Home Habari za michezo HAPA SIMBA PALE YANGA HII NDIO LIGI YA REKODI SASA

HAPA SIMBA PALE YANGA HII NDIO LIGI YA REKODI SASA

Habari za michezo

Kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita wa 2022/23, Wekundu wa Msimbazi wameendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa mara nyingine tena (2023/24) ndani ya mizunguko mitano huku safari hii wakionekana kuwa na pointi nyingi zaidi (15), tofauti na mwaka jana (13).

Ndani ya mizunguko mitano ya msimu uliopita Simba ikiwa na pointi 13 ilikuwa ikiongoza ligi kwa utofauti ya mabao kutokana na kulingana kwao pointi na Yanga ambao walitwaa ubingwa huo huku Namungo ambao msimu huu wanaonekana kuwa na mwanzo mgumu walishika nafasi ya tatu.

Tofauti na msimu uliopita kwa sasa Simba inayonolewa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ inaongoza msimamo huo kwa utofauti wa pointi mbili na Azam FC ambayo ipo nafasi ya pili, Yanga ikiwa ya tatu na pointi 12, huku ikiwa imepoteza mchezo mmoja.

Wakati makocha mbalimbali wa ligi hiyo wakiwa na hesabu za kuboresha vikosi vyao ndani ya wiki hizi mbili za mapumziko ya kimataifa hiki ni kile ambacho kimetokea katika mizunguko hii mitano ikilinganishwa na msimu uliopita ambao ilishuhudiwa maafande wa Polisi Tanzania, Ruvu Shooting na Mbeya City zikishuka daraja.

NI SIMBA NA AZAM TU

Kipindi kama hiki msimu uliopita kulikuwa na klabu tatu ambazo ni Simba, Yanga na Namungo kati ya 16 ambazo zilikuwa hazijapoteza mchezo wowote kwenye ligi ndani ya mizunguko mitano.

Simba imeendelea kuwa na mwanzo mzuri wa msimu kwa kutopoteza ndani ya mizunguko mitano huku Yanga na Namungo zikiangukia pua, kwa msimu huu imeongezeka Azam FC kwa kuwa miongoni mwa klabu ambazo bado hazijapoteza.

Msimu uliopita kulikuwa na timu sita ambazo kipindi kama hiki zilikuwa zimepoteza kuanzia michezo mitatu ambazo ni Kagera Sugar,Polisi Tanzania, Dodoma Jiji, Coastal Union, Ihefu na Ruvu Shooting.

Jinamizi la kuanza vibaya kwa kupoteza michezo mingi ndani ya mizunguko mitano limeendelea kuwatesa, Ihefu, Coastal Union na Tanzania Prisons ambao kila mmoja amepoteza mechi tatu sambamba na Mtibwa Sugar pamoja na wachimba madini wa Geita Gold.

YANGA YATONESHWA

Licha ya kwamba msimu uliopita Yanga ilipoteza dhidi ya Ihefu na ikatwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya pili mfululizo, haikuwa ndani ya mizunguko mitano ya mwanzoni mwa msimu hivyo Miguel Gamondi na vijana wake wana kazi kubwa ya kufanya mbele yao kuhakikisha wanatetea ubingwa huo.

Msimu uliopita Ihefu iliifanya Yanga kumaliza rekodi ya kucheza michezo mingi (49) mfululizo kwenye ligi bila ya kupoteza sawa na dakika 4500 kama ambavyo ilikuwa mwaka jana kwa kuchapwa mabao 2-1 ndivyo ambavyo mwaka huu yamewakuta kwenye uwanja uleule wa Real Estastes Mbarali.

Je! wataweza kutetea kama ambavyo ilikuwa mwaka jana? Tusubiri kuona nini kitatokea kuanzia mwezi wa tatu mwakani, kipindi ambacho maji na mafuta huanza kujitenga kwenye mbio za ubingwa.

SINGIDA MAJANGA

Kwa kile ilichokifanya msimu uliopita ni wazi Singida BG ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutoa changamoto zaidi msimu huu lakini mambo yanaonekana kuwa tofauti kwani ndani ya mizunguko mitano wamepata ushindi mara moja tu huku wakitoka sare na kupoteza mara mbili.

Inawezekana mabadiliko mawili ya benchi la ufundi ambayo yamefanyika ndani ya msimu mmoja na idadi kubwa ya wachezaji waliosajiliwa vimewaondoa kwenye mwelekeo mzuri waliokuwa nao.

Waliuanza msimu wakiwa na Hans van der Pluijm ambaye aliifanya timu hiyo kuwa tishio msimu uliopita lakini akatimuliwa, wakamleta Mjerumani, Ernst Middendorp ambaye aliondoka na sasa timu ipo chini ya Ramadhan Nswazurwimo huku wakiwa kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya.

WAMEPANDA NA MOTO

Msimu uliopita Ihefu ilikuwa ikiburuza mkia ndani ya mizunguko mitano ya ligi japo baadaye iliwashangaza wengi kwa kutoka mkiani na kumaliza msimu ikiwa nafasi ya sita mambo yanaonekana kuwa tofauti msimu huu kwa timu ambazo zimepanda Ligi Kuu Bara.

Tabora United, JKT Tanzania na Mashujaa zinaonekana kupanda na moto kwani ndani ya mizunguko mitano ya ligi kila mmoja amejikusanyia pointi za kutosha tu kiasi cha kuwa miongoni mwa timu saba za juu.

Hadi sasa Mashajaa na Tabora zimevuna pointi nane wapo kwenye nafasi ya tano na sita huku JKT Tanzania ikiwa na pointi saba nyuma yao.

UKUTA CHUJIO

Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar ndio timu ambazo zinaonekana kuwa na ukuta dhaifu kwenye ligi ndani ya mizunguko mitano ya ligi kwani wana wastani wa kuruhusu mabao mawili kwenye kila mchezo.

Prisons imeruhusu mabao 11 huku Mtibwa ikifungwa mabao 10, kwa msimu uliopita hakuna timu ambayo ilikuwa na wastani wa kuruhusu mabao kuanzia mawili ndani ya michezo mitano ya ligi.

HAWAJAPATA USHINDI

Wakati mashabiki wa Simba, Yanga na Azam wakifurahia zaidi ushindi kwa timu zao kwenye michezo mingi ya ligi, mambo ni tofauti kwa Coastal Union ya Tanga, Namungo ya Lindi na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Bado timu hizo ambazo zipo chini kwenye msimamo wa ligi hazijaonja ladha ya ushindi ni kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita kwa Ihefu, Kagera Sugar na Polisi Tanzania.

MTAMBO WA MABAO

Ni Matteo Anthony tu wa Mtibwa Sugar ambaye anaonekana kuanza kwa moto kama ilivyokuwa msimu uliopita akiwa na KMC ndani ya mizunguko mitano ya ligi.

Mshambuliaji huyo tayari amecheka na nyavu mara tatu, msimu uliopita kipindi kama hiki alikuwa na mabao manne kwenye orodha ya wafungaji iliyokuwa ikiongozwa na Reliants Lusajo wa Namungo aliyekuwa na mabao matano.

Msimu huu ni Jean Baleke ambaye anaongoza orodha hiyo akiwa na mabao matano, mshambuliaji huyo anaonekana kuendelea pale alipoishia msimu uliopita, alikuwa mmoja wa wafungaji hatari kwenye ligi.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo, raia wa Senegal anafurahishwa na mwenendo wa timu yake licha ya mapungufu kadhaa ambayo yamekuwa yakijitokeza na wamekuwa wakikabiliana nayo kama benchi la ufundi.

“Bado tunategemea kukutana na upinzani mkali zaidi mbele ya safari kwa sababu kadiri mechi zinavyosogea ndivyo ushindani unaweza kuongezeka, tunatakiwa kufanya vizuri kwenye kila mchezo ili kuwa na msimu mzuri,” anasema kocha huyo.

Kocha wa Mashujaa ya Kigoma, Mohamed Abdallah ‘Bares’ anaamini vijana wake wanaweza kupambana na kuifanya timu hiyo kumaliza msimu ikiwa kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

“Hizi wiki za mapumziko kwetu tumekuwa tukizitumia kujiweka sawa na kufanyia kazi mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza ili mechi za ligi zikiendelea tuwe bora zaidi, nitafurahi kama nitaifanya timu kumaliza katika nafasi za juu,” anasema Bares.

Kwa upande wake kocha wa Simba, Robertinho anasema,”Simba siku zote ipo kwa ajili ya kushinda, tumekuwa tukiupa uzito mchezo mmoja hadi mwingine na ndio maana tumekuwa na mwanzo mzuri wa msimu kwa kushinda michezo yote mitano, bado tunaendelea na safari.”

Abdihamid Moallin wa KMC ambaye ni kocha bora wa Ligi Kuu Bara kwa mwezi uliopita, anasema, “Msimu umekuwa na panda shuka nyingi ambacho tunapambana ni kuhakikisha tunakuwa kwenye mwenendo mzuri wa matokeo.”

SOMA NA HII  HUENDA YANGA IKAWA NDIO TIMU YA KWANZA KWENYE REKODI HII BONGO