Home Habari za michezo MASTAA HAWA SIMBA WANAKUSANYA MAOKOTO KIMYA KIMYA

MASTAA HAWA SIMBA WANAKUSANYA MAOKOTO KIMYA KIMYA

Habari za Simba leo

Simba kimya kimya ipo kwenye hatua za mwisho kusaini mastaa wapya kikosini hapo watakaoingia kwenye dirisha dogo la usajili lililowazi hadi Januari 15, mwakani.

Wakali hao wa Msimbazi chini ya kocha mkuu Abdelhak Benchikha wamepanga kusajili wachezaji wapya wasiopungua watatu kwenye dirisha hili na tayari mchakato wa kuwashusha Msimbazi unaendelea.

Hata hivyo, pamoja na kuwa mbioni kusajili wachezaji wapya lakini kuna mastaa wapo pale Msimbazi ila hawajacheza hata dakika moja kwenye mechi yoyote ya mashindano huku wengine wakicheza dakika chache sana.

Kwa maana hiyo wanakula pesa za Simba bila kuzitumikia kutokana na sababu mbalimbali ambapo kima cha chini cha mshahara kwa mchezaji wa Simba ni Sh1 milioni.

Mwanaspoti kupitia makala haya, linakuletea wachezaji watano wa Simba ambao tangu msimu huu umeanza Agosti 15 mwaka huu ikiwa ni sawa na miezi mitano hawajacheza.

HUSSEIN ABEL

Huyu ni kipa wa Simba aliyesajiliwa katika dakika za mwisho za dirisha kubwa la usajili la msimu huu akitokea KMC ya Dar es Salaam.

Abel aliyewahi kuichezea Tanzania Prisons kwa mafanikio tangu ametua Simba hajapata nafasi ya kucheza walau hata dakika moja kwenye mechi ya mashindano hadi sasa dirisha dogo la usajili limefunguliwa.

Kwa hesabu za kawaida, Abel amekunja mshahara wa miezi mitano Simba bila kuvuja jasho lolote kwenye mechi huku Ayoub Lakred, Ally Salim na Aishi Manula wakicheza eneo lake.

JIMMYSON MWANUKE

Winga huyu wa kulia alisajiliwa na Simba misimu miwili iliyopita akitokea Gwambina lakini ameshindwa kuonyesha ushindani kikosini tangu aliposajiliwa.

Msimu uliopita alionekana kwenye mechi chache lakini msimu huu hadi sasa hajawa na nafasi.

Wachezaji wa pembeni kama Augustine Okrah na Nelson Okwa walikuja wakapata nafasi kidogo pembeni kabla ya kutimka wakimzidi Jimmyson kama alivyozidiwa nafasi ya kucheza pia na kina Pape Ousmane Sakho na Peter Banda, au Kibu Denis na Said Ntibazonkiza. Msimu huu pia Simba ikamleta Willy Onana, ambaye naye ameanza kupata nafasi akimzidi Mwanuke katika nafasi za pembeni.

NASSORO KAPAMA

Staa huyu wa zamani wa Kagera Sugar alitua Msimbazi msimu uliopita lakini hadi leo ameshindwa kupambania namba kwenye kikosi cha timu hiyo.

Msimu uliopita alipata dakika kadhaa za kuichezea timu hiyo lakini tangu msimu huu umeanza hajacheza hata dakika moja kwenye mechi za mashindano hadi kufika Desemba 15, mwaka huu.

Kapama amevuta mshahara wa miezi mitano bila kucheza huku eneo lake wakicheza Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassini na Sadio Kanoute.

ABDALLAH HAMIS

Huyu ni kiungo mwingine anayepatikana kwenye viunga vya Simba lakini tangu msimu huu umeanza amecheza dakika chache tu za mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wydad.

Abdallah ni kiungo wa Kitanzania aliyesajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Orapa United FC ya Botswana na kabla ya hapo aliwahi kuichezea Bandari ya Kenya.

Katika eneo analocheza Abdallah, Kanoute, Ngoma na Mzamiru ndio wanapata nafasi ya kucheza pale Simba.

MOHAMED MUSSA

Huyu ni mshambuliaji wa kati aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Malindi ya Zanzibar alikokuwa straika tegemeo.

Tangu alipotua Simba mambo hayakumuendea vizuri kwani hadi sasa ameifungia bao moja pekee kwenye mashindano yote lakini msimu huu hajapata hata dakika moja ya kucheza kwenye mechi za mashindano.

Mussa pale Simba kwenye eneo lake wanacheza Jean Baleke, John Bocco, Moses Phiri, na Shaban Chilunda.

Tangu msimu huu kuanza, Simba imecheza jumla ya mechi 19 ikiiwemo ile ya juzi ya dhidi ya Wydad Casabalanca iliyochezwa kwa Mkapa lakini mastaa hao watano hakuna hata mmoja aliyeonja dakika kwenye mechi hizo.

Wachezaji wengine waliopo Simba lakini hawajacheza walau dakika 90 kwenye mechi za mashindano ni Hussein Bakari, Ahmed Feruz na Kramo Aubin aliye majeruhi.

SHAABAN CHILUNDA

Alitabiriwa kuja kuwa mmoja wa mastaa wakubwa zaidi ambao Tanzania imewahi kuwa nao alipoonekana kupitia njia sahihi za kukuza kipaji chake alipolelewa na timu za vijana za Azam kisha akaenda kujiunga na Tenerife ya Hispania kwa mkopo.

Hata hivyo, klabu hiyo ya Hispania iliachana naye baada ya kutoridhishwa naye. Hata aliporudi Tanzania, Azam pia ilimruhusu aondoke na kutua Simba ambako hapati dakika nyingi.

SOMA NA HII  MWADUI FC YAZITAKA POINTI TATU ZA YANGA