Home Habari za michezo UIMARA WA LAKRED NA TATIZO LA MSINGI PALE SIMBA….HATMA YA MANULA IPOJE…?

UIMARA WA LAKRED NA TATIZO LA MSINGI PALE SIMBA….HATMA YA MANULA IPOJE…?

Habari za Simba SC

ALIANZA kwa kusuasua pale Lusaka Zambia. Akafungwa bao la kijinga la mbali. Ilionekana maisha yangeendelea kuwa rahisi kwa kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula baada ya kumuona rafiki yetu, Ayoub Lakred akibabaika katika lango la Simba pale Lusaka.

Hata hivyo, kuanzia pale maisha yamebadilika na Ayoub hajatazama tena nyuma. Amekuwa imara kama chuma katika lango la Simba. Basi tu ni vile Simba iliruhusu bao la dakika za jioni katika pambano dhidi ya Wydad pale Morocco lakini tayari Ayoub alishaibuka shujaa baada ya kuicheza penalti ya wenyeji.

Langoni Ayoub ni imara katika kucheza michomo ya wapinzani. Anajua kujipanga vema lakini pia ni mzuri miguuni kama inavyotakiwa kwa makipa wengi wa kisasa. Haya yote yamekuja kuleta shida ya msingi pale Simba. Ni kweli walitamani kipa mzuri kumsaidia Aishi Manula lakini kuwa na kipa imara kutoka nje ni tatizo kidogo kwa Simba.

Kama Aishi akirudi, nani atakuwa kipa namba moja? Nafasi kubwa itaenda kwa Aishi. Kila shabiki anapenda kuwa na timu yenye makipa wawili mahiri. Tatizo wakati mwingine ni vigumu kuwafanya makipa wawili mahiri kuwa na furaha. Hii ni nafasi ambayo kocha huwa hafanyi mabadiliko ya mara kwa mara. Kipa namba moja anabakia kuwa kipa namba moja.

Tatizo la nchi zetu maskini ni ngumu kumfanya kipa wa kigeni kuwa kipa namba mbili. Kinachotokea kwa watani wao ndicho ambacho kinapaswa kutokea. Una kipa namba moja wa kigeni halafu mabenchi wawili wazawa. Ni ngumu kwa kipa namba moja kuwa mzawa halafu benchi wake akawa mgeni. Ni upotevu wa hela.

Katika nafasi ya ukipa mara nyingi unaweza kuwa na makipa wawili waliotofautiana umri au matamanio. Unakuta kipa wa kwanza ni mahiri halafu msaidizi wake labda ana umri mkubwa na ameshapita muda wa kucheza kiwango cha juu au ni kinda aliyeridhika kukaa benchi na kujifunza hapa na pale. Maisha yanakuwa magumu ukiwa na makipa wote wanaoipambania nafasi ya kwanza kama ilivyo sasa pale Simba.

Hapo hapo Simba haina furaha sana na kikosi chake kwa sasa. Katika dirisha dogo la usajili lijalo pamoja na lile kubwa watafanya mabadiliko makubwa kikosini. Mashabiki wanatazamia kuona vifaa vipya. Tatizo unalazimika kukata baadhi ya wachezaji wa kigeni kwa ajili ya kushusha vifaa vipya. Naona kuna kundi kubwa la wachezaji wa kigeni wanaoweza kubakia kuliko wanaoweza kuondoka.

Henock Inonga, Clatous Chotta Chama, Che Malone, Moses Phiri, Jean Baleke, Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma, Lakred mwenyewe hawaonekani kama ni wachezaji wanaoweza kuachwa kwa sasa. Unaweza kuamini kwamba Jose Luis Miquissone anaweza kuachwa lakini kwa hao sidhani kama wanaweza kuachwa.

Kumekuwa na mabadiliko ya vipindi vya hali hewa pale Simba. Kwa mfano, kuna wakati ilikuwa inaonekana kama vile Phiri angeweza kuondoka kutokana na kuwekwa benchi na kocha Robertinho. Ghafla kocha ameondoka na Phiri amerudi katika mipango ya timu. Nasikia watani zao walikuwa wanamnyemelea kimya kimya. Watani pia waliwahi kumtaka kabla hajaenda Simba.

Kuna Willy Essomba Onana. Alikuwa anasugua benchi katika utawala wa Robertinho. Mpaka leo mashabiki wengi hawaridhishwi na kiwango chake lakini ghafla amegeuka kuwa kipenzi cha kocha. Sijui itakuwaje kama kocha Abdelhak Benchikha akiendelea kuwa klabuni hapo mpaka baada ya msimu huu. Nadhani anaweza kuwaambia viongozi kuwa anamuhitaji Onana.

Mchezaji mwingine ambaye hatima yake haieleweki sana klabuni ni Aubin Kramo. Wanaomjua wanadai kwamba licha ya kuwa na majeraha kwa muda mrefu lakini ni miongoni mwa usajili bora uliofanywa na Simba katika dirisha kubwa lililopita. Kama akirudi uwanjani na kufanya mambo ya maana basi atayumbisha vichwa vya viongozi mwishoni mwa msimu.

Licha ya minong’ono ya hapa na pale kuhusu Chama lakini sioni kiongozi wala kocha mwenye uthubutu wa kumuondoa staa huyu wa Zambia pale kikosini. Na ingawa kwa sasa anatokea katika benchi lakini naamini muda wowote kabla ya msimu kumalizika atakuwa amewakumbusha mashabiki wa Simba uhodari wake. Wakati fulani miguu ya Chama inakuwa na maajabu ambayo yanakubadili mawazo yako mabaya kuhusu yeye.

Ukweli ni kwamba sasa hivi tunasikia wachezaji wengi wa kigeni wakihusishwa kujiunga na Simba. Hata hivyo, watatakiwa wageni kadhaa wakatwe ili kuweza kutimiza idadi ya wachezaji 12. Chukulia mfano kama Simba italeta wachezaji wanne au watano wa kigeni. Lakini hapo kuna kundi la wachezaji kama tisa wanaoweza kubakia klabuni. Nani atakatwa?

Hapa ndipo unaweza kuja uamuzi mgumu kuhusu kipa wetu Lakred. Anaweza kutolewa kafara kwa ajili ya nafasi yake kwenda kwa mchezaji wa ndani wa kigeni. Labda kama akihakikishiwa kwamba yeye ni namba moja katika kikosi cha Simba. Itawezekana kwa kipa namba moja wa timu ya taifa kuwa kipa wa pili Simba? Ni swali la kujiuliza.

Na hauwezi kuwafanya makipa wa namna hii, hodari wote wawili na waliokaribiana umri wawe katika lango moja. Inatokea kwa sasa pale Arsenal. Mikel Arteta ameshindwa kuwaridhisha kwa pamoja makipa, David Raya na Aaron Ramsidale. Ni wazi kwamba Ramsidale hana furaha na ana mpango wa kuondoka Arsenal.

Akibaki ina maana nafasi yake ya kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya England inakuwa finyu. Nafasi yake ya kucheza michuano ya Euro 2024 inakuwa ngumu zaidi huku kipa wa Everton, Jordan Pickford anayecheza kila wiki akiwa katika nafasi nzuri zaidi ya kucheza michuano hiyo.

Kinachofurahisha kwa Simba ni kwamba kwa muda mrefu kuna wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza nafasi zao hazipo hatarini. Baada ya muda mrefu sasa tunaona walau nafasi ya Aishi ipo hatarini. Huu ni ushindani unaotakiwa katika timu lakini bahati mbaya yenyewe ni kwamba ushindani wenyewe umeangukia katika nafasi isiyohimili sana ushindani. Lazima mshindi awe mmoja tena kwa haraka.

Bahati mbaya zaidi ni kwamba tupo katika taifa ambalo halina mechi nyingi kiasi cha kudai kwamba inabidi umpumzishe mmoja. Ligi ina timu 16. Michuano ya Ligi ya Mabingwa ina mechi nane kama utafanikiwa kutinga hadi robo fainali. Michuano ya Shirikisho unaweza kuwa bingwa baada ya kushinda mechi sita au saba.

Tusubiri na kuona lakini litakuwa dirisha kubwa lenye kuvutia mwishoni mwa msimu kwa Simba. Vifaa vitakavyoletwa huenda vikasababisha viongozi wa Simba wachukue uamuzi mzito kwa baadhi ya wachezaji wa kigeni. Rafiki yangu Ayoub ameongeza utata katika maamuzi hayo.

Wachezaji wazawa bado wapo salama pale kikosini. Hakuna wachezaji wengi wazawa nje ya Simba ambao wanaweza kuleta ushindani mkubwa wa namba za wazawa ndani ya Simba. Labda ukawachukue wazawa wa Yanga au Azam. Kitu ambacho kwa kiasi kikubwa hakiwezekani kwa nyakati hizi za ushindani baina yao.

Credit:- Edo Kumwembe/Mwanaspoti

SOMA NA HII  ZAHERA AFICHUA SIRI YA KURUDI KWAKE YANGA...AIBUA KAULI MBIU YAKE YA 'ZAHERA MPYA'