Home Habari za michezo BADI YA KARIAKOO YAZUA MASWALI MAKOCHA WAWEKEANA BIFU

BADI YA KARIAKOO YAZUA MASWALI MAKOCHA WAWEKEANA BIFU

Habari za Michezo

HAKUNA ubishi. Baada ya makelele ya siku kadhaa, umewadia ule muda wa Tanzania kugawanyika kwenye rangi mbili kubwa kwa dakika kadhaa.

Ni saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa. Ni ama mwekundu au njano. Ni mechi kubwa ya Simba na Yanga ambayo inabeba hisia za mashabiki hata wasiojua soka. Ili mradi furaha tu.

Yanga wanatamba kwa namna yoyote wanataka pointi tatu huku Simba nao wakisisitiza kitapigwa sana leo jioni. Lakini kuna uwezekano mkubwa kikapigwa kwenye mvua;

JINSI YA KUSHINDA KWENYE MVUA;

Kwa hali ilivyo Dar es Salaam na dondoo za mamlaka za hali ya hewa, mvua ipo. Mara nyingi hali hii imekuwa ni faida au hasara kwa timu yoyote uwanjani. Kuna wakati mvua imekuwa ikinyesha baadhi ya mashabiki wanafurahia kwa kuwa timu yao ina historia nzuri ya kupata matokeo hali hiyo ikitokea, lakini Mwanaspoti limegundua kuna mambo timu zote zinatakiwa kufanya leo kukabiliana na hali ya mvua uwanjani ili kupata ushindi, Simba na Yanga wafuate haya.

VIATU MAALUM…

Viatu ni muhimu sana. Kama dalili ya mvua ikiwepo viongozi wanatakiwa kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa na viatu maalumu ambavyo havitelezi. Si vile wanavyochezea kila mara. Kumbukumbu zinaonyesha, wakati fulani Simba waliwahi kununua viatu vyenye meno eneo la Karume Jijini Dar es Salaam dakika kadhaa kabla ya mechi ili kukabiliana na hali hiyo na wakashinda mchezo.

JEZI NYEPESI…

Tanzania hii haipo sana lakini baadhi ya timu Ulaya na mabara mengine wana jezi maalum ambazo huzitumia kipindi cha mvua kubwa ambazo ni nyepesi na hazinyonyi maji mengi, wataalam wanasema jezi nzito ukichezea kwenye mvua inamyima mchezaji uhuru uwanjani.

CHEZENI CHINI…

Kama leo mvua ipo, timu itakayocheza soka la chini itakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kupata ushindi kwenye mchezo huu kwa kuwa inaaminika kwenye hali hii mipira ya juu mingi imekuwa ikipotea kirahisi.

JARIBU! JARIBU!

Hali ya mvua mara nyingi huzifanya sehemu za uwanja kuteleza na kujaa maji, timu ambayo itajaribu mara nyingi ndiyo ambayo inaweza kupata ushindi kwa kuwa ni rahisi mpira kumponyoka kipa, kudunda kwenye maji na kupoteza mwelekeo, hivyo timu itakayojaribu mara nyingi, ina nafasi ya ushindi.

PASI LANGONI…

Ni rahisi kufanya makosa kama mtacheza na mpira sana kwenye lango lenu, hivyo jambo pekee ambalo mnaweza kufanya ni kuepuka kuanza mipira mingi karibu na lango lenu, au kupiga pasi nyingi jirani na lango lenu.

PUNGUZA MBIO…

Kama utakimbia na mpira ukafanikiwa kufika ni jambo zuri zaidi, lakini ikitokea unakimbia ukaupoteza itakuwa hatari zaidi kwako.

Inaaminika ni ngumu kukimbia sana kwenye hali kama hii, hivyo kama hakuna ulazima, usikimbie na mpira.

MAKOCHA…

Makocha wanashauriwa kuhakikisha wachezaji wake wanafanya maandalizi ya mechi dakika 20 zaidi ya muda wa kawaida, kwa kuwa hali hii huwafanya wachezaji kutumia nguvu kubwa zaidi uwanjani.

UMAKINI…

Mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Danny Mrwanda na sasa anacheza Ken Gold anasema “Kucheza mechi kwenye mvua kwa asilimia 80 mipango ya kocha inavurugika na ni mechi ambayo inakuwa haina mwenyewe na makipa wanakuwa wanafungwa mipira ya kizembe.

“Kuna wakati mwingine unakuwa unashindwa kupima vipimo sahihi vya pasi, unaweza ukapiga mwenzako akashindwa kuuwahi kutokana na kasi ya mpira, pia mpira unaweza ukakwama kwenye matope, hivyo kinachotakiwa ni umakini sana.”

UNAJUA MPIRA WA LIGI UNATELEZA?

Kuna dhana kuwa mpira unaotumika kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ni mzuri, lakini unateleza sana kwenye mvua hivyo umakini unatakiwa.

Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Abalkassim Suleiman amesema mpira wa Ligi Kuu wa msimu huu ni mgumu hasa wakati wa mvua kwani, unateleza sana.

“Hii ni sababu dabi inachezwa jioni kwani wachezaji wengi watakuwa na uwezo wa kucheza vizuri ila kama mvua itanyesha kazi itakuwa ngumu zaidi kwani mpira huu wa sasa unateleza sana na unahitaji mchezaji awe na uwezo mkubwa wa kuuzuia kwa kuwa upo spidi.

Kipa mwingine aliyeunga mkono hoja hiyo ni yule wa KMC Isihaka Hakimu aliitumikia Ruvu Shooting msimu uliopita, alisema kwa mara ya kwanza kuutimia mpira wa ligi huwa ni mzito sana na mchezaji akiuzoea basi hatapata shida ingawa naye alikiri unateleza kukiwa na mvua.

Amesema kipa yeyote hatamani kudaka wakati wa mvua kwani sio rahisi kuushika na inahitaji uwe bora.

“Kwenye mechi ngumu kama Dabi kipa ambaye anapewa alama nyingi za ubora ni wa upande wa Yanga (Diarra) kutokana na uzoefu alionao ijapo mchezo hautabiriki.

“Kama mvua ikinyesha ladha itapungua kwani aina ya mpira tunaoutumia kuuchezea kwenye ligi haujazoeleka na wachezaji kipindi cha mvua nafikiri utawapa taabu sana,” alisema Isihaka.

MECHI YENYEWE…

Mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo, zinathibitisha ugumu wa michezo ya watani wa jadi kwani kati ya hiyo, hakuna timu ambayo imeonekana kuwa mbabe dhidi ya mwenzake na idadi kubwa ya michezo ilimalizika kwa matokeo ya sare.

Kila timu imeibuka na ushindi mara mbili katika mechi hizo 10 zilizopita na zimetoka sare sita, Simba ikifunga mabao saba huku Yanga ikifumania nyavu mara sita, ambapo katika sare sita walizotoka, mechi tatu walitoka ngoma droo kwa mabao huku nyingine tatu zikimalizika kwa sare tasa.

Ni mechi ambayo imekuwa haizalishi idadi kubwa ya mabao katika siku za hivi karibuni ambapo kwa michezo 10 iliyopita, kumekuwa na wastani wa bao 1.3 tu kwa mechi ambapo idadi kubwa ya mabao iliyowahi kufungwa katika miaka ya hivi karibuni ni mabao 4 yaliyopachikwa katika sare ya mabao 2-2 ambayo timu hizo zilipata Januari 4, 2020.

DAKIKA TISHIO

Timu hizo kila moja imeonyesha makali ya kufumania nyavu katika muda wake ambapo Yanga wameonekana kuwa mwiba kwa safu za ulinzi za timu pinzani katika kipindi cha pili wakati Simba ni hatari katika kipindi cha kwanza.

Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, Simba imefunga mabao 16 ambapo katika kipindi cha kwanza imefumania nyavu mara 11 ikiwa sawa na asilimia 68.75 huku mengine matano sawa na asilimia 31.25 ikifunga katika dakika 45 za mwisho.

Katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, Yanga imefunga mabao 20 ambapo katika dakika 45 za pili imefunga mabao 12 sawa na asilimia 60 huku kipindi cha kwanza ikiwa imefumania nyavu mara nane sawa na asilimia 40.

Tofauti na watani wao wa jadi, safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa na uwiano sawa wa kuruhusu mabao katika kila kipindi ambapo kati ya mabao manne ambayo imeruhusu hadi sasa, mawili yamefungwa katika kila kipindi cha mchezo.

MECHI YA HESHIMA

Mbali na kiu ya kuziongoza timu zao kupata pointi tatu, kila kocha anataka ushindi katika mchezo huo ambao utakuwa na maana kubwa kwa kibarua chake ndani ya timu anayoifundisha.

Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anasaka ushindi ambao utamfanya azidi kuboresha historia yake ya kutamba dhidi ya Yanga akiwa na Simba na hata kabla hajajiunga na timu hiyo.

Mbrazil huyo amepata ushindi mara zote nne ambazo amekutana na Yanga, tatu akishinda ndani ya dakika 90 huku mara nyingine moja akipata ushindi kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi kumalizika kwa sare tasa katika muda wa kawaida wa mchezo.

Kwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi atakuwa anasaka ushindi wa kwanza dhidi ya Simba tangu alipoanza kuinoa timu yake na kabla ya hapo alipoteza kwa mikwaju ya penalti 3-1 katika mashindano ya Ngao ya Jamii yaliyofanyika Tanga, Agosti mwaka huu.

MAKOCHA SASA…

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema hana presha na mechi ya kesho dhidi ya Yanga kwani mtindo wake ni kucheza vizuri na kupata pointi tatu, lakini akisisitiza yeye ni Mbrazili. Robertinho alisema ataingia na mkakati mpya kuhakikisha anaiua Yanga kwani ana wachezaji wenye na atawatumia vizuri.

“Mpango wetu kama timu ni kushinda kila mechi, nawaheshimu wapinzani najua haitakuwa mechi rahisi lakini kesho inaweza kuwa sapraizi na wala hajali jambo lolote.” Alisema Robertinho Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema hataki timu yake ifanye makosa kwani itawaadhibu kwa kuwa wanacheza na timu kubwa. “Tumeandaa mpango wa kuhakikisha tunashinda mechi ya kesho, lakini sitaki wachezaji wafanye makosa kwa sababu inaweza kutugharimu, sisi ni timu bora, lazima tuonyesha ubora wetu kwa kuibuka na ushindi tu.” Alisema Gamondi

Ishu ya Robertinho kujiita Mbrazili inaonyesha kuwa mechi ya leo ni kati ya makocha wa nchi mbili ambazo ni mahasimu kwenye soka kati ya Brazili na Argentina anapotoka Gamondi.

REFA WA 1-0

Refa kutoka Manyara, Ahmed Arajiga ndiye aliyepangwa na kamati ya waamuzi ya TFF, kuchezesha mechi hiyo ya watani wa jadi leo.

Historia inaonyesha refa huyo amekuwa na historia tamu na chungu kwa kila timu kwani mechi mbili alizowahi kuzichezesha, kila moja imeonja kipigo mbele ya mwenzake tena ushindi ukiwa ni wa bao 1-0, zote zikiwa ni katika Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Alichezesha mechi ya fainali ya ASFC, Julai 25, 2021 mkoani Kigoma ambayo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa na Lwanga Taddeo. Mwaka uliofuata, Mei 28, Arajiga akiwa pilato wa mechi ya nusu fainali ya ASFC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Feisal Salum.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Karim Boimanda, Arajiga atasaidiwa na Mohammed Mkono na Kassim Mpanga, refa wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko huku kamishina wa mchezo akiwa ni Hosea Lugano.

Ni mechi yenye hadhi ya kimataifa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya maofisa walioteuliwa kuisimamia wengine wakiwa ni Lisobine Kisongo (daktari), Aaron Nyanda (ofisa masoko), Fatma Abdallah (ofisa protokali), Karim Boimanda (ofisa habari), Hashim Abdallah (ofisa usalama), Iman Mabrouk (mratibu wa mechi), Ramadhan Misiru (mkuu wa kituo) na Hafidh Badru (mratibu msaidizi wa mechi).

SOMA NA HII  SIMBA WAPATA PIGO.... KRAMO MAMBO SIO MAMBO, DAKTARI AANIKA UKWELI WOTE