Home Habari za michezo MAROUF TCHAKEI KUTUA SIMBA DIRISHA KUBWA…? UKWELI UNAOFAA KUJUA HUU HAPA…

MAROUF TCHAKEI KUTUA SIMBA DIRISHA KUBWA…? UKWELI UNAOFAA KUJUA HUU HAPA…

Habari za Simba leo

Umewatazama Barcelona kwa siku za karibuni. Wamekuwa tena sio timu ya mfano. Hawachezi lile soka lao lililokuwa likiwafanya wengi watamani kucheza kama wao. Kuna mahali walikosea.

Hawakutaka kujifunza kutoka kwa mahasimu wao, Real Madrid. Real Madrid imeifundisha Barcelona somo moja tu – kutafuta mbadala ingali mapema.

Barcelona ilichelewa kujiandaa na maisha baada ya Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Lionel Messi. Haikutafuta mbadala sahihi hata alipoondoka Neymar. Na sasa Barcelona imekuwa kawaida sana. Real Madrid ilifahamu mapema kuna maisha baada ya Cristiano Ronaldo. Maisha baada ya Karim Benzema.

Inatambua kwamba kuna maisha baada ya Toni Kroos, Luka Modric na Sergio Ramos. Mapema tu ikawasajili watu mapema wa kuja kuziba nafasi za wababe hao. Ilitembea na ule msemo wa Kata mti, panda miti.

Kuchelewa kupata mbadala sahihi ndiko kunakozigharimu Manchester United na Chelsea kwa sasa. Kuna wakati Man United ilikuwa na fowadi yenye wakali kama Wayne Rooney, Ronaldo, Carlos Tevez na Dimitar Berbatov.

Kulikuwa na Chicharito na Louis Saha. Wakajisahau kufanya uamuzi wa kuleta mbadala sahihi, matokeo yake wakajikuta wamebaki na kina Danny Welbeck, mara Anthony Martial na wakamfanya Marcus Rashford kuwa silaha yao kubwa.

Hiyo sio kariba ya timu kubwa. Chelsea haijapata mtu sahihi baada ya Didier Drogba na Diego Costa kuondoka. Maisha yamekuwa magumu.

Kwenye soka, kama kuna eneo ambalo mchezaji aliyepo anakupa huduma bora, anakupa matokeo mazuri, basi mkazo mkubwa unapaswa kuwekezwa katika kutafuta mbadala wake, ingali mapema ili ajifunze na pengine kuwa bora nyakati zitakapofika na kukabidhiwa mikoba. Kuchelewa kufanya uamuzi wa aina hiyo kutakulazimisha kufanya usajili wa kujaza nafasi.

Hadithi hii inaweza kuwahusu Simba. Wekundu wa Msimbazi wanafahamu wazi kuna wachezaji wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chao na zama zao zinaelekea ukingoni, lakini bado hawajafanya uamuzi wa kutafuta mbadala wao mapema.

Matokeo yake itakuja kusajili kwa kuongeza idadi na si kupandisha ubora. Kwenye dirisha dogo la usajili, Simba imeachana na washambuliaji wake Jean Baleke na Moses Phiri. Washambuliaji wa kiwango cha juu kwa ubora wa soka letu.

Simba inavuna kitu kutoka kwa Saido Ntibazonkiza. Inavuna kikubwa sana kutoka kwa Clatous Chama. Wawili hao hawana maisha marefu kwenye kikosi. Muda unakwenda kasi na umri nao unapepea. Wako wapi wabadala wao?

Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute hilo ni kundi jingine muhimu. Wako wapi wabadala wao. Kuna Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Henock Inonga wako wapi wabadala wao? Kariba ya timu kubwa haipaswi kuweka daraja kubwa baina ya mchezaji anayeanza na atakayekuwa benchi badala yake.

Hiyo haitakuwa maana halisi ya kuwa na kikosi kipana. Lakini, kubwa na muhimu ni la kutengeneza mbadala mapema.

Kwenye dirisha dogo la usajili, wakati Simba inaachana na Baleke na Phiri ilihusishwa na mchezaji wa Singida Fountain Gate, Marouf Tchakei kabla hajakwenda kujiunga na Ihefu.

Huduma maridhawa ingefanikiwa kuinasa. Tchakei ameonyesha kitu kwenye soka la ndani. Ameonyesha kitu kwenye soka la kimataifa akicheza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika (CAF). Ana kitu ambacho Simba inahitaji kuwa nacho kwenye kikosi.

Bila shaka katika dirisha kubwa la usajili la mwisho wa msimu, Simba itakuwa siriazi kurejea kwenye meza ya Tchakei kuulizia upatikanaji wa huduma yake hasa wakati huu ambao inafikiria mustakabali wa maisha yake baada ya Chama.

Kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2024, Simba ilionekana kukosa huduma sahihi ya namba 10. Ilikosa huduma ya mtu aina ya Chama. Yule wa kutulia na mpira nje ya boksi la timu pinzani na kupiga pasi za kuamua mpira uende kushoto au kulia na kutengeneza nafasi za kufunga. Hilo ni pengo na linahitaji kuzibwa kwa haraka. Tchakei anaweza kuipa Simba kile ambacho inakitaka.

Sio mchezaji wao, lakini huko Ihefu aliko hana mkataba wa maisha. Na si kwamba hanunuliki. Wakati mwingine ni bora kusajili mchezaji ambaye ameonyesha mbele ya macho yako kile ambacho anaweza kukifanya ndani ya uwanja.

Simba ingefanikiwa kunasa saini ya Tchakei kwenye dirisha dogo, ingekuwa imepiga bao la maana. Uzuri wa kuwa na Tchakei kwenye kikosi anampa kocha wigo mpana wa machaguo kwenye upangaji.

Staa huyo wa Togo anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji, hivyo anaweza kutumika kwenye namba 10 na kuwa mbadala wa Chama. Tchakei anaweza kucheza kama winga, hivyo kuwa naye unaweza kumkabidhi buti za Saido akapiga mzigo.

Tchakei ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa kati akakupa chaguo la kuwa na watu wengi katikati ya uwanja kwenye mechi ambazo kocha atahitaji kuwabana wapinzani kwa kuwa kwenye umiliki mpira muda mrefu. Tchakei ni risasi moja inayoua ndege watatu.

Dirisha dogo limefungwa, lakini dirisha kubwa halina muda mrefu kuanzia sasa na hakika kama lisemwalo lipo kwamba, Simba ilijaribu kunasa saini ya Tchakei kwenye usajili uliopita ni huduma muhimu wanayoihitaji kwenye kikosi kwa sababu ni mchezaji mmoja anayeweza kumpa kocha Abdelhak Benchikha machaguo zaidi ya manne ya upangaji wa kikosi akicheza winga, namba 10, kiungo wa kati na wakati mwingine anaweza kutumika kama namba 9 bandia.

Kwenye ile fomesheni pendwa ya Benchikha ya 4-2-3-1, Tchakei anaweza kucheza kwenye kila nafasi katika huo mstari wa mastaa watatu nyuma ya mshambuliaji wa kati, lakini pia anaweza kucheza kwenye ule mstari wenye wachezaji wawili, kwa maana akitumika kama namba 8 na pia anaweza kuwa kwenye huyo mmoja wa mbele na kuongoza mashambulizi kwa sababu ana macho pia ya kuliona goli na kufunga.

Nyota huyo wa kimataifa wa timu ya taifa ya Togo, alinukuliwa mapema baada ya kuhusishwa na Simba kwa kusema, hashangazwi na kunyemelewa na timu kubwa kama hiyo, kwani kipindi hicho dirisha la usajili lilikuwa wazi.

Pia alisema bado ana mkataba wa Singida Fountain Gate iliyomelta nchini kabla ya kuibukia Ihefu na kusema kama kweli Simba ina nia ya kumsajili inapaswa kuzungumza na mabosi wake ili mambo yasiwe mengi, kwani kwa sasa ni vigumu kuzungumzia dili hilo kwa vile atakuwa anavunja mkataba alionao na timu yake ya sasa.

Katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Tchekei mwenye umri wa miaka 28 na aliyewahi kuzichezea timu za Gbikinti na ASKO Kara za kwao Togo na AS Vita ya DR Congo kabla ya kunyakuliwa na Singida aliyojiunga nayo Julai mwaka jana amefunga mabao matano akiwa na kikosi hicho alichoachana nacho.

Pia alihusika kuifungia mabao matatu katijka michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na Singida ilikwamia kwenye raundi ya pili, akifunga mawili dhidi ya JKU mechi ya raundi ya kwanza kisha kuongeza jingine walipoenda kulala 4-1 mbele ya Future ya Misri, kuonyesha sio mchezo mwepesi mwepesi uwanjani.

SOMA NA HII  RASMI...LIGI YA BONGO SASA KAMA MBELE TU...WACHEZAJI KULIPWA VIINUA MGONGO WAKISTAAFU...

2 COMMENTS

  1. Haya yoote uliyoandika unadhani kuna la maana hata moja? Ukiyasoma yote ni mawazo na hosia zako wewe binafsi jinsi unavyoziona hizo timu na siyo technical opinions, hakuna mahala popote kwa mfano Bacelona ilipokiri kufanya kosa kwenye usajiri wake au ilipokiri kupata somo kwa Madrid. Ni mawazo yako, amvayo yanatawaliwa na hisia zako. Inaonesha hukujipanga wala kujiandaa kuandika makala yenye mashiko. Nashauri fanya tafiti kabla ya kuandika.

  2. Mimi ni mwanasimba wa damu, jamani tunaposhindwa kufanya mazuri inakuwa inaumiza sana, naomba kama mshibiki wa chama langu jitahidini kusajili wachezaji wenye uwezo na mpira, inaumiza sana ujue.