Home Habari za michezo SIMBA vs AL AHLY KESHO….MBRAZILI AANDA SUB HII YA KUMALIZA MCHEZO MAMBO...

SIMBA vs AL AHLY KESHO….MBRAZILI AANDA SUB HII YA KUMALIZA MCHEZO MAMBO YAKIWA MAGUMU..

Habari za Simba

WAKATI wapinzani wao, Al Ahly ya Misri, wakiwa tayari wameshatua nchini kwaajili ya mchezo wa ufunguzi wa African Football League, Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema ameshakiandaa kikosi chake kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa Ijumaa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa huku akitamba kuwa na ‘supa sub’ ya kuweza kubadili matokeo kipindi cha pili.

Simba na Al Ahly, Kesho Ijumaa watakata utepe katika michuano hiyo inayoshirikisha klabu nane bora barani Afrika, zingine zikiwa ni Wydad Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Esperance Tunis (Tunisia), Petro Atletico de Luanda (Angola), Enyimba FC (Nigeria) na TP Mazembe (DR Congo).

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Robertinho alisema kikosi chake kiko tayari kuwavaa Mabingwa wa Afrika, lakini yeye kama mwalimu ni lazima achague nani wa kuanza na kwa sababu gani, lakini ana kazi ya kuchagua wale ambao watasubiri ili kuingia kipindi cha pili kwa ajili ya kubadilisha mbinu, kusaidia wenzao watakapokuwa wamechoka au tatizo lolote litakalijitokeza.

“Kila kitu kiko tayari hapa kilichobaki ni kuchagua nani wa kuanza, kikosi gani nianze nacho na wachezaji gani wa kukaa benchi kwa ajili ya kusubiri wenzake, kwa mfano kwa sasa ninaye mchezaji wangu ambaye namtegemea sana akiingia kipindi cha pili na anabadilisha mchezo, Luis (Miquissone), unajua aliumia, kwangu mimi ni muhimu sana.

“Natarajia tutakuwa na mechi ngumu, lakini tumejiandaa, siku zote mpira si jambo la siri, tumejiandaa kucheza vizuri na kushinda ndiyo malengo yetu, nimeona watu wengi hawasemi tena jina langu ni Robertinho badala yake wananiita Mr. Objective na wataona siku hiyo waje kwa wingi uwanjani,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.

Simba inakwenda kucheza na Al Ahly kwenye ufunguzi wa michuano hiyo ikiwa na rekodi ya kuifunga kwenye mechi zote tatu ambazo imewahi kukutana nayo hapa nchini, lakini hushindwa kufanya hivyo ikiwa ugenini.

Hata hivyo, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, ambaye jana kwa kushirikiana na wanachama na mashabiki wa timu hiyo walikuwa na kazi moja tu ya kuipamba Dar es Salaam kwa mabango kuelekea mechi hiyo ya ufunguzi, amesema kwa sasa Simba kuifunga Al Ahly siyo stori tena, badala yake safari hii wanataka kuiondosha kwenye mashindano.

Mara ya kwanza zilikutana mwaka 1984 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwenye Kombe la Washindi barani Afrika (sasa Kombe la Shirikisho), Simba ikishinda mabao 2-1, yaliyowekwa kwenye kamba na Zamoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani, lakini ikaenda kutolewa Cairo nchini Misri kwa kufungwa mabao 2-0.

Zilikutana tena Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi 2019, Simba ikishinda bao 1-0 la Meddie Kagere, na hii ni baada ya kufungwa mabao 5-0 jijini Cairo, 2021 zilikuwa tena kundi moja la Ligi ya Mabingwa Al Ahly ikifa tena kwa mara nyingine kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa bao 1-0 lililotiwa nyavuni na Miquissone ambaye baadaye alinunuliwa na timu hiyo, lakini kwa sasa amerejea tena Simba na atakuwapo Ijumaa.

Katika mechi ya marudiano nchini Misri 2020, Simba ilionesha ukomavu baada ya Al Ahly nayo kushinda kwa tabu bao 1-0.

SOMA NA HII  RUVU SHOOTING YAINGIA SOKONI KUSAKA MAJEMBE YA KAZI

1 COMMENT