Home Habari za michezo YANGA KWENYE VITA YA MTETEZI SIO POA

YANGA KWENYE VITA YA MTETEZI SIO POA

Habari za Yanga

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga wao wanarudi tena kwenye mechi za hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara ya pili wakiwahi kufanya hivyo mwaka 1998.

Baada ya miaka 25 Yanga wanarudi tena msimu huu wakiangukia kundi D sambamba na timu za Al Ahly ya Misri, CR Belouizdad kutoka Algeria na Medeama ya Ghana.

Yanga itafungua dimba ugenini leo dhidi ya Belouizdad ambayo hawajawahi kukutana katika historia ya mashindano ya Afrika ikiwa ni timu pekee ambayo hawakuwahi kukutana.

Mechi zao tano zilizopita Yanga ndio timu pekee ambayo imeshinda zote tofauti na wapinzani wao watatu katika kundi lao, rekodi ambayo itawapa ubora wakati wakianza mechi hizo za makundi.

Waalgeria hao hawana ushiriki mzuri wenye kutisha katika mashindano ya Afrika ambako kwao wamewahi tu kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mara nne miaka ya 2004, 2010, 2018 na 2020.

Belouizdad bado hawajatulia sawasawa wakiwa nyumbani msimu huu wakionyesha kuathirika na mabadiliko ya makocha wao mara kwa mara ambapo kwenye mechi zao tano za mwisho wameshinda tatu na kupoteza mbili.

Yanga ina rekodi nzuri binafsi ukilinganisha na Belouizdad ambapo ni msimu uliopita tu Wanajangwani walitinga fainali ya Shirikisho Afrika walipokutana na USM Alger ya huko huko Algeria wakitangulia kupoteza hapa kabla ya Wananchi kwenda kulipa kisasi kwa kushinda ugenini kisha kulikosa taji kwa kanuni tu za idadi ya mabao ya kufunga ugenini.

Yanga baada ya kuwa na ushiriki bora kwenye shirikisho msimu uliopita kikosi chao ni kama kimeanza kushika kasi ile ile ambapo msimu huu kimekuwa na ubora mkubwa kwa mashindano ya ndani na hata mechi za awali za mtoano.

Timu pekee ambayo Yanga imekutana nao mara nyingi ni mabingwa watetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa Al Ahly ambao wamekutana nao mara tano ambapo Waarabu hao wakishinda mara tatu mabingwa hao wa Tanzania wakishinda mara moja kisha kutoa sare moja.

Al Ahly ambao ni mabingwa wa Afrika mara 11 ikiwa ndio timu iliyochukua taji hilo mara nyingi, haitaweza kuidharau Yanga ikikumbuka kwamba mara ya mwisho walikutana hapa nchini ambako ndiko watakapoanzia tena walikubali kichapo cha bao 1-0.

Mwaka 1982, Yanga haitasahau kipigo kikali zaidi mbele ya Waarabu hao ambao watakutana nao kwenye mchezo wa pili wa makundi walipotoka sare ya bao 1-1 hapa nyumbani kisha ugenini kwenda kukutana na kichapo cha mabao 5-0 na kutolewa hatua ya pili ya mtoano kwa jumla ya mabao 6-1.

Msimu huu Ahly bado haijaanza kwa kasi ikishindwa kucheza fainali ya African Football League ilipotupwa nje na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini ambao ndio mabingwa wa michuano hiyo mipya.

Kwenye mechi zake tano za mwisho za mashindano, Ahly imeshinda mechi mbili na ikitoa sare mechi mbili na kupoteza moja.

Kundi hilo pia lina FC Medeama ya Ghana ambao wao wamekutana na Yanga mara moja ikiwa ni katika hatua ya makundi ya shirikisho mwaka 2016 na mchezo wa kwanza hapa nyumbani ukamalizika kwa suluhu kisha miamba hao wa Ghana kwenda kushinda kwao kwa mabao 3-1.

Yanga itaanzia ugenini dhidi ya Madeama ambayo bado haina mwendo mzuri kwenye ligi ya kwao msimu huu, kwani ndani ya mechi zake tano za mwisho imeshinda mbili na kupoteza tatu.

SOMA NA HII  MASTAA YANGA WAIPIGA MKWARA MZITO ALAHLY