Home Habari za michezo SIMBA NA MZIMU WA SARE ULIOKITA MIZIZI MSIMBAZI

SIMBA NA MZIMU WA SARE ULIOKITA MIZIZI MSIMBAZI

Mzimu wa sare umeendelea kuiandama Simba baada ya jana Jumamosi (Desemba 2, 2023) kushindwa kutamba katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kulazimishwa suluhu na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume.

Simba iliingia katika mchezo huo wa kundi B ikihitaji ushindi baada ya mchezo wa kwanza wa hatua hiyo uliopigwa Novemba 25, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kutoka sare ya bao 1-1 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Sare hiyo ni ya tatu mfululizo kwa Simba katika mashindano yote huku ikizidi kuweka presha zaidi ndani ya kikosi hicho kwani mara ya mwisho kupata ushindi ulikuwa wa mabao 2-1, dhidi ya Ihefu katika Ligi Kuu Bara Oktoba 28, mwaka huu.

Mchezo wa jana ni wa kwanza kwa kocha mkuu wa timu hiyo Mualgeria, Abdelhak Benchikha tangu alipojiunga na kikosi hicho Novemba 24, akichukua nafasi ya mtangulizi wake Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa Novemba 7, mwaka huu.

Simba iliingia katika mchezo huo ikihitaji kulipa kisasi dhidi ya Jwaneng baada ya msimu wa 2021/22 kutupwa nje ya mashindano hayo kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini kufuatia mechi mbili baina yao kuisha kwa sare ya mabao 3-3.

Simba imeendeleza rekodi mbovu inapocheza ugenini katika michuano ya Klabu Afrika kwani kwenye michezo 11, imeshinda mitatu, sare mitatu na kupoteza mitano.

Kwa matokeo hayo yanaifanya Simba kushika nafasi ya pili na pointi mbili baada ya michezo miwili huku Jwaneng ikiongoza na pointi nne ikifuatiwa na ASEC Mimosas yenye moja ambayo saa 4:00 usiku itacheza na Wydad Casablanca iliyopoteza mechi ya kwanza.

SOMA NA HII  KAMA YANGA INATAKA USHINDI LEO BASI JAMBO HILI LAZIMA WALIACHE