Home Habari za michezo BILIONI 10 ZATAKIWA TIMU ZA TAIFA…RAIS SAMIA ACHANGIA MILIONI 500…

BILIONI 10 ZATAKIWA TIMU ZA TAIFA…RAIS SAMIA ACHANGIA MILIONI 500…

Taifa Stars leo

Kamati ya hamasa ya timu za Taifa Tanzania imesema kiasi kinachohitajika kwa ajili ya kuzichangia timu za taifa ni Sh10 bilioni.

Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya timu za Taifa, Theobald Sabi amesema kiasi kitakachokusanywa katika awamu ya kwanza ya michango hiyo kitakabidhiwa katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu.

“Awamu ya kwanza itakamilika ndani ya miezi mitatu kwa hiyo kamati yetu itakabidhi michango ndani ya siku 90. Nitumie fursa hii kuwaomba wadau wachangie.

“Lengo hili la kukusanya kiasi cha Sh10 bilioni tutalifanikisha. Kamati hii ina majukumu matatu. La kwanza ni kukusanya fedha kutoka kwa wadau ambazo zitatumika kwa timu za taifa.

“Kuelimisha umma kuhusu uwepo wa timu za taifa na kuhamasisha umma kuhusu kuchangia timu za taifa. Kamati yetu imejiwekea mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu,” alisema Sabi.

SAMIA ATOA MILIONI 500.

Rais Samia Suluhu Hassan amechangia Sh500 milioni katika harambee ya kuzichangia timu za Taifa inayoendelea hapa Dar es Salaam.

Akizungumza moja kwa moja kwa njia ya mtandao na wadau wa michezo waliojitokeza katika harambee hiyo, Rais Samia amesema kuwa mchango huo ni mwendelezo wa juhudi za serikali kukuza michezo.

“Michezo pia ni gharama ndugu zangu. Serikali imejitahidi, tumehamasisha, timu zetu zinasonga mbele lakini tumefika mahala tuna uchache wa bajeti. Wito wangu na ombi langu kwenu Watanzania wenzangu, tuchangie timu zetu ili ziende kuwakilisha jina la Tanzania.

“Kwa kuanzia mimi na marafiki zangu wameniahidi kwa kusema tutachangia Sh500 milioni. Niwaombe sana shughuli iende vizuri, niwaombe ndugu zangu tuendelee na michango,” amesema Rais Samia.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ndiye anaongoza harambee hiyo, alisema kuwa lengo kuu ni kukusanya kiasi cha Sh10 bilioni ambacho kitagawanywa kwa timu za taifa za michezo tofauti.

SOMA NA HII  KISA DIARA...YANGA YAFIKIRIA KUSAJILI KIPA MWINGINE...INJINIA HERSI AANIKA MPANGO MZIMA...