Home Habari za michezo AZIZ KI AFUNGUKA WALIPOWASHIKA SIMBA

AZIZ KI AFUNGUKA WALIPOWASHIKA SIMBA

Habari za Yanga SC

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga ni wa moto kila idara lakini kwa mujibu wa takwimu mabomu ya timu hiyo kumaliza mechi yapo kwa kiungo Stephane Aziz Ki, ambaye amefichua siri ya mbinu za Gamondi kwenye kipindi cha pili dhidi ya Simba.

Msimu uliopita Yanga ilikuwa chini ya Fiston Mayele, ambaye ndiye alikuwa mwamuzi wa mchezo akimaliza msimu kwa mabao 17 ya ligi na mabao saba Kombe la Shirikisho Afrika ambapo kwenye mashindano yote aliibuka kinara.

Licha ya wachezaji wote wa Yanga msimu huu kuwa na mchango mkubwa kwenye matokeo kiungo Aziz Ki, amekuwa bora zaidi akiibeba timu hiyo kwenye mechi ngumu.

Ki alianza kufanya hivyo msimu uliopita lakini hakufua dafu kwa Mayele ambaye alikuwa wa moto na kuibeba Yanga ndani na kimataifa licha ya hayo yote aliibeba timu yake na kuivusha kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika mchezo dhidi ya Club Africain wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini.

Msimu huu Aziz Ki kwenye mechi kubwa hadi sasa amefunga mabao matatu ‘hat trick’ kwenye mchezo dhidi ya Azam ambao timu yake ilishinda mabao 3-2,mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Juzi kahusika kwenye mabao mawili kwenye dabi ya Kariakoo dhidi ya watani zao Simba ambao walikubali kichapo cha mabao 5-1 ambapo yeye alifunga bao moja na kutoa asisti ya bao moja lililofungwa na Maxi Zengeli.

Mwanaspoti limezungumza na staa huyo ambaye amefunguka kuwa mchezo wa juzi ulikuwa mgumu na wa presha kwao lakini maandalizi mazuri na kuingia kwa kuwaheshimu wapinzani ndio siri ya ushindi.

“Simba walikuwa bora tuliwazidi kimbinu na tuliandaliwa kisaikolojia kuucheza mchezo huo bila ya presha hilo lilifanikiwa kwani licha ya kusawazishiwa bao kipindi cha kwanza tuliamini bado tuna nafasi ya kuongeza mabao mengine.

“Tukiwa vyumbani tulipewa maelekezo mengine na Kocha Miguel Gamondi ambaye alitusisitiza kuendelea kupeleka mashambulizi kwa wapinzani wetu kwa kasi ili kuwapa presha mabeki wao jambo ambalo tulifanikiwa na kufanya tupate matokeo muhimu kwetu,” alisema.

Akizungumzia ubora wake msimu huu akifunga mabao saba, alisema ni kuamini katika kupambana na kujihakikishia nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa wachezaji waliopo ndani ya timu hiyo.

“Yanga imefanya usajili mkubwa dirisha kubwa la usajili hivyo ilikuwa ni lazima nipambane kuhakikisha narudi kwenye nafasi kutokana na kuwa na uzoefu ndani ya timu baada ya kucheza msimu mmoja sasa ni wa pili,” alisema Aziz Ki.

SOMA NA HII  KISA MSUVA KULIPWA BILION 1.6....FAMILIA YAKE NZIMA WAANGUKA NA KULIA...BABAKE AFUNGUKA WALIVYOMPIGANIA...