Home Habari za michezo KUELEKEA SIMBA vs YANGA….UTAMU WOTE WA ‘SHOW’ UKO HAPA….

KUELEKEA SIMBA vs YANGA….UTAMU WOTE WA ‘SHOW’ UKO HAPA….

Habari za michezo

MACHO na masikio yote ya mashabiki wa soka nchini kwa sasa yameelekezwa katika mchezo mkali na wa ‘Derby ya Kariakoo’ utakaozikutanisha Simba itakayokuwa wenyeji wa Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili hii ya Novemba 5, unaweza kujiuliza itakuwaje? kwa kuwa rekodi Jumapili zipo upande wa Simba.

Mchezo huo utakaopigwa saa 11:00 jioni unavuta hisia kali kwa mashabiki wa timu hizo kutokana na uhasama uliojengeka tangu miaka ya nyuma huku ikiwa ni miongoni mwa ‘Derby’ kali tano Barani Afrika zinazotajwa kufuatiliwa na watu wengi.

Timu hizo zinakutana zikiwa na matokeo tofauti tangu msimu huu kuanza ambapo kwa wenyeji Simba wameshinda michezo yake yote sita ya Ligi Kuu Bara iliyocheza huku kwa upande wa Yanga ikipoteza mechi moja tu kati ya saba ilizocheza.

Wakati mashabiki wakisubiria mchezo huu ila unapaswa kutambua rekodi zinaibeba zaidi Simba inapokutana na Yanga siku ya Jumapili kwani tangu 1965, Ligi Kuu Bara ilipoanza huu utakuwa ni mchezo wa 37 siku hiyo huku kiujumla ukiwa ni wa 111 kukutana.

Katika michezo 36 iliyopita timu hizo zilipokutana siku ya Jumapili, Simba imeshinda 10 wakati Yanga imeshinda saba huku 19 ikiisha sare.

Licha ya Simba kuonekana mbabe siku hiyo ila Yanga ndio timu ya kwanza kushinda mchezo uliochezwa Jumapili kwa sababu ilifanya hivyo Juni 18, 1972, iliposhinda kwa bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Leonard Chitete.

Mchezo wa kwanza kwa timu hizo kuchezwa Jumapili ulipigwa Juni 4, 1972 na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 ambapo Simba (Sunderland) ilifunga kupitia kwa, Willy Mwaijibe dakika ya 11 tu kisha Kitwana Manara kuisawazishia Yanga dakika ya 19.

Simba ndiyo timu pekee ambayo inaongoza kuwa mwenyeji mara nyingi siku ya Jumapili dhidi ya wapinzani wao ambapo mchezo huu ujao pia utaifanya kufikisha jumla ya michezo 22 jambo ambalo linawafanya mashabiki waamini Simba siku yao ni Jumapili na Yanga ni Jumamosi, huku kwa upande wa Yanga ikiwa imefanya hivyo kwa mara 15, tu tangu 1965.

Mchezo wa kwanza kabisa wa Ligi Kuu Bara kwa timu hizi kukutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikuwa ni Oktoba 26, 2008 ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lililofungwa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Ben Mwalala dakika ya 15.

Hata hivyo, mechi ya mwisho kwa timu hizi kukutana siku ya Jumapili katika Ligi Kuu Bara ilikuwa ni Aprili 16, mwaka huu ambapo Simba iliendeleza ubabe kwa kushinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Henock Inonga dakika ya 2 na Kibu Denis dakika ya 32.

Kama haitoshi mara ya mwisho miamba hii kukutana ilikuwa Agosti 13, mwaka huu katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga ambapo Simba ilishinda kwa penalti 3-1, baada ya dakika 90 kuisha bila mbabe.

REKODI YA KIPEKEE SIMBA

Ushindi wa juzi ilioupata Simba wa mabao 2-1, dhidi ya Ihefu umemfanya kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kufikisha jumla ya michezo 17 ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza kuanzia msimu uliopita wa 2022/2023 na huu wa 2023/2024, huu utakuwa mchezo wa pili wa Ligi Kuu Robertinho anakutana na Yanga, akiwa alishinda 2-0 msimu uliopita, lakini ni wa pili kwa ujumla akiwa alishinda kwa penalti 3-1 kwenye Ngao mwanzoni mwa msimu.

Katika michezo hiyo, Robertinho ameshinda 15 huku miwili pekee ikiisha sare tangu alipoanza kuifundisha Simba Januari 3, mwaka huu. Mbali na rekodi hiyo ya Robertinho ila ushindi huo kwa Simba ilioupata umeifanya kufikisha jumla ya michezo 29 ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Azam FC bao 1-0, Oktoba 27, 2022, lililofungwa na Prince Dube.

Katika michezo hiyo 29, ambayo Simba imecheza bila kupoteza wowote imeshinda 24 huku mitano pekee iliyosalia ikiisha kwa sare.

KAULI YA ROBERTINHO

Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akizungumzia kuhusu mechi dhidi ya Yanga alisema ni mapema sana kuuzungumzia ingawa wao kama benchi la ufundi, wachezaji na viongozi wanatambua umuhimu wa kushinda mchezo huo.

MOTO WA YANGA..

Kwa upande wa Yanga imeonekana kuwa tishio msimu huu katika upatikanaji wa mabao kwani katika michezo saba iliyocheza imefunga 20 huku ikiruhusu nyavu zake kutikishwa mara nne tu.

Mbali na hilo ila mastaa wa timu hiyo Stephane Aziz Ki ndiye kinara wa mabao kwani amefunga sita na Jean Baleke wa Simba huku Maxi Nzengeli akifuatia akiwa na matano hadi sasa.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi huu utakuwa ni mchezo wake wa kwanza msimu huu kukutana na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wa Simba katika Ligi Kuu Bara tangu alipojiunga na kikosi hicho, Julai mwaka huu na faida kubwa aliyonayo ni kwamba ameshakwenda kwenye Uwanja wa Mkapa mara mbili kuitazama Simba ikicheza, alikwenda kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly, lakini akaenda kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Ihefu, hivyo atakuwa ameshaisoma timu hiyo kwa dakika 180 ikiwa uwanjani.

SOMA NA HII  SIMBA YALETA STAILI MPYA CAF...MORRISON APEWA MECHI MBILI TU...SAIDO ACHONGEWA KWA NABI...

1 COMMENT