Home Habari za michezo KOCHA YANGA AWAAMSHIA MASTAA, KISA HIKI HAPA

KOCHA YANGA AWAAMSHIA MASTAA, KISA HIKI HAPA

Habari za Yanga SC

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kila mchezaji aliye ndani ya kikosi cha Yanga ana umuhimu na ubora, huku akisisitiza kuwa mchezo wa kesho dhidi ya Medeama utaendelea kuibua maswali kwake nani aanze na yupi asubiri kutokana na idadi ya wachezaji wanaoanza.

Yanga licha ya mastaa wake wengi kukosa namba kikosi cha kwanza, wengi wako kwenye levo nzuri ya ubora na wana utimamu wa miili, hivyo hicho ndicho kinampa jeuri ya kuona kila mchezaji ni staa kikosini.

Gamondi amefunguka hayo siku moja baada ya kutoa nafasi kwa wachezaji ambao wamekuwa wakikosa namba kikosi cha kwanza kucheza kwa ubora ndani ya dakika 90, wakiipa timu hiyo ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Siwezi kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja. Nachoweza kusema Yanga ina wachezaji wengi wazuri na bora, lakini idadi ya wachezaji wanaotakiwa kuanza ni 11, hivyo napata wakati mgumu nani aanze kulingana na ubora lakini lengo la wote ni kuona timu inasonga mbele,” alisema.

“Juzi kulikuwa na mabadiliko mengi kikosini na hiyo imetoa mwanga namna Yanga ilivyo bora na inanipa mtihani wa kupanga kikosi. Nafurahishwa na hilo na najivunia kuongoza timu inayonipa matokeo bila kujali nani yupo na nani hayupo.”

Gamondi alisema wamesahau matokeo dhidi ya Mtibwa Sugar na sasa akili zao zimehamia kimataifa wakiamini bado wana nafasi ya kufanya vizuri huku akiweka wazi kuwa matokeo waliyopata yameongeza morali.

“Tumecheza mechi tatu bila matokeo mazuri kimataifa, kushinda kwenye ligi na kupata idadi kubwa ya mabao ni moja ya njia sahihi kuwarudisha wachezaji mchezoni,” alisema.

“Kuhusu mwendelezo wa wachezaji waliotumika dhidi ya Mtibwa Sugar kucheza kesho hilo kama kocha nitaliamua baada ya mazoezi ya mwisho kwani mchezaji ni binadamu – leo anaweza kuwa mzima na bora kesho ikawa tofauti.”

Gamondi alisema ushirikiano na ubora ulioonyeshwa na mastaa wake anatamani kuona unaendelea kimataifa ili kujihakikishia kucheza robo fainali jambo ambalo linawezekana wakipambana na kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa mechi mbili walizonazo.

Kesho Yanga itaialika Medeama kwenye Uwanja wa Mkapa ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia sare ugenini baada ya kufungana bao 1-1.

SOMA NA HII  POWER DYNAMO WAINGIA UBARIDI MBELE YA SIMBA KABLA YA KUINGIA UWANJANI, KOCHA ASEMA HAYA