Home Habari za michezo KISA LUSAJO VIONGOZI WAHAHA NAMUNGO

KISA LUSAJO VIONGOZI WAHAHA NAMUNGO

Habari za Michezo, habari za Simba

Wakati dirisha dogo la usajili nchini likiendelea kwa timu kuboresha vikosi vyao, Namungo imesema inahitaji straika mmoja tu atakayekuwa mwarobaini wa mabao kikosini.

Namungo iliyopo nafasi ya nane kwa pointi 17 kwa sasa haina kocha mkuu baada ya aliyekuwapo, Denis Kitambi kutimkia Geita Gold na kuwafanya mabosi wa timu hiyo kusaka mbadala wake.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa amesema katika kipindi hiki cha dirisha dogo hawahitaji mabadiliko makubwa kutokana na uwezo walionao wachezaji isipokuwa wanaangalia upatikanaji wa mshambuliaji mmoja tu.

Amesema kuanzia sehemu ya kipa hadi winga wachezaji wanafanya vizuri isipokuwa ni eneo moja tu la straika linahitaji nguvu kidogo, hivyo wapo kwenye harakati za kuangalia nani atawafaa.

“Timu iko vizuri sana licha ya kupoteza mechi dhidi ya Prisons, lakini tunahitaji straika mmoja ambaye atakuwa mwarobaini wa mabao, maeneo mengine kikosi kimekamilika.

“Ligi inasimama, tunaenda kujipanga zaidi kuhakikisha tunaendelea kufanya vizuri, tunayo mashindano mawili, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ligi Kuu, yote hayo ni muhimu sana kwetu kufanya vizuri,” alisema Nsajigwa.

Beki wa timu hiyo, Frank Magingi amesema bado wanao uwezo wa kufanya vizuri na kumaliza ndani ya nafasi nne za juu akiwaomba wenzake kikosini kuendelea kupambana kwa kila mechi.

Wakati timu hiyo ikitafuta mshambuliaji, aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Reliants Lusajo ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram wa kuiaga klabu yake.

Katika ujumbe wake huo, Lusajo ameandika; “Napenda Kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Namungo na benchi la ufundi bila kusahau mashabiki wote wa timu ya Namungo kwa kipindi chote tulichokuwa pamoja. Ni muda wangu sasa wa kuangalia changamoto sehemu nyingine. Nipende kuwatakia kila la kheri katika msimu huu wa ligi.”

Reliants ameitumikia Namungo tangu mwaka 2021akitokea KMC na katika msimu huu wa ligi 2023/2024 ameifungia mabao mawili na asisti moja.

SOMA NA HII  MOURINHO ABEBA MATUMAINI KIBAO KWA NYOTA WAKE MPYA NDANI YA SPURS