Home Habari za michezo MASTAA KAMBI YA TAIFA STARS HAINA KUPOA

MASTAA KAMBI YA TAIFA STARS HAINA KUPOA

Taifa Stars

Nyota wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambao wapo kwenye maandalizi ya kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Niger, wameonyesha kuwa tayari kwa mchezo huo ambao utachezwa Jumamosi, Novemba 18, huku wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri ugenini.

Stars inakwenda Niger ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare na wenyeji wao hao kwenye mchezo wa mwisho kucheza nao nchini humo, Juni 4, 2022 ambao ulikuwa wa kupigania nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) wakiwa katika kundi F.

straika Saimon Msuva ambaye anaichezea JS Kabylie ya Algeria, alisema kuanza na mpinzani ambaye unamfahamu vizuri inaweza kuwa faida kwa Taifa Stars kwenye safari ya kwenda fainali za Kombe la Dunia.

“Kwanza kabisa nina furaha kuwa sehemu ya kikosi hiki. Tuna mchezo mgumu mbele yetu, lakini kama timu tunajiandaa kuhakikisha tunakuwa na mwanzo mzuri pamoja na kwamba tunaanzia ugenini, hilo siyo tatizo kabisa kwetu kwa sababu siku hizi mpira hauna cha nyumbani wala ugenini,” alisema Msuva.

“Tumecheza na Niger mara mbili nakumbuka kwenye mechi za kufuzu kwa Afcon. Wana timu nzuri japo, lakini maandalizi yetu yalitufanya kuwafunga nyumbani na kwao tulitoka sare. muda umepita na wanaweza kuwa wamebadilika, hivyo tunatakiwa kuwa bora zaidi ili kuendelea kufanya vizuri dhidi yao.”

Beki wa Aldershot Town ya England, Haji Mnoga ambaye kwa sasa amekuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Stars chini ya kocha Adel Amrouche, alisema: “Natamani kuona Tanzania siku moja ikicheza kombe la Dunia, najua kuwa sio jambo jepesi lakini tunatakiwa kuamini na kujaribu kufanya kile ambacho kinawezekana.”

Kwa upande wake, Kwesi Kawawa ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuitwa kwenye kikosi cha Stars akitokea Hammarby IF ya Sweden, alisema: “Ni raha iliyoje kupata nafasi kwenye kikosi cha taifa langu. Nasubiri kwa hamu kuanza kucheza huku nikivaa beji ya Tanzania.”

Msuva na mastaa wengine ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi mara baada ya kuwasili walipewa mapumziko ya siku moja wakati wenzao wakianza maandalizi ya mchezo huo kabla na wao kujumuika nao jana, Jumanne kwa ajili ya kuendelea na maandalizi hayo.

Mara baada ya mchezo dhidi ya Niger, Stars itarejea nyumbani Tanzania kwa kibarua kingine kigumu cha kucheza dhidi ya Morocco, Jumanne ya Novemba 21.

SOMA NA HII  KOSA LA SIMBA KUSHINDWA KUTAMBA KIGALI....... HILI HAPA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here