Home Uncategorized MBELGIJI WA SIMBA ANAAMINI KUWA KIKOSI KIKIWA FITI WANASHINDA MECHI ZOTE

MBELGIJI WA SIMBA ANAAMINI KUWA KIKOSI KIKIWA FITI WANASHINDA MECHI ZOTE

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji, amesema anafahamu kwamba wanakabiliwa na mechi ngumu za kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara, hivyo amekuwa akiomba wachezaji wake wasipate majeraha ili washinde mechi zote.
Mbelgiji huyo ameongeza kuwa, kama wachezaji wake wakiendelea kuwa salama, atakuwa na uhakika wa kushinda mechi zao zinazokuja na kuchukua ubingwa wa ligi kuu pamoja na Kombe la FA.
“Tunacheza mechi ngumu kwa sasa za kumaliza ligi na utaona bado timu haijawa sawa, tunahitaji muda zaidi wa kuendelea kujifua wakati tunaenda kumaliza mechi zetu.

“Licha ya hivyo, lakini pia nahitaji kuona tunashinda mechi zote zilizosalia na hilo linawezekana kama nyota wangu wote wakiwa wazima.
“Pia nataka kuona tunamaliza ligi wachezaji wote wakiwa fiti bila ya kupata majeraha ya namna yoyote ile. Tunapambana kuchukua mataji ya ligi na FA, lakini kitu kikubwa ni kumaliza tukiwa tuko salama kabisa,” alimaliza Sven.

Simba imetia timu Mbeya ambapo ina mchezo wa Ligi Kuu Bara kesho dhidi ya Mbeya City iliyo chini ya Kocha Mkuu, Amri Said.

Simba ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 75 baada ya kucheza mechi 30 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya 18 baada ya kucheza mechi 30 na kibindoni ina pointi 30.

Mchezo utakuwa mgumu kwa Mbeya City ambayo inahaha kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na Simba ambayo inataka kutangazwa mabingwa mapema.
SOMA NA HII  UKATA WAITESA MWADUI FC