Home Habari za michezo SOKA ‘KHARAM’ LA BENCHIKHA LAKOMBA MASTAA WOTE WA SIMBA KWENDA ZNZ….

SOKA ‘KHARAM’ LA BENCHIKHA LAKOMBA MASTAA WOTE WA SIMBA KWENDA ZNZ….

Habari za Simba

KIKOSI cha Simba leo kinatarajiwa kuvuka Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar tayari kusaka ubingwa wa tano wa Kombe la Mapinduzi 2024, huku benchi la ufundi likidaiwa kufanya kikao na wachezaji na kuwataka kukomaa ili warejee na taji hilo.

Simba ipo Kundi B ikitarajiwa kushuka uwanjani kesho dhidi ya JKU ya Zanzibar iliyoanza vibaya kwa kufumuliwa mabao 4-1 na Singida Fountain Gate, mechi itakayopigwa kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja. Timu nyingine ya kundi hilo ambayo kesho pia itashuka uwanjani ni APR ya Rwanda itakayoikabili vinara wa kundi hilo Singida.

Wekundu wa Msimbazi ndio klabu iliyocheza fainali nyingi zaidi kwenye michuano hiyo, (nane) huku ikitwaa taji mara nne ikishika nafasi ya pili nyuma ya Azam iliyobeba ubingwa huo mara tano tangu michuano iliyoasisiwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2007.

Mara ya mwisho kwa Simba kubeba taji ilikuwa mwaka 2022 ilipoitungua Azam FC bao 1-0 lililowekwa kimiani na Meddie Kagere ambaye kwa sasa yupo Singida, kwani msimu uliopita timu hiyo ilitolewa hatua ya makundi na kushuhudiwa Singida ikienda kucheza fainali na Mlandege iliyobeba taji.

Licha ya kuwakosa wachezaji kadhaa walioitwa kwenye timu za taifa, lakini Simba itakayoingia Zanzibar mchana wa leo ina majembe ya maana ambao wamepewa nafasi kubwa ya kufanya maajabu msimu huu.

Ikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha, Simba imeenda na nyota wake wote ambao hawapo kwenye timu za taifa zinazojiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 itakayofanyika Ivory Coast kati ya Januari 13 hadi Februari 11 mwakani.

“Timu itaondoka na kufika Zanzibar majira ya mchana, ikiwa na wachezaji wote wakiwamo Moses Phiri ambaye amekuwa akihusishwa kutaka kuondoka kikosini, pia kuna majembe mapya mawili,” kilisema chanzo kutoka Simba na kuongeza;

“Hakuna mchezaji atakayeachwa Dar es Salaam, kwani kocha anataka kuwasoma wote na kufanya uamuzi kwenye dirisha hili la usajili, kabla ya safari kocha amefanya kikao na wachezaji na kuwaeleza ni lazima warudi Dar na ubingwa, anaamini michuano hiyo ni sehemu ya kujiweka fiti kabla ya kurejea katika Ligi na michuano ya CAF.

Simba inashika nafasi ya pili katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikisaliwa na mechi mbili za kufungia Kundi B, ikianzia ugenini Februari 23 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kisha kuikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana Machi Mosi na kuamua hatma ya kwenda robo fainali au la.

Baadhi ya nyota waliokuwa katika msafara huo wa Simba ni pamoja na ; Jimmyson Mwanuke, Abdallah Khamis, Hussein Kazi, Hussein Abel, Ally Salim, Fondoh Che Malone, John Bocco na David Kameta ‘Duchu’,

Wengine ni Willy Onana, Luis Miquissone, Shaaban Idd Chilunda, Fabrice Ngoma, Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute, Henock Inonga, Ayoub Lakred, Shomary Kapombe na Moses Phiri.

Wachezaji wengine Mohammed Hussein, Kibu Denis, Mzamiru Yasin, Aishi Manula na Kennedy Juma wapo timu ya taifa, Taifa Stars inayojiandaa na fainali za Afcon, Tanzania ikipangwa kundi moja na Zambia, Morocco na DR Congo.

Miongoni mwa nyota wapya wanaotajwa watakuwa sehemu ya kikosi hicho ni winga kutoka Mtibwa Sugar, Ladack Chasambi anayedaiwa ameshamalizana na mabosi wa Wekundu wa Msimbazi hao wanaoshika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara inayoongozwa na Azam kisha kufuatiwa na Yanga.

Mara baada ya kumalizana na JKU kesho, Simba itarudi tena uwanjani Januari 3 kuikabili Singida kabla ya kumalizana na APR Ijumaa ijayo ikiwa ni mechi za kusaka tiketi ya robo fainali itakayochezwa kuanzia Januari 7 na fainali ya michuano hiyo ya msimu wa 18 itapigwa Januari 13.

Mechi zijazo za Simba SC

Kesho Jumatatu

vs JKU (Saa 2:15 usiku)

Januari 03, 2024

vs Singida FG (Saa 2:15 usiku)

Januari 05, 2024

vs APR(Saa 2:15 usiku)

SOMA NA HII  5G YA YANGA YAMPONZA ROBERTINHO