Home Habari za michezo MDOGO MDOGO…HIVI NDIVYO AYOUB LAKRED ANAVYOFUTA UFALME WA MANULA MSIMBAZI…

MDOGO MDOGO…HIVI NDIVYO AYOUB LAKRED ANAVYOFUTA UFALME WA MANULA MSIMBAZI…

Habari za Simba SC

Kiwango alichokionyesha kwenye mechi mbili zilizopita za Ligi ya Mabingwa Afrika, kimembeba kipa Ayoub Lakred kuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza na pia kunusurika na panga lililokuwa likitajwa linaweza kumpitia katika dirisha dogo linalofunguliwa leo hadi Januari 15 mwakani.

Ipo hivi. Ayoub alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa huenda wakapitiwa na panga ndani ya Simba, lakini ujio wa Kocha Abdelhak Benchikha na kujitonesha kwa Aishi Manula kumemhakikishia namba.

Kiwango bora alichoonyesha kwenye mechi mbili dhidi ya CAF dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na Wydad AC ya Morocco siku chache zilizopita, zimemfanya Ayoub kuwa lulu kikosini akitumiwa na Benchikha kwenye mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Ayoub aliyetua Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea FAR Rabat ya Morocco, amejihakikishia kubaki kutokana na ubora aliouonyesha, lakini sababu nyingine ni majeraha yanayomsumbua aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula aliyeumia awali Aprili 7 kwenye mechi ya ASFC dhidi ya Ihefu.

Kipa huyo alikaa nje kabla ya kuibuka kwenye Kariakoo Derby Novemba 5 na Simba kulala 5-1 kisha akaitwa timu ya taifa na huko alienda kujitonesha jeraha na kumfanya awe nje na kutoa nafasi kwa Ayoub kupata nafasi iliyomvutia Kocha Benchikha.

Inaelezwa kiwango alichokionyesha na kuumia huko kwa Manula kumelifanya benchi kuachana na mpango wa kumfyeka na sasa kumtegemea kama kipa namba moja akiwaweka benchi Hussein Abel na Ally Salim aliyekuwa namba moja baada ya Manula.

Licha ya Simba kutotoa taarifa kamili ya majeraha ya Manula, lakini Mwanaspoti linajua kipa huyo alitonesha eneo la nyoga na huenda akakaa nje ya uwanja hadi Februari mwakani.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopo sasa ni kwamba huenda Manula akazikosa mechi nne za ligi ikiwamo ya juzi dhidi ya Kagera na zile zijazo za KMC, Tabora United na Mashujaa, sambamba na mchezo wa CAF dhidi ya Wydad iliyomtema kocha wake, Adil Ramz pamoja na michuano mizima ya Kombe la Mapinduzi 2024.

SOMA NA HII  BANGALA AMKINGIA KIFUA FEI TOTO