Home Habari za michezo KWA HILI UNAWEZA KUSEMA OKTOBA NI MWEZI WA YANGA

KWA HILI UNAWEZA KUSEMA OKTOBA NI MWEZI WA YANGA

Geita vs Yanga

Ligi Kuu Bara inaendelea leo ambapo macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini yataelekezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Yanga itakapowakaribisha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, huku Oktoba ukiwa mwezi wa Wanajangwani.

Mchezo huu utakaopigwa saa 12:30 jioni unatazamiwa kuleta upekee kwani timu itakayoshinda itaongoza ligi ambapo Yanga itafikisha pointi 15 sambamba na Simba ingawa zitatofautiana zaidi kwenye michezo na mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam ambayo haijapoteza mchezo kati ya mitano iliyocheza, ikishinda itafikisha pointi 16 na kukwea kileleni jambo ambalo linaongeza ushindani mkali kwa miamba hii wakati itakapokuwa inapambana leo.

MECHI YA 31

Huu ni mchezo wa 31 kwa timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu Azam FC ilipopanda rasmi Julai 27, 2008, baada ya kuifunga Majimaji ya Songea mabao 2-0, Uwanja wa Jamhuri Dodoma na Yanga imeshinda 12, sare tisa na kupoteza tisa.

MCHEZO WA KISASI

Mchezo huu ni wa kisasi zaidi kwa Azam kwani mara ya mwisho ilipokutana na Yanga ilikuwa ni Agosti 9, mwaka huu katika Kombe la Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali na kufungwa 2-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Kama haitoshi katika Ligi Kuu Bara mara ya mwisho Azam ilipoteza kwa 3-2, mechi iliyochezwa Desemba 25 mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mabao yaliyofungwa na Fiston Mayele, Stephane Aziz KI na Farid Mussa.

Mabao mawili ya Azam katika mchezo huo yalifungwa yote na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Abdul Suleiman ‘Sopu’ dakika ya 27 na 47.

OKTOBA YA YANGA

Tangu miamba hii ilipoanza kukutana 2008, huu ni mchezo wa saba wa Ligi Kuu Bara kuchezwa Oktoba, Yanga imeshinda miwili na kutoka sare minne kati ya sita iliyopita huku Azam haijaonja ladha ya ushindi katika mwezi huo.

Mchezo wa kwanza kabisa ulikuwa Oktoba 15, 2008 ambapo Yanga ilishinda 3-1 wa mwisho ulikuwa ni wa Oktoba 30, 2021 na Yanga ilishinda 2-0, kwa mabao yaliyofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Fiston Mayele na Jesus Moloko.

MECHI ZA MABAO MENGI

Tangu zimeanza kukutana ni michezo mitatu tu ambayo imezalisha mabao mengi, matano (5) huku Azam FC ikishinda miwili ikianza na 3-2 Aprili 8, 2009 kisha 3-2 Septemba 23, 2013 huku Yanga ikishinda mara moja kwa mabao 3-2, Desemba 25 mwaka jana.

BOCCO MBABE WAO

John Bocco ni mmoja kati ya washambuliaji watakaozidi kukumbukwa kwenye kikosi cha Azam kutokana na mchango wake ndani ya timu hiyo aliyodumu nayo kwa miaka 10 kabla ya kujiunga na Simba Julai 2017 anakokipiga hadi sasa.

Bocco anashikilia rekodi kwa nyota wa Azam FC anayeongoza kuifunga Yanga mabao mengi ambapo hadi anaondoka alifunga mara 10 akifuatiwa na Daniel Amoah na Abdul Suleiman ‘Sopu’ wenye mawili kila mmoja na wawili hao bado wanaendelea kuichezea timu hiyo.

FEI TOTO, BANGALA MTEGONI

Nyota wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yannick Bangala watakuwa katika mtihani mwingine kwa mashabiki wa timu hiyo wa kudhibitisha uwezo wao wakati watakapokuwa wanacheza na Yanga timu ambayo ndiyo waliyotokea kabla ya kujiunga nayo msimu huu.

‘Fei Toto’ mwenye mabao manne ya Ligi Kuu Bara ndiye mwenye uhakika zaidi wa kucheza kutokana na ufiti aliokuwa nao huku kwa Bangala akitegemea hali yake ya kiafya baada ya kuchanika msuli wa nyama za paja katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji Oktoba 3.

KAULI ZA MAKOCHA

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo alisema Yanga ni timu bora ambayo wanaiheshimu kwa kiasi kikubwa ila wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo wowote wa ligi.

“Sio rahisi unapocheza na timu kama Yanga kwa sababu ina wachezaji wazuri ambao tayari wameonyesha ubora mkubwa msimu huu, hivyo kwetu ni kipimo sahihi cha kuonyesha ni kwa jinsi gani tunahitaji kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema licha ya kuwaheshimu wapinzani wao kutokana na ubora waliokuwa nao msimu huu lakini malengo yao makubwa ni kupata pointi tatu ambazo zitazidi kuwatengenezea mazingira mazuri mbeleni.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA YANGA KINAZIDI KUMEGUKA.....WENGINE WAWILI KUONDOKA