Home Habari za michezo KOCHA TAIFA STARS ALIVYOBADILI UPEPO WA MASHABIKI WA BONGO KUHUSU TIMU YA...

KOCHA TAIFA STARS ALIVYOBADILI UPEPO WA MASHABIKI WA BONGO KUHUSU TIMU YA TAIFA…

Taifa Stars

Zimebaki siku chache sana kabla ya kuanza kwa fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) ambazo zitafanyika huko Ivory Coast, kuanzia Januari 13 hadi Februari 11.

Tayari timu zote 24 zitakazoshiriki mashindano hayo zimeshatoa vikosi vyake vya awali na baadhi zimeshaamua kuweka hadharani vikosi vyao vya mwisho ambavyo vitapeperusha bendera kwenye hayo mashindano.

Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ bado haijatangaza kikosi chake cha mwisho ambacho kitashiriki AFCON lakini kocha Adel Amrouche ameshaanika majina ya nyota 55 wa kikosi chake cha awali ambao watachujwa na kubakia 27 watakaokuwepo Ivory Coast.

Katika kikosi cha awali, kocha Adel Amrouche ameita idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania pengine kuliko nyakati nyingine zote ambazo tumewahi kushuhudia kikosi cha Stars kikitangazwa.

Idadi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ni 27 ambayo ni kama nusu ya kikosi chote, namba ambayo ni kubwa zaidi na jambo zuri zaidi wengi wao ni vijana ambao wanaweza kuitumikia Taifa Stars kwa muda mrefu zaidi ikiwa watatunza na kuboresha zaidi viwango vyao.

Ni aina ya mabadiliko ambayo kocha Amrouche anaonyesha anataka yafanyike katika nchi kwanza kwa kujenga hali ya ushawishi kwa idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza hapa nyumbani watamani zaidi kwenda nje ili wakaboreshe na kuimarisha zaidi viwango na vipato vyao.

Tunapaswa kukubali kwamba bado timu zetu za hapa nchini haziwezi kututengenezea timu bora na tishio ya taifa ambayo itatupa uhakika wa kufanya vizuri dhidi ya mataifa ambayo yamepiga hatua kubwa kisoka.

Lakini Amrouche anatubadilisha fikra zetu juu ya umuhimu wa kuwa na wachezaji ambao wana asili ya Tanzania na kutukumbusha kutengeneza misingi bora na utaratibu mzuri wa kuwapata na kuwatumia kwa faida ya timu.

Kuna wachezaji amewaita kutoka madaraja ya chini inawezekana viwango vyao havitofautiani sana na wale waliopo hapa nchini lakini kwa kuitwa timu ya taifa na kucheza, tutawapandisha thamani na watapata timu za madaraja ya juu zaidi na hivyo kuwa tegemeo letu siku za usoni.

Ni uthubutu tu wa Amrouche ambao naamini utatubadilisha mashabiki na wachezaji wetu.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA KUTAMBULISHWA SIMBA...KOCHA MRENO AIBUKA NA NENO HILI LA KWANZA KWA MASHABIKI...