Home Habari za michezo …’BACCA’ APEWA UBEKI BORA AFRIKA….FEI TOTO KWENDA KUKIPIGA ULAYA BAADA YA AFCON…

…’BACCA’ APEWA UBEKI BORA AFRIKA….FEI TOTO KWENDA KUKIPIGA ULAYA BAADA YA AFCON…

Taifa Stars

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Adel Amrouche amemtaja beki wa Yanga na Taifa Stars, Abdallah Hamad ‘Bacca’ kuwa ni mchezaji Bora anaecheza eneo hilo Afrika kwa sasa.

Mbali na Bacca Amrouche amewataja viungo wa Azam FC, Sospeter Bajana na Feisal Salum ‘Fei toto’ kuwa ni wachezaji wazuri huku akimzungumzia zaidi Fei Toto kuwa ni kiungo ambaye anamuona mbali baada ya Fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zinazotarajiwa kuchezwa Ivory Coast.

Amrouche amefunguka hayo muda mchache baada ya kutangaza kikosi cha timu ya Taifa kitakachoiwakilisha Tanzania kwenye michuano hiyo akitaja majina 31 huku mchujo mwingine ukipangwa kufanyika baada ya mechi za kirafiki nchini Misri.

Akizungumza na waandishi wa habari saa chache kabla ya kuondoka alisema anafurahishwa na uwezo mkubwa wa Bacca huku akimtaja kuwa ni beki bora wa Afrika kwa sasa.

“Ubora wa Bacca alionao sasa na nidhamu yake ya mchezo anazidi kuwa mchezaji mkubwa na mimi namuona mbali sana, kwa sasa ukiniambia nikutajie beki bora Afrika jina langu la kwanza ni Bacca, ni beki mzuri,” amesema Amrouche na kuongeza;

“Ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kutengeneza mashambulizi, anakaba na ni mwepesi kupanda na kushuka amekuwa bora eneo hilo, siyo mwoga wa kufanya maamuzi.” alisema.

Wakati huohuo akimzungumzia Fei Toto alisema kiungo huyo alikuwa chini kwa muda kutokana na changamoto yake ya mkataba baina yake na timu yake akarudi akiwa chini kiuwezo.

“Nakumbuka nilimuita na kukaa naye kwa ajili ya kumjenga kuwa anatakiwa kusahau yaliyopita awekeze nguvu kwenye mpira kwa sababu ndio ajira yake namshukuru Mungu amefanya hivyo na ameonyesha uwezo mkubwa;

“Anachokifanya sasa kwenye ligi kama atakiendeleza kwenye michuano ya Afcon tutakuwa tunazungumzia mambo mengine hapo baadaye, sioni kama ataendelea kucheza soka la Afrika ni mchezaji mzuri na bora,” alisema

Mbali na wachezaji hao wawili pia alimzungumzia Bajana ambaye pia amemtaja kuwa miongoni mwa wachezaji wazuri kwenye kikosi cha timu ya taifa na ni hazina.

SOMA NA HII  MZUKA WA MECHI ZENYE ODDS KUBWA WIKI HII UKO HIVI NDANI YA MERIDIANBET...