Home Habari za michezo BENCHIKHA SIO POA SASA NI VITA KAMILI

BENCHIKHA SIO POA SASA NI VITA KAMILI

Habari za Simba leo

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha anapeleka kikosi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, inayotarajiwa kuanza kesho 28, huku kichwani akiwa na mambo mawili, ikiwamo kulinoa panga alilonalo mkononi kwa ajili ya kuweka mambo sawa kwenye kikosi hicho.

Benchikha amesema anaenda kwenye michuano hiyo ili kupata muda na kukisoma kikosi hicho na wachezaji wa timu hiyo ili kurekebisha makosa yaliyopo hasa kwenye eneo la ushambuliaji kabla ya kufanya maamuzi kupitia dirisha dogo litakalofungwa siku mbili baada ya kumalizika kwa Kombe la Mapinduzi.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo kutoka Algeria alikiri eneo la ushambuliaji limekuwa likiangusha timu hiyo kwenye mechi tano alizoiongoza timu hiyo tangu apewe mkataba na sasa atatumia michuano hiyo ya Mapinduzi kuweka mambo sawa, sambamba na kufanya maamuzi ya kuimarisha kikosi.

Mechi ambazo amekaa Benchikha benchi ni dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana iliyoisha kwa suluhu, Wydad AC ya Morocco iliyowachapa 1-0 ugenini kabla ya kurudiana nao Dar es Salaam na kulipa kisasi kwa kuifunga mabao 2-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mechi za Ligi ikishinda 3-0 mbele ya Mtibwa Sugar na kulazimishwa sare ya 2-2 na KMC. Katika mechi hizo Simba imefunga mabao saba, huku mabeki wakiruhusu mabao matatu.

“Nimeona changamoto ya kushindwa kumalizia kufunga kwenye nafasi zinazotengenezwa, sasa tunakwenda Mapinduzi ambako nitayafanyia kazi mambo mengi ikiwemo na hilo,” alisema Benchikha na kuongeza;

“Ni nafasi nzuri kushiriki Mapinduzi kwani inashiriki timu nyingi, hivyo itakuwa rahisi kuyafanyia kazi mapungufu, ili tutakaporejea kwenye Ligi Kuu, kutakuwa na mabadiliko mengi.”

Simba inayoshika nafasi ya pili ya kutwaa mataji mengi (manne) ya michuano hiyo ya Mapinduzi imepangwa Kundi B na za JKU, APR ya Rwanda na Singida Fountain Gate na itakata utepe kwa kuvaana na vinara wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU kabla ya kuvaana na Singida Januari 3 na kumalizia dhidi ya APR Januari 5.

Katika hatua nyingine, kocha huyo inadaiwa amependekeza kuongezwa washambuliaji wawili wa kati wa kigeni ili kuimarisha eneo hilo ambalo kwa sasa linawategemea, Jean Baleke, Moses Phiri na John Bocco wanaosaidiwa na mawinga Willy Onana, Kidbu Denis na Saido Ntibazonkiza.

Hata hivyo, hadi sasa mabosi wa timu hiyo wanakuna kichwa kutokana na gharama za kuwasajili wachezaji hao aliopendekeza Benchikha, japo kwa sasa wanapambana kuzungumza nao ili kuona kama watapunguziwa na kukidhi matakwa ya kocha huyo mwenye misimamo mikali hasa upande wa nidhamu na kupiga kazi.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA TIMU YA TAIFA KITAKACHOANZA LEO DHIDI YA BOTSWANA