Home Habari za michezo MTIBWA NAE KAPATA PA KUFUFUKIA

MTIBWA NAE KAPATA PA KUFUFUKIA

Klabu ya Mtibwa Sugar imetumia vyema uwanja wake wa Manungu Complex baada ya kuifunga Mashujaa mabao 2-1, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo huo mabao ya Mtibwa yalifungwa na Seif Karihe dakika ya 23 na Matheo Anthony dakika ya 73 huku lile la kufutia machozi kwa upande wa Mashujaa likifungwa na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Adam Adam dakika ya 41.

Ushindi huo kwa Mtibwa ni wa kwanza kwa timu hiyo baada ya kucheza michezo sita mfululizo na kuchezea kichapo tangu mara ya mwisho ilipofunga Geita Gold mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mechi iliyopigwa Oktoba 26, mwaka huu.

Licha ya ushindi huo ila Mtibwa inaendelea kuburuza mkia mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi nane baada ya kucheza michezo yake 14 ambapo kati ya hiyo imeshinda miwili na kutoa sare miwili huku ikichezea vichapo katika mechi zake 10.

Kwa upande wa Mashujaa huu ni mchezo wa tisa mfululizo kwa timu hiyo bila ya kushinda tangu mara ya mwisho ilipoifunga Ihefu mabao 2-0, Septemba 16, mwaka huu na kuifanya kupoteza mchezo wake wa saba msimu huu kati ya 12 iliyocheza.

Katika michezo hiyo 12, Mashujaa imeshinda miwili, sare mitatu na kupoteza saba ikiendelea kubaki nafasi ya 15 na pointi tisa.

SOMA NA HII  KUMEKUCHA FEI TOTO ATAKA KULIANZISHA TENA AZAM, ADAI HANA FURAHA