Home Habari za michezo FUNDI MPYA WA YANGA NI BALAA NA NUSU….KAZI YAKE YA KWANZA HII...

FUNDI MPYA WA YANGA NI BALAA NA NUSU….KAZI YAKE YA KWANZA HII HAPA…

Habari za Yanga leo

Rekodi za mtaalamu mpya wa Yanga aliyetua kambini majuzi kutoka Sauzi, Mpho Maruping zinaonyesha ni mtu kwelikweli na kama ataifanya kazi kwa ufanisi, basi mashabiki wa klabu hiyo watarajie mambo makubwa hasa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi hicho kikiwa makundi.

Mabosi wa Yanga waliamua kumleta mtaalamu huyo wa kusoma mchezo (video analyst) ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mtunisia, Khalil Ben Youssef aliyekuwapo enzi za Nasreddine Nabi kabla ya kuondoka baada ya kumaliza mkataba na klabu hiyo.

Mpho, aliyezaliwa Agosti 7, 1991 katika mji wa Tembisa, Gauteng kabla ya kuanza kucheza soka tangu akiwa dogo akiitumikia nafasi ya kiungo katika klabu kadhaa ikiwamo Royal Eagles, TS Sporting, Free State Stars na Bloemfontein Celtic za Afrika Kusini, ametua nchini tangu Jumatatu akiwa na rekodi tamu kwenye sekta hiyo ya kusoma wapinzani kama alivyokuwa uwanjani akicheza kabla ya kusataafishwa na majeraha.

Mkali huyo alisoma masuala ya picha na video katika Chuo Kikuu cha Pretoria kabla ya kujikita zaidi katika uchambuzi wa mechi videoni na ukocha akianza kufanya kazi kama msaidizi wa Joel Masutha katika timu ya Pretoria Callies iliyokuwa Daraja la Pili (NFD).

Anaelezwa ni mtaalam wa kupanga mipango ya timu kuwasaidia makocha kupitia mechi mbalimbali za timu yake na hata wapinzani na alikuwa sehemu ya mafanikio ya timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini, Banyana Banyana iliyobeba ubingwa wa Afrika mwaka jana nchini Morocco.

Pia alikuwa kwenye kikosi kilichofika 16 Bora ya Fainali za Kombe la Dunia 2023 kwa kung’olewa na Uholanzi, huku akifanya kazi chini ya Akademi ya Rais wa sasa wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Dk Patrice Motsepe ya Venda Football Academy.

Mtaalamu huyo mwenye mke na watoto wawili, ameongeza mzuka kambini akifanya kazi na kocha Miguel Gamondi akiamini ataisaidia timu kufikia malengo kwenye mechi zilizoopo mbele yao hasa zile za CAF.

“Tunanaendelea na mazoezi ya uwanjani kabla ya kukaa na kuelekezana kwa kutumia video mbalimbali, kwa kushirikiana pamoja tutafanya vizuri na kufikia malengo,” kilisema chanzo kutoka Yanga kilichofichua ataisoma vema CR Belouzdad itakayocheza mechi ya Ligi Kuu ya Algeria kesho dhidi ya JS Kabylie.

SOMA NA HII  BAADA YA 'KUGEUZWA GEUZWA' JANA...KINYOONGEEE DICKSON JOB AFUNGUKA KILICHOIUA YANGA JANA..