Home Habari za michezo KUHUSU ALIPO ‘MSAKA WACHEZAJI’ WA SIMBA….AHMED ALLY AVUNJA UKIMYA….KUMBE HAISHI TZ…

KUHUSU ALIPO ‘MSAKA WACHEZAJI’ WA SIMBA….AHMED ALLY AVUNJA UKIMYA….KUMBE HAISHI TZ…

Habari za Simba

Mei, mwaka huu, Klabu ya Simba ilimtangaza skauti mkuu wa wachezaji, Mels Daalder ambaye ni raia wa Uholanzi ingawa hapo awali alikuwa akifanya na uongozi wa timu hyo kwa kuuletea wachezaji.

Miongoni mwa mastaa walioletwa na skauti huyo ni Ismail Sawadogo, Augustine Okrah na Pape Sakho ambao wote walishaondoka ndani ya Simba huku msimu huu akimleta Aubine Kramo pekee ambaye yupo nje ya uwanja baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.

Simba ilimuuza Sakho kwenye timu ya Union Sportive Quevillaise-Rouen Métropole ya Ufaransa inayoshiriki League 2 na akiwa amedumu ndani ya Simba kwa miaka miwili huku akitwaa tuzo ya bao bora kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sawadogo na Okrah wenyewe walivunjiwa mikataba baada ya kushindwa kuonyesha viwango bora ndani ya timu hiyo.

Kwa upande wa Kramo ambaye alisajiliwa msimu huu amefanyiwa upasuaji Oktoba na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili, hajacheza mechi hata moja akiwa amesaini mkataba wa miaka miwili na kuna tetesi za mchezaji huyo kutemwa katika dirisha hili.

Juzi, Jumamosi, dirisha dogo la usajili lilifunguliwa kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu, Championship, First League na ile ya Wanawake (WPL) ili kusajili nafasi ambazo zina upungufu tangu zianze kuchezwa na litanguwa Januari 16, 2024.

Hata hivyo, kumekuwepo na maswali kwa wadau wa soka nchini juu ya skauti huyo alipo wakihoji namna usajili wa Simba unavyofanywa kutokana na historia ya wachezaji wote aliowaleta kutokuwa na viwango bora ukiachana na Sakho ambaye alipata nafasi ya kucheza mechi nyingi kabla ya kuondoka.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema kwamba kipindi hiki ndicho cha skauti wao kutimiza majukumu aliyopewa na mabosi wake.

“Sio kwamba hayupo, yupo ila haishi hapa Tanzania. Majukumu yake makubwa ni kutuletea wachezaji kwani tayari anakuwa ameambiwa upungufu wa timu, hivyo yeye anawafuatilia huko na kuwaleta kama alivyoelekezwa,” alisema.

“Benchi la ufundi linakuwa limeshaona upungufu wa timu yetu, huwasilisha mabosi ambao humwambia skauti wetu aina ya wachezaji wanaotakiwa na kwa nafasi zipi. Akiwaleta lazima kocha ajiridhishe kama ndiyo aina ya wachezaji aliowataka.

“Kama kocha hajaridhika ambaye pia ana nafasi ya kupendekeza mchezaji anayemtaka basi atasema na ataletwa. Hivyo mashabiki wetu watambue kuwa skauti wetu yupo ila kazi yake kubwa ni kipindi kama hiki cha usajili.”

Hata hivyo, wakati Ahmed akielezea kuwa skauti huyo bado anaendelea na majukumu yake lakini habari za ndani ni kwamba benchi la ufundi na baadhi ya mabosi wa Simba ndiyo wanaotafuta wachezaji na kuwasajili kwa sasa.

Kuhusu ratiba ya kikosi chao, Ahmed alisema: “Baada ya mechi ya leo (juzi) na Kagera Sugar timu itaendelea na kambi. Hakutakuwepo na mapumziko kama inavyokuwa siku zote kwamba baada ya mechi wanaenda nyumbani maana ratiba yetu imetubana.

“Tukicheza na Kagera tuna mechi dhidi ya Wydad, KMC, Mashujaa, Tabora United na kuna Mapinduzi Cup, hivyo ratiba imebana ila tutapambana nayo kusaka ushindi.”

SOMA NA HII  NABI ANATAKA MABAO MENGI MBELE YA RIVERS UNITED