Home Habari za michezo YANGA CAFCL WARUDISHA AKILI KWA MKAPA BAADA YA KUSHINDWA KUTAMBA UGENINI

YANGA CAFCL WARUDISHA AKILI KWA MKAPA BAADA YA KUSHINDWA KUTAMBA UGENINI

Habari za Yanga

Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Medeama juzi, mechi mbili zijazo za nyumbani zimeshikilia kwa kiasi kikubwa ndoto za Yanga kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ingawa bado inahitajika kuiombea mema Al Ahly katika mechi zake mbili zinazofuata dhidi ya CR Belouizdad na Medeama.

Yanga inapaswa kuibuka na ushindi katika mechi hizo dhidi ya Medeama na Belouizdad ili ifikishe pointi nane zitakazoifanya ifuzu kabla ya mechi ya mwisho kwenye kundi lake D ikiwa Al Ahly haitoruhusu kufungwa na Belouizdad na Medeama katika michezo inayofuata.

Medeama na Belouizdad zikipoteza mechi mbili zijazo kwa kila moja na Yanga ikashinda, timu hiyo inayowakilisha Tanzania itasonga mbele kwani haitoweza kufikiwa na Beloizdad na Medeama ambazo zitajikuta kila moja ikiwa na uwezekano wa kumaliza na pointi saba tu.

Lakini kama Yanga haitopata ushindi katika mechi mbili zijazo dhidi ya Medeama na CR Belouizdad hesabu zake za kwenda robo fainali zitakuwa ngumu zaidi hasa iwapo Al Ahly itashindwa kuifunga timu mojawapo katika ya Belouizdad na Medeama.

Mtihani mwingine unaoikabili Yanga ni wa kuhakikisha inapata ushindi mnono dhidi ya CR Belouizdad, Februari 23 ili ikitokea timu hizo zimelingana kwa idadi ya pointi, ibebwe na kanuni ya kunufaika na mabao ya ugenini katika kuamua mshindi iwapo timu mbili zimelingana pointi kwani katika mechi ya kwanza baina yao, Yanga ilipoteza kwa mabao 3-0.

Kitendo cha Al Ahly kupoteza mechi mojawapo au zote dhidi ya Belouizdad na Medeama, kitaiweka Yanga katika nafasi ngumu zaidi kwa timu hizo mbili zitakuwa na uwezekano wa kupata pointi zaidi ya nane ambazo Yanga inazitegemea zichangie kuibeba kwenda robo fainali.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema wanazipa uzito mkubwa mechi mbili zijazo za nyumbani dhidi ya Medeama na Belouizdad wakiamini matokeo tofauti na ushindi yatawaweka katika nafasi ngumu zaidi.

“Nina furaha kwa namna tunavyocheza na ninaamini tunaweza kufanya vizuri, kwa nini isiwe hivyo. Ni kushinda mechi tatu zilizobakia uende hatua inayofuata. Ninaridhika na kupiga hatua kwa timu. Yanga inastahili kupata pointi nyingi zaidi ya hizo tulizonazo.

“Ninawaahidi nitapambana hadi mechi ya mwisho. Hata kama tupo nafasi ya mwisho katika kundi tunapaswa kuamini na kama ilivyo kauli mbiu ya Yanga, daima mbele nyuma mwiko,” alisema Gamondi.

Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema mechi zao mbili zinazofuata ni kama fainali na watahakikisha wanaibuika na ushindi.

“Tunaporejea nyumbani tunakwenda kurekebisha matokeo na mazoezini kufanyia kazi makosa yote tuliyoyafanya kwani kocha atakuwa ameshajua nini cha kuboresha kwani alitutia moyo kwa kutuambia kundi liko wazi bado.

Hakuna kingine zaidi ya ushindi tu katika uwanja wa nyumbani ili kujiweka katika mikono salama kwani wanaocheza wote ni mabingwa wa nchi zao kwa hiyo kwa sisi kupata sare ugenini ni jambo la kawaida ijapo tutalifanyia kazi,” alisema Mwamnyeto.

Baada ya matokeo ya mechi za juzi, Al Ahly inaongoza msimamo wa kundi D ikiwa na pointi tano ikifuatiwa na Medeama na Belouizdad ambazo kila moja imekusanya pointi nne huku Yanga ikishika mkia na pointi zake mbili.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUDAKA MECHI ZOTE KWA KIWANGO KIKUBWA...HAULE AIBUKA NA HILI KUHUSU MSHERY...AMTAJA DIARRA...