Home Habari za michezo HIVI NDIVYO SIMU YA ENG HERSI ILIVYOTIBUA DILI LA ‘TRY AGAIN’ NA...

HIVI NDIVYO SIMU YA ENG HERSI ILIVYOTIBUA DILI LA ‘TRY AGAIN’ NA SIMBA YAKE…

Habari za Yanga

YANGA imemalizana na kiungo kiraka Shekhan Khamis Ibrahim akitokea JKU ya Zanzibar ikiwapokonya tonge mdomoni watani wao Simba, lakini filamu nzima ilikuwa hivi.

Simba ilikuwa klabu ya kwanza kumfuata Shekhan, aliyeng’ara kwenye michuano ya Vijana ya U18 ya nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), lakini wakiwa wamebakiza hatua chache tu kukamilisha dili hilo wakazembea na hapo ndipo Yanga ikafanya mambo na kumbeba juu kwa juu.

Wekundu hao hadi juzi walibakiza hatua ya chache kumalizana kifedha na kinda huyo anayemudu kucheza nafasi nne tofauti ndani ya uwanja, lakini wakachelewa.

Mmoja wa wasimamizi wa Shekhan alifichua, Simba ilikuwa inahitaji baraka za Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyekuwa nje ya nchi kumaliza dili hilo.

“Wao Simba watajilaumu sana kama mchezaji huyu atawika Yanga, walishafanya kila kuanzia mazungumzo hadi makubaliano kwa pande zote likabaki suala la kumalizana tu,” alisema kaka huyo wa Shekhan aliyekataa kutajwa jina gazetini

“Hivi karibuni tukazungumza nao tena wakasema wanamsubiri bosi wao yuko nje ya nchi kwamba basi watakuja kumalizana wakija kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ili nao viongozi wa juu wamuone pamoja na kocha wao.

“Jana (juzi) tukawapa taarifa klabu zimeanza kusumbua wakimtaka dogo (Shekhan) ndio wakashtuka wakasema wanatuma pesa ya boti ili mchana asafiri aje huko Dar wamalizane kwa hatua za awali sisi tukasema sawa.”

Baada ya hatua hiyo ya Simba, mabosi wa Yanga chini ya Eng Hersi Said ambaye ni Rais wa Klabu hiyo wakaibuka na maamuzi kamili ambapo fasta wakatangulia kumalizana na JKU, kisha wakahamia kwa mchezaji na kumaliza kila kitu.

Yanga haikuishia hapo wakatuma haraka tiketi ya ndege ya kutoka Zazibar kuja Dar es Salaam, huku kila kitu kikienda kwa haraka kwa usimamizi wa makamu wa Rais wa klabu hiyo, Arafat Haji.

“Yanga walikuja kama moto wa gesi waliuliza alipo mchezaji tulipowaambia yuko Unguja wakasema asifanye maamuzi yoyote wakamalizana na JKU hapo.

Chanzo hicho kiliongeza kwa kusema;

“Walipomaliza kuzungumza klabu yule kiongozi wao (Arafat) akahamia kwa mchezaji nako wakakubaliana wakizidi hata kile kiasi alichotakiwa kupewa na Simba na baadaye wakamwambia aachane na mambo ya boti abadili njia na kuelekea uwanja wa ndege tiketi ataikuta hapo.

“Kweli kuna gari ikatufuata na JKU walishatupa taarifa kwamba wao wameshamalizana na Yanga na wanamruhusu Shekhan azungumze nao kuhusu maslahi yake

“Ule mchana sasa ambao Simba walikuwa wanasubiri kutusafirisha wakati wanatupigia sisi tunatoka uwanja wa ndege hapo Dar na kwenda kwa viongozi wao kule Posta.”

Shekhan 18, aina ya uchezaji wake inatajwa kufananishwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kwenye Ligi ya Zanzibar tayari amefunga mabao mawili likiwemo alililowatumbua watetezi, KMKM walipoilaza mabao 2-1 na pia ameasisti mara tatu hadi sasa.

SOMA NA HII  BAADA YA KUTUNGULIWA KIMOJA DAR...WYDAD WAAMUA KUFANYA MAAMUZI HAYA MAZITO...