Home Habari za michezo UNAJUA SIMBA WALIMNASA VIPI BENCHIKHA….. MBINU ILITUMIKA HIVI

UNAJUA SIMBA WALIMNASA VIPI BENCHIKHA….. MBINU ILITUMIKA HIVI

Kocha Mpya wa Simba

Sahau matokeo ya Simba iliyopata mbele ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwenye pambano la Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imewasapraizi mashabiki wa klabu hiyo kwa kuamua kumleta kocha Abdelhak Benchikha baada ya bilionea Mohamed ‘Mo’ Dewji kuingilia kati dili hilo.

Simba ilikuwa inajiandaa kumpokea kocha huyo Mualgeria aliyeizuia Yanga kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, ikiwa ni siku chache tangu mabosi wa klabu hiyo kumkaushia mara baada ya kutaka dau kubwa ili aje nchini, na kufanya vigogo wa Msimbazi kumgeukia Mtunisia Radhi Jaidi.

Hata hivyo, wakati akiendelea kuzungumza na Jaidi bilionea wa klabu hiyo, Mo Dewji aliamua kuingilia kati na kurudi kwa Benchikha na kuwashirikisha baadhi ya mabosi wa Simba kwa kuwaambia; “Huyu ndiye anayetufaa, tusimwache…”

Ipo hivi. Baada ya Simba kumfuta kazi Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, siku chache baada ya kufungwa 5-1 na watani zao wa jadi Yanga, iliingia sokoni kutafuta kocha mpya atakayeziba pengo hilo haraka.

Simba iliingia sokoni ikitaka kocha mwenye uzoefu wa kutosha na soka la Afrika ili akitua Msimbazi aendane na kasi ya michuano inayoshiriki hasa Ligi ya Mabingwa, pia awe tayari kutimiza malengo ambayo Wekundu wa Msimbazi hao wamejiwekea kwa msimu huu.

Makocha wengi kutoka ndani na nje ya Afrika walituma maombi wakitaka kazi Simba, lakini mabosi hao wakayakacha na kupendekeza majina matatu ya kwanza akiwamo Benchikha, kocha wa zamani wa Yanga, Nassredine Nabi na Sven Vandenbroeck aliyewahi kukinoa kikosi hicho.

Hata hivyo, ishu ya Nabi na Sven zilionekana kuwa ngumu tangu mwanzo na Simba ikaachana nao na kuwekeza nguvu zote kwa Benchikha ambaye pia alikuwa na ofa kutoka Zamalek ya Misri.

Wakati vigogo wa Simba wakienda vyema na Benchikha, ghafla shida ikaja pale tu alipowatajia mkwanja ambapo alihitaji zaidi ya Sh49 milioni kwa mwezi jambo ambalo liliwaduwaza wengi wao kwani kabla ya hapo Simba haijawahi kulipa kocha kiasi hicho.

Hali hiyo iliwafanya kupozi kidogo kwenye dili hilo na kugeukia kwa Mtunisia Radhi Jaidi waliyejadiliana naye kila kitu na kwenye hatua za mwisho lakini ghafla Mo alipiga simu Msimbazi na kuulizia ishu ya kocha wakamwambia kwa Benchikha imegoma kutokana na dau alililotaja na sasa wako kwa Jaidi.

Taarifa za ndani zinasema Mo Dewji aliwaambia; “Niachieni mimi”.

Katika hali ambayo viongozi wengi wa Simba wamekataa tamaa na Benchikha kutokana na dau lake, inaelezwa Mo Dewji aliwaomba mahitaji ya kocha huyo, wakamtumia na hapo hapo bila kupiga bei, akawaambia wamalizane naye na mkwanja wote atalipa yeye.

Kwa kuwa alikuwa huru anasikilizia dili hilo kukakamilika, Benchika alivyovutiwa waya na kiongozi wa Simba akimueleza wamekubaliana kumlipa kama anavyotaka, fasta alisaini mkataba ‘online’, na rasmi kutambulishwa juzi Msimbazi akiwa bado nchini kwao Algeria.

Mwanaspoti kama kawaida yetu tukazama chimbo na kugundua kocha huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu wenye kipengele cha kuongeza na sasa atakuwa kocha anayelipwa pesa nyingi zaidi Tanzania akivuta zaidi ya Sh 49 Milioni kwa mwezi.

Kocha huyo aliyewanyima Yanga ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu ulipita akiwa na USM Alger anatarajiwa kuanza kazi rasmi Jumatatu, ambapo amepewa malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Benchika katika karia yake ya ukocha ametwaa makombe nane tofauti, ikiwemo lile la Kombe la Shirikisho Afrika alilolichukua msimu uliopita akiwa na USM Alger CAF Super Cup alilobeba mara mbili.

WASIFU WA BENCHIKHA

1999-2001 kocha msaidizi CR Blouizdad

2001-2003 Kocha mkuu Arderia U23

2002-2005 kocha mkuu CABB Arreridj(Morroco)

2005-2006 Kocha mkuu Umma Salal (Qatar)

2006-2007 Kocha mkuu Es Zarzis (Tunisia)

2007-2008 Club Africain (Tunisia)

2009-2010 Kocha mkuu timu ya taifa Algeira

2011 Kocha mkuu MC Algier (Algeria)

2011-2012 Kocha mkuu Club Africain (Tunisia)

2013-2014 Kocha mkuu Difaa El Jadida (Morocco)

2014 Kocha Mkuu Raja Casablanca (Morocco)

2014 – 2015 Kocha Mkuu Ittihad Kalba (Morocco)

2015 – 2017 Kocha Mkuu Ittihad Tanger (Morocco)

2017 Kocha Mkuu Raja Casablanca (Morocco)

2017 Kocha mkuu Moghreb Tétouan (Morocco)

2018 Kocha Mkuu ES Setif (Algeria)

2018-2019 Kocha mkuu Al Ittihad (Libya)

2019-2020 Kocha Mkuu Mouloudia (Morocco)

2020-2022 kocha mkuuu Difaa El Jadida (Morocco)

2022 Kocha Mkuu RS Berkane (Morocco)

2022-2023 Kocha Mkuu US Alger (Morocco)

SOMA NA HII  WAKILI WA YANGA, AWAPIGA DONGO HILI SIMBA SC, MANGUNGU AHUSISHWA