Home Habari za michezo UMAKINI ANAO UTAKA BENCHIKHA UNAAMBIWA KAMA JESHINI

UMAKINI ANAO UTAKA BENCHIKHA UNAAMBIWA KAMA JESHINI

Habari za Simba

Baada ya kukiangalia kikosi cha timu yake, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, ni kama ametoa angalizo kwa viongozi wa klabu hiyo kuwa makini wanapoenda sokoni kipindi cha dirisha dogo la usajili kulingana na aina ya wachezaji aliokuwa nao kwa sasa.

Kauli hiyo imekuja baada ya mchezo wa juzi uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC FC.

Benchikha alisema ana kazi kubwa ya kufanya ndani ya kikosi chake ili kurudi katika ubora na kuendelea kupata ushindi katika michezo iliyopo mbele yao na kufikia malengo yao.

Alisema walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi wakashindwa kuzitumia, lakini pia kulikosekana umakini katika safu yake ya ulinzi.

“Kwa sasa tutaendelea kukisuka kikosi katika michuano ya Mapinduzi pamoja na kufanyia kazi maboresho ya kikosi katika maingizo mapya, naamini tutarejesha makali yetu.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya, tunahitaji kurudi katika hali ya kawaida na kupigamia mataji, timu inacheza vizuri, lakini kuna vitu vinakosekana ikiwamo kutumia nafasi tunazotengeneza, hilo ndilo jambo tunapaswa kulimaliza,” alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa wanaelekea kipindi cha mapumziko ambacho watakuwa makini katika maboresho ya kikosi kulingana na mahitaji ya timu lakini pia kutumia Kombe la Mapinduzi kuandaa kikosi imara.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, pia alikiri timu yao inahitaji mabadiliko makubwa kwa kusajili wachezaji wazuri wenye uchu wa mafanikio.

“Lazima tukiri kuwa kikosi chetu kinahitaji mabadiliko makubwa mawili, kwanza ni kuongeza wachezaji wenye ubora, uchu na kiu ya mafanikio.

“Pili ni wachezaji waliopo kuongeze ubora wao wa upambanaji. Huwezi kufanikiwa kwa kuwa na matokeo ya panda shuka, timu kubwa yenye malengo ya ubingwa lazima iwe na mwendelezo wa kupata matokeo mazuri,” alisema Ahmed.

Aliongeza kuwa wana miezi miwili ya kufanya mabadiliko hayo mawili makuu ambayo ameona ni tatizo ambalo linawakwamisha mpaka sasa.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili ni kwamba, majina yanayotajwa kuwamo mezani mwa uongozi wa klabu hiyo ni Alves Ngakosso Oko, Hardest Malonga, Moise Gbai, Mohammad Alzabbad, Abdoulaye Djire, Abdul Aziz Issah, Derrick Fordjour, Ibrahim Seck na Jonathan Alukwu.

SOMA NA HII  WAKALI WA KUSEPA NA CLEAN SHEET BONGO HAWA HAPA