Home Habari za michezo BANDA SASA ANATAKIWA KUONGEA LUGHA MOJA NA MBRAZIL

BANDA SASA ANATAKIWA KUONGEA LUGHA MOJA NA MBRAZIL

Singida Fountain Gate, iko mbioni kukamilisha usajili wa aliyekuwa winga wa Simba, Peter Banda, huku kocha mkuu wa kikosi hicho Mbrazili Ricardo Ferreira akiachiwa maamuzi ya mwisho ya kama atapendezwa na nyota huyo ili asajiliwe.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza Banda tayari ameshafanya mawasiliano ya moja kwa moja na viongozi wa timu hiyo baada ya kuachana na Nyassa Big Bullets ya Malawi kufuatia mkataba wa miezi mitatu aliousaini kumalizika.

“Mazungumzo ya awali yanaendelea vizuri lakini maamuzi ya mwisho yatabaki kwa benchi la ufundi kama litaridhia usajili wake ila kwetu viongozi hatuna wasiwasi na kiwango chake ila tunaheshimu watu kwa taaluma zao,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumzia hilo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Singida, Olebile Sikwane alisema kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia suala la usajili kwa sababu bado hawajakamilisha kwa asilimia zote, hivyo muda utakapofika kila kitu watakiweka wazi.

“Dirisha linapofunguliwa tetesi zinakuwa nyingi kwa sababu kila mtu atazungumza jambo lake, siwezi kuthibitisha kama ni kweli au sio kweli hadi pale tutakapofikia makubaliano na wachezaji tunaowahitaji kupitia ripoti ya benchi la ufundi.”

Raia huyo wa Malawi kwa mara ya kwanza alitua nchini 2021 na kujiunga na Simba akitokea FC Sheriff Tiraspol ya Moldova na kushindwa kufanya makubwa kutokana na kupata majeraha mara kwa mara kabla ya kumtemwa Agosti 28 mwaka huu na kurudi Nyassa Big Bullets iliyompa mkataba mfupi wa miezi mitatu.

SOMA NA HII  UNAAMBIWA AJIB NI ZAIDI YA AZIZ KI