Home Habari za michezo KATWILA AFUNGUKA KUHUSU MCHEZO WA YANGA

KATWILA AFUNGUKA KUHUSU MCHEZO WA YANGA

Habari za Michezo

Baada ya kuipa Ihefu FC pointi tatu dhidi ya Yanga, kabla hajatupiwa virago kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema hana presha na mchezo ujao licha ya kuwa na matokeo mabaya, huku akidai kuwa hawaiogopi Yanga.

Mtibwa Sugar itakuwa ugenini Jumamosi dhidi ya Yanga ambao wanarudi kwenye ligi baada ya kukosekana kwa muda kutokana na kubanwa na ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katwila aliyejiunga na timu hiyo Oktoba, mwaka huu akitokea Ihefu FC, ameiongoza katika mechi sita na kushinda moja, ameliambia gazeti hili kuwa wanaendelea na maandalizi kuhakikisha kikosi kinarudi kwenye ushindani bila kujali wanakutana na timu gani.

Akizungumza Mwanaspoti kocha huyo alisema timu haina mwenendo mzuri hivyo ni lazima afanye kazi ya ziada kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa bila kuhofia mshindani wao huku akisisitiza kuwa mbinu na maandalizi bora ndivyo vitakavyoamua matokeo.

“Tutaingia kwa kuwaheshimu Yanga Jumamosi na siyo kuwaogopa tunacheza na timu yenye wachezaji 11 kama sisi na changamoto tunayoipitia ni kipindi cha mpito timu nyingi huwa zinapitia nyakati ngumu kama hizi matokeo haya hayanifurahishi, nimeandaa programu nyingine za mazoezi na kuwapa wachezaji muda zaidi wa mazoezi wa kuongeza viwango vyao,” alisema.

Kocha huyo alisema anataka kuiona Mtibwa Sugar ikiendelea kushiriki Ligi Kuu na kupanda juu katika msimamo. Katika msimamo, Mtibwa Sugar inaburuza mkia ikiwa na pointi tano baada ya kushuka dimbani mara 12.

Kocha huyo aliiongoza Mtibwa Sugar kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Geita Gold kabla ya kufungwa bao 1-0 na KMC kisha kupoteza 2-1 ilipocheza na JKT Tanzania na kukubali kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Azam FC huku ikikubali kufungwa mabao 2-1 na Tabora United kisha kuchapwa bao 1-0 na Namungo.

SOMA NA HII  YANGA NA MCHONGO HUU LIGI YA MABINGWA