Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Shaffih Dauda amesema kuwa mabeki wa Simba wana madhaifu mengi jambo linalowafanya kufanya makosa mengi yanayoigharimu timu yao na kufungwa karibu kila mechi.
Dauda amesema hayo kuelekea mechi ya Dabi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga utakaopigwa Jumapili ijayo, Novemba 5, 2023 katika Dimba la Mkapa.
“Madhaifu makubwa ya Simba yapo kwa Henock Inonga, ni mchezaji anayependa kukokota mpira na kujaribu kupiga chenga ambazo mara nyingi huwa hazina faida kwa klabu kwa maana ya kimbinu.
“Huwa anafanya vitu vingi ambavyo binafsi sioni kama vina faida badala yake vinaiweka klabu kwenye nafasi ngumu endapo ikitokea wamepoteza mpira.
“Ukiangalia Che Malone anajaribu kuziba makosa yanayofanywa na Inonga lakini kwa kuwa Inonga anafanya vitu vinavyopendwa na watu wengi basi huwa inamfanya asiangaliwe sawa lakini ni makosa ambayo hayatakiwi kwa nafasi yake,” amesema Shaffih Dauda.