Home Habari za michezo NAMUNGO WATUMA SALAMU HIZI KWA SIMBA BAADA YA ADHABU YA YANGA

NAMUNGO WATUMA SALAMU HIZI KWA SIMBA BAADA YA ADHABU YA YANGA

Nahodha wa Timu ya Namungo, Jacob Massawe amesema licha ya Simba kuwa bora lakini wasitarajie mchezo mwepesi kutoka kwao kutokana na namna walivyokuwa na kiu ya matokeo mazuri kwa sasa.

Namungo ilizinduka katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC na kufanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Simba baada ya kuchezea kichapo cha mabao 5-1 leo Jumapili na watani zao, Yanga itaikaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Mkapa, mechi itakayochezwa Novemba 9, mwaka huu.

Akizungumza, Massawe alisema wanatambua Simba ni timu kubwa na wanauheshimu ukubwa wao lakini soka lina matokeo ya aina tatu, hivyo wako tayari kuhakikisha wanapambana mbele ili kuondoka na pointi tatu.

“Kila mchezaji anafahamu kucheza na Simba au Yanga ni timu za namna gani lakini ni lazima tucheze maana wote tunahitaji matokeo mazuri, na dakika 90 zitaamua,” alisema.

Kuhusu timu yao kutofanya vizuri mechi zilizopita alisema, ni upepo mbaya uliwakumba na wamebaini makosa yao ambayo wanaendelea kuyarekebisha.

“Ligi ni ngumu sana na ina ushindani ni mkali kila timu inapambana kupata matokeo mazuri sehemu yoyote ile, unaweza kufungwa nyumbani ukashinda ugenini ndio soka,” alisema.

Katika michezo minane ambayo Namungo imecheza imeshinda mmoja tu, ikipata sare nne na kupoteza mitatu ikiwa na pointi saba kibindoni ikishika nafasi ya 12 huku Simba ikiwa na pointi 18 ikiwa nafasi ya pili baada michezo sita iliyocheza ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

SOMA NA HII  MWAMBA KAGOMA KUSEPA NANI ATOKE SIMBA !?