Home Uncategorized SVEN – ETI NINI….NDEMLAA..!!!??

SVEN – ETI NINI….NDEMLAA..!!!??

KIPENZI cha mashabiki wa Simba, Said Ndemla, huenda akawa amejisafishia njia ya kuendelea kupangwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kutokana na kandanda alilolionyesha juzi walipovaana na Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ilishinda mabao 3-0 na hivyo kuzidi kujikita kileleni katika msimamo wa kipute hicho, ikifikisha pointi 75.

Katika kuonyesha jinsi alivyokunwa na kiwango cha Ndemla katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa kiungo huyo si wa kawaida, akiahidi kuendelea kumtumia.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Sven alisema anafahamu watu wanavyofurahi kumuona Ndemla katika ubora aliouonyesha, akitamba kuwa kiungo wake huyo ataendelea kuuwasha moto katika mechi zijazo.

“Niliwaambia wachezaji wangu wakati tunaanza mazoezi baada ya mapumziko ya corona kuwa atakayejituma mazoezini na kunionesha uwezo, atapata nafasi ya kucheza, ndicho kilichotokea kwa Ndemla na Mlilipi (Yusuf), lakini pia kwa Kichuya (Shiza) katika mchezo uliopita.

“Ndemla amefanya kile ambacho alitakiwa kukifanya kabla ya mechi, nilimwambia leo (juzi) nampa jukumu, nataka anionyeshe kuwa bado ana nafasi katika kikosi na kweli amefanya hivyo.

“Kuanzia sasa na wakati ujao, natarajia Ndemla atakuwa katika kiwango hiki hiki na namuhakikishia kupata nafasi ya kuanza katika mechi zinazokuja,” alisemakocha huyo.

Alisema kuwa amefurahi mabadiliko ya mfumo wa uchezaji aliyoyafanya kwa haraka yamepokelewa vizuri na wachezaji ndani ya siku tatu tu ambayo yamechangia kupata ushindi wa juzi.

Aliongeza kuwa kwa sasa wana mechi ngumu ambazo wanahitaji kushinda zote ili kutimiza lengo la kuwa mabingwa wa Bara kwa mara ya tatu mfululizo.

“Kila mmoja anapaswa kufanya kazi kwa asilimia zote, sio 60% wala 70% kwa sababu mwisho wa ligi, ndio bingwa anakabidhiwa kombe, kwa hiyo wakati huu bado tunahitaji kuwa makini tunapocheza ili kupata pointi tatu kwa kila mechi iliyopo mbele yetu,” alisisitiza.

SOMA NA HII  KMC YACHWAPA MABAO 3-1 NA SIMBA