Home Habari za michezo KWA HALI HII YA BOCCO, HAWA JAMAA WATASUBIRI SANA

KWA HALI HII YA BOCCO, HAWA JAMAA WATASUBIRI SANA

Habari za Simba SC

Mashabiki wa Simba wanaonekana kumchoka nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kiasi cha kufikia hatua ya kumrushia chumba uwanjani, lakini kwa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ mambo ni togfauti, kwani amesema anataendelea kumpanga mkongwe huyo, huku Jean Baleke na Moses Phiri wakisubiri benchi.

Bocco aliyeendeleza rekodi yake ya kufunga katika misimu mfululizo akiifikia rekodi ya staa wa zamani wa kimataifa wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ya kuwa mfungaji wa muda wote katika Ligi Kuu Bara.

Straika huyo juzi alifunga bao la pili la Simba wakati ikiichapa Tanzania Prisons kwa mabao 3-1, likiwa ni bao la 153 kwake tangu aanze kucheza katika ligi hiyo mwaka 2008 ikiwa ni misimu 16 na kuifikia rekodi ya Mmachinga ya kufunga idadi ya mabao hayo katika misimu 13 tu akiwa na timu nje.

Akizungumza nasi jana, kocha Robertinho alisema ameiona hali ya mashabiki wa klabu hiyo kutomkubali Bocco, ila kwa mtazamo wake bado ni mshambuliaji bora anayeweza kucheza kwa maelekezo na kuisaidia timu, hivyo hawezi kumuacha nje kizembe.

Mbrazili huyo alisema Bocco pekee amekuwa akifanikiwa kucheza kwa maelekezo yake kwa kutumia muda mwingi kukaa ndani ya eneo la wapinzani faida ambayo imewapa nafasi ya timu hiyo kufunga mabao.

“Sikiliza, ni kweli naiona hiyo hali, mashabiki waje uwanjani kuangalia Simba inacheza mpira vizuri. Kwangu Bocco bado ni mshambuliaji mzuri kwani anakwenda kufanya kile ninachokitaka afanye,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Hata katika mechi dhidi ya Dynamos (Power) aliingia akafanya nilichotaka tukapata bao lililosaidia kutuvusha makundi na leo (juzi) nimempa nafasi ya kuanza amefunga tena, lakini akawafanya mabeki wa Prisons kwa muda mwingi kubaki nyuma, nataka mshambuliaji wa aina hii anayekaa muda mrefu eneo la hatari la wapinzani na hili ndicho anafanya Bocco huyu bado ni bora kwangu.”

Kocha huyo alisema anao washambuliaji wengine kama Jean Baleke na Moses Phiri ambao nao ni wazuri kwa kukimbia pembeni lakini wamekuwa hawajaweza kucheza kwa nidhamu kama anavyofanya Bocco.

“Simba tunajivunia kuwa na washambuliaji wengi wazuri, kwa Baleke na Phiri angalieni tu, muda mwingi wanataka kukimbia pembeni hili linatufanya kushindwa kutumia vizuri nafasi tunazotengeneza tunaendelea kuwaongezea ubora huo na wao ili wacheze kama Bocco.

“Nimezungumza na Bocco nimemwambia aachane na mambo ya mashabiki anisikilize mimi kama kocha wake, mashabiki wanataka ushindi hesabu zetu ndio zitakazowapa furaha, unaona amefunga wamenyamaza nataka aendelee kufanya hivyo hivyo kila mara kwani nitaendelea kumtumia,” alisisitiza Robertinho aliyefikisha jumla ya mechi 15 bila kupoteza katika Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  YANGA: MBINU ZA EYMAEL ZIMEJIBU, MASHABIKI WANASTAHILI PONGEZI