Home Habari za michezo KWA HILI SASA KAZI NI KWA YANGA TU

KWA HILI SASA KAZI NI KWA YANGA TU

Tetesi za usajili Yanga

Straika wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro amevunja ukimya kwa mara ya kwanza kwa kuzungumza na Mwanaspoti juu ya tetesi za kusajiliwa na Yanga akisema hatma yake ipo mikononi mwa mabosi wa timu hizo mbili iwapo watamalizana mapema.

Yanga imekuwa ikihusishwa na nyota huyo wa zamani wa Marumo Gallants tangu mwishoni mwa msimu uliopita kabla ya kuibukia Kaizer Chiefs ikielezwa alitangulizwa na Kocha Nasreddine Nabi aliyekuwa mbioni kujiunga na timu hiyo baada ya kutimka Jangwani.

Hata hivyo, baadaye Nabi aliibukia FAR Rabat ya Morocco, lakini hivi karibuni ilidaiwa viongozi wa Yanga walirudi tena kwa mchezaji huyo ili kumsajili dirisha dogo hasa wakizingatiwa hajacheza michuano ya CAF, hivyo ni rahisi kumtumia kwenye mechi za makundi na za mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwanaspoti lilimsaka Chivaviro na kuzungumza naye juu ya tetesi za kutakiwa Jangwani na bila hiyana alifunguka huku akimtaja Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ na mabeki wa kati wa Jangwani ni watu wanamvutia na kutamani kuja Tanzania. Skudu aliwahi kucheza naye Marumo.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwanaspoti, Chivaviro alisema bado ana mkataba na Kaizer Chiefs ingawa anafahamu kwamba Yanga wanamtaka.

Chivaviro alisema kama Yanga itamalizana na Kaizer maarufu kama Amakhosi hatasita kujiunga nayo ikiwa ni moja ya klabu kubwa barani Afrika na hususan ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mimi nina mkataba hapa (Kaizer Chiefs), lakini hizo taarifa nazisikia na niliwahi kuzunguza na kiongozi mmoja wa klabu hiyo, ila ni muda kidogo,” alisema Chivaviro mwenye asili ya Zimbabwe.

“Nachoweza kusema Yanga ni klabu kubwa sio rahisi kwa mchezaji kuikataa, lakini nadhani ni suala klabu mbili kumalizana. Endapo watazungumza mimi kazi yangu ni kucheza tu.”

Chivaviro aliyemaliza nafasi ya pili ya ufungaji mabao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiifungia Marumo mabao sita nyuma ya Fiston Mayele aliyekuwa Yanga aliyemaliza kinara na mabao saba, aliongeza kuwa ndani ya Yanga kwa sasa ana marafiki wawili akiwemo winga, Skudu na mabeki wa timu hiyo ambao huwa wanawasiliana hadi sasa tangu walipokutana kwenye mechi za nusu fainali za Shirikisho na Marumo kung’olewa na Yanga.

“Yanga ina wachezaji wazuri kwa sasa yuko pale kaka yangu Skudu. nNilikuwa naye Marumo Gallants, lakini tangu tulipokutana na timu hiyo msimu uliopita kuna marafiki zangu mabeki wale wa kati, jambo ambalo limenifanya kuijua vyema klabu hii.”

Yanga inahaha kusaka mshambuliaji wa kati wa kuongeza nguvu kufunga mabao ambapo tangu ameondoka Mayele hakuna aliyeonyesha kuvaa viatu hivyo, licha ya kusajiliwa Hafiz Konkoni kutoka Ghana na kikosini kuwepo kwa Clement Mzize na Kennedy Musonda.

Hata hivyo rekodi za msimu huu zinaonyesha Chivaviro ameichezea Kaizer kwenye mechi 10 za Ligi Kuu (PSL ) akifunga bao moja na kuasisti moja, tofauti na msimu uliopita katika michezo 19 akiwa na Marumo alifunga mabao 10, mbali na mechi 10 za kimataifa alipofunga jumla ya mabao sita.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMANNE, LIPO MTAANI NA ZAWADI