Home Habari za michezo BAADA YA UKIMYA MWINGI ONYANGO AFUNGUKA HAYA

BAADA YA UKIMYA MWINGI ONYANGO AFUNGUKA HAYA

Habari za Michezo leo

Baada ya kimya cha muda mrefu bila kuonekana uwanjani akiwa na kikosi cha Singida Fountain Gate, beki Joash Onyango ameweka wazi kilichofanya asionekane ni majeraha na yeye bado ni mali ya timu hiyo na sasa anapambana kuirejesha namba yake kikosini.

Mara ya mwisho kwa beki huyo kuonekana uwanjani ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida na kuisha kwa suluhu na kuibuka kwa tetesi nyingi ikiwemo huenda ametimka ndani ya kikosi hicho, kwani hakukuwa na taarifa zilizowahi kutolewa na uongozi juu ya kutoonekana uwanjani.

Hata hivyo, juzi akizungumza na Mwanaspoti, Onyango alisema alikuwa nje ya uwanja kutokana na jeraha la goti, ila kwa sasa yupo fiti na tayari ameanza mazoezi pamoja na wenzake, huku akikiri ana kibarua kigumu cha kurudi kwenye nafasi yake.

“Bado nipo Singida, mie ni mchezaji halali wa timu hiyo, kutoonekana uwanjani ni kwa sababu nilikuwa nauguza jeraha la goti na kwa sasa nipo fiti na muda wowote naweza kuonekana nikiipigania timu kwenye michuano tuliyopo,” alisema beki huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya na Simba.

“Licha ya kurudi nikiwa fiti, bado nina kibarua cha kuhakikisha narudi kikosi cha kwanza, kwani tayari kuna ukuta ulioanza kuaminiwa na umefanya mambo makubwa kwenye mechi ambazo sijapata nafasi ya kucheza hivi karibuni,” aliongeza beki huyo wa kati aliyewahi kukipiga timu ya taifa ya Kenya.

Alisema ukuta unaojengwa na Abdulmajid Mangalo, Biemes Carno, Laurian Makame na Hamad Wazir ‘Kuku’ wote wakipata nafasi ya kucheza unampa mtihani wa kupambana ili kurejesha namba kama ilivyokuwa kabla ya kuumia japo anaamini maamuzi ya mwisho yapo kwa benchi la ufundi kuwapanga.

SOMA NA HII  KUHUSU ISHU YA MASHABIKI KUSHINDWA KUANGALIA MECHI RWANDA, UONGOZI WA YANGA WASEMA HAYA