutaangalia huko Mwanza,” alisema Gamondi aliyeiongoza Yanga kwenye mechi 10 za mashindano yote akipoteza mbili na kushinda nane, huku akifunga jumla ya mabao 24.

SOMA NA HII  MAJANGA MKUDE AMFUNGULIA MASHTAKA MO DEWJI ADAI FIDIA KISA HIKI HAPA