Home Habari za michezo MAXI MZUKA KIBAO KUELEKEA DABI YA KARIAKOO

MAXI MZUKA KIBAO KUELEKEA DABI YA KARIAKOO

Habari za Yanga

Yanga iko kambini kwaajili ya maandalizi ya kukutana na watani wao wa jadi Simba, kiungo wao Maxi Nzengeli amepata mzuka wa aina yake haswa kutokana na kiwango chake cha sasa huku akisema mechi ya Jumapili itanoga.

Mabosi wa Yanga mara baada ya kiungo huyo kupiga mabao mawili kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Singida Big Stars wakamfanyia jambo kwa kumpa zawadi ya Gari ili kumpandisha mzuka zaidi wa dabi.

Maxi kuanzia juzi anatembelea gari hiyo aina ya Toyota Crown iliyotolewa na mabosi wa klabu hiyo kwa kiwango ambacho amekiendelea kukionyesha huku ikielezwa kuwa pia ilikuwa ni sehemu ya makubaliano ya pande hizo mbili.

Amezungumzia mechi dhidi ya Simba na kusema ni miongoni mwa mchezo wenye presha na mgumu kwani zinakutana timu kubwa zenye ushindani na ubora hivyo macho ya watu yanatamani kuona nini kitakwenda kutokea na wao wamejipanga kufanya jambo.

“Huu ni mchezo mkubwa utakaotazamwa sana hivyo kila mchezaji anatakiwa kucheza kwa juhudi kubwa na morali ili kuweza kufanikiwa katika mechi hiyo yenye ushindani mkubwa,”alisema Maxi huku akionyesha kuwa na ari ya mchezo huo ambao Simba ni wenyeji.

“Wachezaji wa pande zote ni bora na hatutacheza wote hivyo kazi kubwa itakuwa kwa wale watakaopangwa kwani kazi yao ni kujituma na kufanya timu iwe kwenye nafasi nzuri katika ligi na kupata matokeo,”alisema Maxi.

Maxi ambaye ameanza kutumikia kikosi hicho msimu huu akitokea Meniema FC ya DR Congo amekuwa ni miongoni mwa wachezaji wageni ambao wameendana na mfumo wa kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi ambaye amekuwa akimpa uhuru wa kucheza namba nyingi uwanja kadri mchezo unavyokwenda.

Maxi ambaye licha ya uwezo wake uliompa nafasi ya kuchezea kikosi cha kwanza, amekuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao matano na kutoa asisti mbili mpaka sasa Yanga ikiongoza Ligi kwa pointi 18, ilizopata katika michezo saba ambayo hawajaonja sare.

Katika mechi saba amecheza dakika 489 huku akitoa asisti kwenye mchezo dhidi ya Geita na KMC na kufunga mabao mawili dhidi ya JKT Tanzania na mawili Singida Big Stars na bao moja dhidi ya Geita. Amekuwa akitumika kama mshambuliaji na winga wa pembeni na kote amekuwa akitendea haki na kuonyesha madhara.

Maxi ambaye anazungumza Kifaransa, Kingereza na Kiswahili kwa mbaali alisema anafurahia kiwango chake ijapokuwa anatamani kuongeza juhudi ili kuwa na mwendelezo wa kuwa na rekodi nzuri ukizingatia ligi ndio kwanza imaaza.

SOMA NA HII  BAADA YA KUTOLEWA LIGI YA MABINGWA...MBRAZILI SIMBA ATAKA MBADALA WA CHAMA NA BALEKE...