Home Habari za michezo YANGA SIMBA HAKUNA KUZUBAA KIMATAIFA

YANGA SIMBA HAKUNA KUZUBAA KIMATAIFA

Mashabiki wa Simba na Yanga

Simba na Yanga zinapaswa kupambana hadi tone la mwisho la damu leo katika mechi zao za raundi ya pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika viwanja na miji tofauti Afrika ili kila moja ivune ushindi mabao utaweka hai matumaini ya kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu huu.

Kitendo cha kila moja kutopata ushindi katika mechi ya mwanzo kinalazimisha matokeo ya ushindi katika mechi za leo ili timu hizo mbili zinazowakilisha Tanzania katika mashindano hayo zijiweke katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali.

Simba iliyoanza kwa kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani na Asec Mimosas ya Ivory Coast, leo itakuwa ugenini huko Botswana katika Uwanja wa Obed Itani Chilume kukabiliana na kinara wa kundi lake B, Jwaneng Galax katika mchezo utakaoanza saa 10:00 kwa muda wa Tanzania.

Baada ya hapo, saa 1:00 usiku, Yanga ambayo ilianza hatua hiyo kwa kupoteza kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya CR Belouizdad, itaikaribisha Al Ahly inayoongoza kundi lao D katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ujio wa kocha mpya, Abdelhak Benchikha unaonekana utaipa nguvu kubvwa Simba leo hasa katika kuongeza ari ya kupambana kwa wachezaji ili watengeneze mazingira ya kujihakikishia nafasi kikosini.

Ni mchezo ambao unaonekana utakuwa mgumu kwa Simba kwani Jwaneng Galaxy ndio vinara wa kundi B baada ya kupata ushindi katika mechi ya kwanza ugenini huko Morocco dhidi ya Wydad Casablanca.

Kupoteza mechi ya leo kutaiweka Simba katika uwezekano finyu wa kuingia robo fainali hasa ikizingatiwa mechi mbili zinazofuata ni ngumu dhidi ya Wydad ambayo msimu uliopita iliwatoa katika robo fainali ya Ligi ya Mbaingwa Afrika.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limempanga refa Mohamed Adel kutoka Misri kuchezesha mechi hiyo.

Mbali na kuweka hai matumaini ya kuingia robo fainali, Simba inahitaji ushindi katika mechi ya leo ili kurudisha morali na hamasa ya timu ambayo imeonekana kupotea katika siku za hivi karibuni kutokana na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha.

Kwa Simba hiyo ni fursa nzuri ya kulipa kisasi kwa Jwaneng Gaaxy ambayo msimu wa 2021/2022 iliwatupa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kanuni ya faida ya mabao ya ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Kumbukumbu ya mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika inaonyesha Simba haina ubabe unini ambapo imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare mbili na kupoteza tano.

Lakini hilo halipaswi kuipa hofu Simba kwani Jwaneng Galaxy nao wamekuwa hawana historia ya utemi nyumbani ambapo katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika, wameshinda nne tu, sare moja na wamepoteza mechi tano.

Kocha wa makipa wa Simba, Daniel Cadena alisema wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo ambayo anaamini wachezaji wake watarudisha heshima.

“Morali ya timu iko juu sana na wachezaji wanatamani kupata ushindi katika huu mchezo ili tuweze kupata pointi tatu ambazo zitatuweka katika nafasi nzuri kwenye kundi,” alisea Cadena.

Kikosi cha Simba leo kinaweza kuundwa na Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Enock Inonga, Fondoh Malone, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Fabrice Ngoma, Jean Baleke, Clatous Chama na Kibu Denis.

Kwa Yanga, nidhamu kubwa hasa dhidi ya mashambulizi ya kushtukiza inahitajika kuwepo kwa safu ya ulinzi ya Yanga leo dhidi ya Al Ahly ili kutoruhusu kujirudia kwa makosa kama yale ambayo yaliwaponza katika mechi ya kwanza dhidi ya CR Belouizdad.

Urejeo wa kipa Djigui Diarra unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa Yanga kutokana na uwezo wa kipa huyo raia wa Mali kuwa na uwezo mkubwa wa ujenzi wa mashambulizi kuanzia nyuma, kuipanga na kuituliza safu ya ulinzi lakini pia kuokoa hatari zinazoelekezwa langoni mwake.

Mchezo huo wa leo utachezeshwa na refa : Abdel Aziz Mohamed Bouh kutoka Mauritania.

Kupoteza au kutoka sare dhidi ya Al Ahly nyumbani leo maana yake kutaweka rehani uwezekano wa Yanga kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kundi lake hivyo kwa namna yoyote ile inatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inapata ushindi katika mechi ya leo dhidi ya timu hiyo ya Misri ambayo ni bingwa mtetezi wa mashindano hayo.

Hapana shaka kocha Miguel Gamondi ataendelea na soka lake la kushambulia kama ambavyo amekuwa akifanya dhidi ya timu nyingine lakini akichukua tahadhari ya kujilinda kwa haraka pindi timu inapopoteza mpira.

Yanga haina historia nzuri mbele ya Al Ahlyt iwe katika mechi za nyumbani au ugenini na pengine leo ni muda sahihi wa kuthibitisha kuwa nyakati za unyonge dhidi yao zimeshaisha kwa kupata ushindi nyumbani.

Historia inaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 10 katika mashindano tofauti ya klabu Afrika ambapo katika idadi hiyo ya michezo, Al Ahly imeibuka na ushindi mara sita, sare tatu na Yanga imepata ushindi mara moja tu.

Katika mechi hizo 10, tano, Yanga ilikuwa mwenyeji ambapo iliibuka na ushindi mara moja, sare tatu na ikapoteza mechi moja.

Lakini kwa sasa mambo yanaonekana kubadilika sana na hapana shaka Al Ahly itakutana na mechi ngumu zaidi pengine kuliko zote walizowahi kucheza na Yanga kutokana kuimarika vilivyo kwa wawakilishi hao wa Tanzania kunakobebwa na hali ya kujiamini hasa inapokuwa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kuthibitisha hilo, katika mechi tano zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo ilicheza nyumbani,Yanga imeibuka na ushindi mara nne na kupoteza mechi moja tu.

Kikosi cha Yanga leo kinaweza kuundwa na Djigui Diarra, Yao Attohoula, Joyce Lomalisa, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahaya, Clement Mzize, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.

Kocha Gamondi alisema kuwa ana matumaini timu yake itaibuka na ushindi katika mchezo wa leo.

“Ni mchezo muhimu kwetu kupata ushindi. Hatukufanya vizuri katika mechi ya kwanza hivyo kesho (leo) ni lazima kupata ushindi ili tuweke sawa hesabu zetu kwenye kundi,” alisema Gamondi.

SOMA NA HII  BAADA YA KURUDI RASMI NA KUKIWASHA JANA...MIQUISSONE APEWA ZA USO KWA UNENE WAKE...