Home Habari za michezo HIZI HAPA SABABU 9 ZA FEI TOTO KUTUA SIMBA….MAKOCHA WAMPA ‘GO AHEAD’...

HIZI HAPA SABABU 9 ZA FEI TOTO KUTUA SIMBA….MAKOCHA WAMPA ‘GO AHEAD’ YA KWENDA…

Habari za Simba leo

NAMBA za Feisal salum ‘Fei Toto’ hazisemi uongo. Tangu atue Azam FC, amefunga mabao manane na kuasisti mara nne. Jumla amehusika kwenye mabao 12. Si haba kwa mchezaji wa safu ya kiungo na msimu wenyewe hata nusu haujafika.

Yupo mahali salama na bila shaka anafurahia maisha yake ndio maana anapata wakati mwafaka wa kutoa namba kama hizo uwanjani.

Umbali wa kilomita 18 kutoka Chamazi hadi Kariakoo, Dar es Salaam kuna klabu ingependa kuwa na kiungo wa aina ya Fei Toto kwenye kikosi kutokana na huduma anayotoa uwanjani. Hao ni Wekundu wa Msimbazi, Simba.

Watampataje? Mkataba wa Fei Toto huko Azam FC bado mbichi, lakini kwenye soka chochote kinaweza kutokea wakati wowote. Fei Toto anaweza kuondoka Azam. Fei Toto anaweza kwenda Simba.

Pamekaaje hapo? Achana na habari za mkataba, kwamba kuna madai ya kuwapo kipengele kinachomzuia eti asiende Simba. Hayo ni mambo ya kisheria, lakini mfano tu, kama Fei Toto ataachwa na Azam FC kwa sababu zozote zile, kisha Fei Toto akawa mchezaji huru mtaani, Simba haiwezi kumsajili? Kuna kitu kingine, Azam FC inaweza kumuuza Fei Toto, kisha ikafanyika u-turn ‘Zanzibar finest’ akatua Msimbazi.

Kwanini dili hili litatokea? Hizi ni sababu za kumpeleka Fei Toto Simba.

Wanatakana; Simba inamtaka Fei na Fei anaitaka Simba. Baada ya kucheza Yanga na Azam FC, klabu mbili kubwa katika soka la Tanzania, mahali ambako Fei Toto atakuwa amebakiza ni Simba na bila ya shaka mwenyewe atahitaji kwenda kucheza ili kuingia kwenye orodha ya wachezaji waliopata kucheza kwenye timu zote kubwa katika soka hapa nchini.

Kama kuna kitu Fei Toto amekifanya Yanga na Azam FC, ni wazi atahitaji kwenda kukifanya pia kwenye kikosi cha wababe hao wa Msimbazi ili kuweka jina lake kwenye anga za juu katika soka la ndani. Simba pia inahitaji huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Tanzania.

2. Michuano ya kimataifa; Linapokuja suala la soka la kimataifa, Simba ni klabu inayoonekana kuwa siriazi kwenye mashindano hayo ikivuka hatua za makundi mara nne kwa miaka ya karibuni na kutinga robo fainali katika mashindano ya klabu Afrika.

Kwa Simba kwenda kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa itahitaji kuwa na huduma ya mchezaji wa aina ya Fei Toto kwenye kikosi ili kuvuna matokeo inayotaka. Lakini, ushiriki wa Simba kwenye soka la kimataifa na kutamba kwa maana ya kufika kwenye hatua za juu kama robo fainali ni jambo litakalomvutia Fei Toto kwenda kujiunga na timu hiyo kwa sababu itampa fursa ya kujitangaza na kuonekana ndani na nje.

3. Rekodi ya upekee; Kwa wachezaji wazawa ni wachache waliowahi kuandika rekodi ya kucheza timu tatu kubwa kwenye soka la Tanzania – Simba, Yanga na Azam FC. Kwa miaka ya karibuni, rekodi hiyo iliwekwa na winga Mrisho Ngassa, bila ya shaka Fei Toto atapenda pia kuingia kwenye rekodi hiyo ya kipekee kwa kucheza Yanga, Azam FC na Simba.

Kingine ni kwamba imeshuhudia mastaa kadhaa wakivuka kutoka Azam FC kwenda Simba kama vile John Bocco, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni na Aishi Manula kwa kuwataja kwa uchache na wakali hao wote walipata mafanikio makubwa wakiwa kwenye jezi za Simba. Bila shaka Fei Toto atataka kwenda kuingia kwenye orodha hiyo ya wenye rekodi za kipekee.

4. Staili ya uchezaji; Simba ni timu yenye historia ya kutandaza soka la chini na kuwa na wachezaji wengi wenye ufundi mwingi kwenye sehemu ya kiungo. Staili ya uchezaji ya miamba hiyo ya Msimbazi inaendana kabisa na mpira anaocheza Fei Toto. Staili ya kiuchezaji za pande zote mbili zinashaabiana, hivyo Simba wataamini wanamsajili mchezaji ambaye hatakuwa na shida ya kuzoea staili yao na Fei mwenyewe hatakuwa na kikwazo kwa sababu anatambua anakwenda kucheza mahali ambako staili yake ya uchezaji moja kwa moja itakwenda kutiki kwenye mfumo.

5. Mrithi sahihi wa Chama; Hakuna kificho, Simba kwa sasa inapiga hesabu za kuachana na supastaa Clatous Chama ikiwa na sababu nyingi tofauti. Umri pia umeanza kumtupa mkono Chama, hivyo Simba inahitaji damu changa kwenye eneo analocheza Mzambia huyo ili kuwa na nguvu mpya katika kikosi. Na kwenye hilo, Fei Toto linaweza kuwa chaguo sahihi katika orodha ya wachezaji wanaostahili kwenda kurithi buti za Chama kutokana na uwezo wake wa kufunga kwa staili zote na kupiga pasi za mwisho.

Faida kubwa itakayopata Simba kwenye usajili wa Fei Toto tofauti na ambavyo Chama amekuwa akiipatia huduma, staa huyo wa Zanzibar amekuwa na uwezo wa kufunga kwa mabao ya mashuti ya mbali.

6. Mashabiki wanampenda; Fei Toto alicheza kwa miaka mingi kwenye kikosi cha Yanga ambacho ni mahasimu wakubwa wa Simba. Amewafunga mara nyingi, lakini sehemu ambayo Fei amefanikiwa ni kukubalika kwa mashabiki wa Simba, hivyo ni mahali ambako atakwenda na kupokewa kifalme endapo ataamua kwenda kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.

Hakuna takwimu rasmi kuonyesha ni kiasi gani mashabiki wa Simba wanamkubali Fei Toto, lakini ni usajili ambao hakuna shabiki wa wababe hao wa Msimbazi atauchukia.

7. Kocha Abdelhak Benchinkha anafurahia; Hakuna kocha kwenye soka la ukanda huu wa Afrika atakataa kuwa na huduma ya mchezaji kama Fei Toto kwenye kikosi chake. Huko Simba Benchikha atahitaji kuwa na wachezaji wenye viwango na uwezo wa kuamua mechi kama ambavyo Fei Toto amekuwa akifanya, hivyo saini yake ikinaswa ni kitu kitakachompa furaha kocha huyo kwa sababu mchezaji huyo atampa machaguo mengi ya mifumo ndani ya uwanja.

8. Alishamalizana na Yanga; Msuguano uliotokea wakati Fei Toto anaachana na Yanga kwenda Azam FC bila shaka umeacha makovu mengi kwenye pande zote mbili. Yanga haikufurahishwa na staili ambayo Fei Toto aliondoka nayo, hivyo ni mahali ambako hata mwenyewe atafikiria mara mbili litakapokuja suala la kurudi tena kucheza kwenye eneo hilo.

Kwa kile kilichotokea, Fei Toto ni kama ameshamalizana na Yanga. Hata mashabiki wa timu hiyo kwa sasa hawamkubali kama ilivyokuwa awali, hivyo jambo hilo linaweza kumsukuma akafanya uamuzi mwepesi kabisa itakapoletwa mezani ofa ya kwenda kujiunga na Simba.

9. Uhakika wa makombe; Yanga ilimpa mataji ya kutosha Fei Toto. Amehamia Azam FC kwenda kuanzisha utawala wake na kusaka mataji. Lakini, kama wababe hao wa Chamazi watashindwa kumpa mataji, bila ya shaka Fei Toto anafungua milango kwenda Simba kwa sababu ni mahali ambako anaamini mataji yanapatikana kirahisi.

Kwa msimu huu Simba imeshabeba Ngao ya Jamii na imetinga nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, hivyo ni timu ambayo haijajiweka mbali na mataji, mvuto ambao utamfanya Fei Toto kwenda Simba.

WASIKIE MAKOCHA

Akizungumzia nafasi ya Fei Toto ndani ya kikosi cha Simba, Kocha wa TMA FC inayoshiriki Ligi ya Championship, Maka Mwalwisi amesema: “Endapo Simba watamsajili Fei, basi utakuwa ni bonge la usajili ambao haujawahi kutokea kwa Simba hivi karibuni.

“Fei ni mchezaji mzuri. Ana uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga. Akienda Simba kocha amchezeshe kama namba 10, yaani acheze nyuma ya mshambuliaji maana Saido (Said Ntibazonkiza) amepungua nguvu, hivyo pale Simba akisajiliwa anaingia kikosi cha kwanza moja kwa moja.”

Naye kocha wa JKU, Salim Ali Haji ameelezea kuwa: “Ingawa sina imani kabisa kwamba Fei Toto anaweza kwenda Simba, ila lolote linaweza kutokea. Wakifanikiwa basi Simba watakuwa wamelamba dume.

“Kwa sasa Tanzania haina kiungo bora mzawa kama Fei Toto, ingawa hata hao wageni wanaowapigia kelele hawafikii uwezo wake. Anamudu kucheza mifumo yoyote ambayo kocha ataamua kuitumia iwe 4-4-2, 4-3-1 na mingine. Ni mchezaji wa kipekee.”

SOMA NA HII  ‘GUTY’ HUYOO SIMBA