Home Habari za michezo EDO KUMWEMBE:- KWA UWEZO WA HUYU NANGUKA….WAZUNGU WASINGECHELEWA HAPA…

EDO KUMWEMBE:- KWA UWEZO WA HUYU NANGUKA….WAZUNGU WASINGECHELEWA HAPA…

Habari za Yanga leo

ALIWAHI kuulizwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger. Ni kwanini alikuwa anampanga Cesc Fabregas mara kwa mara wakati huo akiwa na miaka 16 kuelekea miaka 17? Wazungu walikuwa wanaona kuna uwezekano wa Fabregas kuchoka mapema kama angetegemewa mapema katika timu kubwa kama Arsenal.

Wenger alijibu kwamba Fabregas alikuwa mbele ya muda. Kwamba alikuwa anacheza mpira wa kikubwa mbele ya muda wake. Wenger alikiri kwamba alikuwa anashawishika kumuweka Cesc nje lakini matamanio ya kumpanga kila mechi yalikuwa makubwa zaidi na kujikuta akimpanga kila mechi.

Sijui Wenger angechukua uamuzi gani baada ya kumuona Hamis Nanguka, kinda mlinzi wa Yanga. Nimeuona katika michuano hii ya Kombe la Mapinduzi nimemuona na yeye kwa huu mpira wetu yupo mbele ya muda.

Mrefu, ana akili ya mpira, anapiga pasi za kwenda mbele. Anajiamini kuliko wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu nchini. Kama Pep Guardiola angemuona basi angempenda zaidi maana ni mchezaji wa aina yake. Mchezaji ambaye anacheza kama Victor Costa. Anapenda kukaa na mpira na kucheza kutokea nyuma. Anajiamini vilivyo na ni mlinzi wa kisasa hasa.

Sijui Yanga wataamua nini juu yake baada ya michuano ya Kombe la Mapinduzi lakini naweza kubashiri ambacho kitaweza kutokea. Sioni kama ataendelea kutumika zaidi katika mechi za Ligi Kuu na tukizubaa tunaweza kukuta tunakutana naye tena Januari mwakani katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Mbele yake kuna Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca. Ni walinzi wazoefu kwa mujibu wa soka letu. Wamecheza mechi nyingi za kimataifa mbele yake. Halafu kuna Gift Fred, mlinzi wa kimataifa wa Uganda.

Huyu Gift amebadili mawazo ya wengi baada ya michuano hii ya Kombe la Mapinduzi. Ni bonge la beki. Jina lake lilihusishwa kukatwa kwa ajili ya kutafuta nafasi kwa wachezaji wa nafasi za mbele. Sijui kama mawazo hayo yataendelea kuwepo.

Nahisi watu wa Yanga wamekubaliana kwamba Gift ni beki mzuri lakini walio mbele yake wamemtangulia kwa sababu wametengeneza kombinesheni nzuri na pia ni watoto wa nyumbani wanaofanya vizuri katika Yanga na timu ya taifa pia.

Kama Gift hachezi nafasi inawezaje kuangukia kwa Nanguka? Mzee Wenger angechukua uamuzi mgumu ya kumuingiza katika kikosi cha kwanza na kucheza baadhi ya mechi huku akithibitisha ubora wake. Wenzetu wanaamini wachezaji wao kwa kuamini kwamba wana vipaji vizuri na wapo mbele ya muda.

Wachezaji wengi waliokuwa na vipaji maalumu walinufaika kwa kuaminiwa mapema. Kina Cesc, Wayne Rooney, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Erling Haaland na wengineo. Ndani ya miaka 18 tu walikuwa wanapata nafasi ya kudumu katika timu kubwa.

Wenger angemuingiza Nanguka kikosini. Wazungu wengine ambacho wangefanya ni kumpeleka kwa mkopo katika klabu ya Ligi Kuu acheze walau msimu mmoja na kisha arudi katika kikosi cha kwanza. Ni kwa ajili ya kupata uzoefu. Sisi tunawapeleka kwa mkopo wachezaji ambao tunamini ni wabovu na hawapaswi kurudi klabuni ila tunasubiri mikataba yao iishe.

Lakini kama unavyojua. Inawezekana Yanga wakawa sahihi kuendelea kumsugulisha benchi Nanguka kwa sababu kina Job wapo mbele yake. Hivi tunavyozungumza wanaenda Ivory Coast kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Kwa wenzetu Nanguka angekuwa bidhaa ya kuuzwa tu. Angeuzwa kwenda katika nchi nyingine au angetolewa kwa mkopo. Yanga wangeingiza kipengele kinachoonyesha akiuzwa kwenda timu nyingine basi wanapata asilimia 20 ya mauzo.

Wakati mwingine lazima tukubaliane kwamba sio kila mchezaji mahiri kinda klabuni basi ataishia katika kikosi cha kwanza. Hapana. Imekuwa rahisi kwa Clement Mzize kwa sababu nafasi ya ushambuliaji huwa ina watu wachache. Wengi wanaweza kuitwa washambuliaji lakini hawana ubora mwingi katika kutupia nyavuni.

Ukiwa mshambuliaji unaweza kupenya kwa urahisi kwenda katika kikosi cha kwanza. Kwa nafasi hii ya ulinzi, hasa kwa timu zetu hizi kubwa ni ngumu kupenya. Hapa ndipo ambapo klabu inachukua uamuzi rahisi wa kuwatafuta mawakala au kukubali ofa za mawakala na kumuweka mchezaji sokoni.

Mchezaji kama yeye, mwenye umbo kama lake ni ngumu kukosa timu ya kucheza katika nchi za watu. Baadaye inakuwa faida kwa timu ya taifa. Ni kama kilichomtokea Novatus Dismas. Alikwenda zake Biashara Shinyanga kwa mkopo, akawasha moto, aliporudi Azam akakuta nafasi yake ina wakongwe, akapelekwa kwa mkopo Israel. Kilichofuata ni historia.

Kwa sababu klabu zetu kubwa zinapenda zaidi kutumia wachezaji kutoka nje, nadhani huu ni wakati sahihi zaidi kutengeneza uhusiano wa kibiashara na baadhi ya timu za nje na kuwapeleka makinda moja kwa moja katika timu hizo badala ya kuwacheleweshea muda wao kwa kisingizio cha kusubiri waingie kikosi cha kwanza.

Washkaji zetu kule Brazil ni mara ngapi wameuza makinda kwenda Ulaya huku wakiwa hawajagusa katika vikosi vya kwanza vya timu zao? Ni suala la ‘connections’ tu ambazo baadaye zitakwenda kulisaidia taifa. sio lazima mchezaji asubiri kuingia kikosi cha kwanza au aende kusota kwa mkopo katika klabu za mikoani ambazo zitadumaza ubora wake kutokana na kuwepo kwa ufinyu wa kambi na miundombinu kwa ujumla.

Nimeona makinda wanne wa Yanga ambao wanaweza kuwa mali moja kwa moja katika vikosi vya vijana nchi za watu kuliko kuwapotezea muda. Macho yetu tumeyaelekeza kwa wachezaji wa kigeni zaidi na nafasi ni ngumu kwao.

Credit:- Mwanaspoti/ Edo Kumwembe

SOMA NA HII  AHMED ALLY: TUWE WA KWELI...WACHEZJI WENGI WA SIMBA WAMECHOKA MNOO..HAWAWEZI TENA...