Home Habari za michezo GAMONDI AWAPA NENO MASHABIKI KUELEKEA MCHEZO WA MADEAMA LEO

GAMONDI AWAPA NENO MASHABIKI KUELEKEA MCHEZO WA MADEAMA LEO

Habari za Yanga SC

Kuelekea mchezo wa leo Jumatano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu ya Yanga SC dhidi ya Medeama, kocha mkuu wa kikosi cha Yanga, Miguel Angel Gamondi, amesema ni muhimu zaidi kushinda kuliko kitu kingine.

Gamondi ameenda mbali zaidi na kusema kwamba, katika uwanja wa mazoezi, ameiandaa timu yake kushinda mchezo huo ili kujiweka timu kwenye mazingira mazuri zaidi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Leo Jumatano, Yanga itakuwa mwenyeji wa Medeama katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D utakaochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Kwetu ni mchezo mgumu sana, naweza kusema ni mchezo mkubwa kwa sababu tunatakiwa kushinda pointi tatu ili kutuweka katika sehemu nzuri kwenye kundi. Licha ya kwamba kundi bado lipo wazi, lakini kwetu pointi tatu ni lazima kesho (leo).

“Sio ngumu sana, kwa sababu tangu mwanzo wote tulikuwa tunajua tunahitaji kushinda, hata wachezaji wanafahamu umuhimu wa mchezo huu.

“Tumejiandaa vizuri sana kimbinu na kila kitu, kesho utakuwa ni mchezo wa akili sana, tunakwenda kucheza na timu nzuri sana, hatuwezi kuruhusu makosa ya kutushambulia hata kwa kutushtukiza.

“Mchezo ni wa dakika tisini, lazima muda wote tuwe makini, tunahitaji kufahamu namna ya kutumia mbinu kuweza kushinda.

“Sote tulifanya makosa katika mchezo wa kwanza, tumekaa na kuangalia udhaifu wa Medeama na tumejaribu kufanyia kazi na kuweka msisitizo katika mbinu zetu juu ya makosa ya Medeama.

“Ninaamini kesho (leo) wachezaji watakuwa vizuri kwa sababu nina furaha kwa aina ya wachezaji tulionao, wamefanya kazi vizuri kipindi cha maandalizi, ninaamini kesho tutaonesha mabadiliko ambayo nimeyaona katika maandalizi yetu. Hii inatosha kutupatia pointi tatu.

“Nawaomba mashabiki wa Yanga waje uwanjani kutusapoti, ninawafahamu mashabiki wa Yanga watakuja kutusapoti, kuna wakati mambo yanaenda tofauti, lakini bado wanakuwa nyuma ya timu, tumefanya kila liwezekanalo katika maandalizi ili kupata kitu kizuri na kesho tuna matumaini ya kushinda Mungu akipenda,” alisema Gamondi.

Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya hivi sasa kuwa na alama mbili zilizotokana na kucheza mechi tatu.

SOMA NA HII  MBRAZILI SIMBA MPYA IMEENEA.... YANGA MPYA HAPO VIPI...