Home Habari za michezo KUHUSU ISHU YA KUWAACHA KONKONI , GIFT….MABOSI YANGA WAPASUA VICHWA…

KUHUSU ISHU YA KUWAACHA KONKONI , GIFT….MABOSI YANGA WAPASUA VICHWA…

Habari za Yanga

IKIWA imesalia wiki moja tu kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa rasmi, huku Yanga ikitajwa kushusha mshambuliaji mmoja kabla ya kufungwa kwa usajili, vita mpya imeibuka kutoka kwa mastaa wanaotajwa kuachwa huku Hafiz Konkoni na Gift Fred wakiwapasua vichwa mabosi wa klabu hiyo.

Yanga inapambana kusaka saini ya mshambuliaji atakayeiongeza nguvu eneo hilo akisaidiana na Kennedy Musonda, shida iliyopo ni namna Hafiz Konkoni anawapasua kichwa mabosi wa timu hiyo akiwataka wavunje benki ili awapishe wachezaji wengine.

Yanga tayari imemsajili winga Augustine Okrah, lakini inasaka saini ya mchezaji mwingine wa eneo la ushambuliaji huku Konkoni aliyerejea Dar kutoka Zanzibar iliko timu, imethibitishwa kuwa ameugomea uongozi kumtoa kwa mkopo kwenda timu yoyote, akitaka avunjiwe jumla mkataba.

Mbali na Konkoni pia taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimethibitisha kuwa mpango wa kuachwa kwa beki Gift Fred unaweza kuota mbawa kutokana na beki huyo kuonyesha uwezo mzuri kwenye michuano ya Mapinduzi.

Gift ndio lilikuwa chaguo la pili kupisha sajili mpya kwa mastaa wa kigeni ndani ya timu hiyo lakini kocha Gamondi ameonekana kuvutiwa na uwezo wa beki huyo Mganda anayetumika katika michuano ya Mapinduzi 2024 kutokana na safu ya ulinzi ya timu hiyo hasa beki ya kati yote kuitwa timu ya taifa.

Ubora wa Gift anaouonyesha ndani ya timu hiyo nao unaongeza ugumu wa kufanya uamuzi kwa viongozi wa Yanga hivyo kubaki wakiwaza wanamtoa nani na anabaki nani ili kuingiza sajili mpya.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa, Konkoni ameondoka Zanzibar baada ya kushindwana na viongozi kuhusiana na kuomba kupewa muda zaidi ili aonyeshe uwezo, huku viongozi wakimuomba wamtoe kwa mkopo katika moja ya timu zilizopo kwao Ghana.

“Ni suala la muda tu kwa mshambuliaji huyo kumalizana na klabu kwani mazungumzo yalikuwa ni kutolewa kwa mkopo huku yeye mwenyewe akiomba kupewa muda wa kucheza ili aweze kuonyesha uwezo alionao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

‘’Mchezaji aligoma kutolewa kwa mkopo na kuuomba uongozi umalizane naye kwa kumlipa stahiki zake zote za mkataba ili aende kutafuta maisha mengine nje ya Yanga kwa kutafuta timu anayoitaka yeye acheze.

“Kwa Gift pia mapya yameibuka anaonekana kumkosha Gamondi kwani amekuwa bora sasa tofauti na alivyokuwa anachukuliwa mbele ya uwepo wa Dickson Job, Bakari Mwamnyeto ambaye pia mkataba wake unaelekea ukingoni na Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ ambao wamejihakikishia nafasi kutokana na ubora wao hivyo kumnyima nafasi ya kuonekana na sasa kabaki mwenyewe anafanya vitu vikubwa na kumpa wakati mgumu kocha kufanya uamuzi.”

Wakati hali ikianza kuwa nzuri kwa upande wa Gift, mtihani upo kwa Moloko na Skudu ambao wana kazi ya kufanya ili kujihakikishia nafasi ya kubaki.

Moloko mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu huku Skudu akiwa bado ana mkataba na timu hiyo.

SOMA NA HII  AHMED ALLY : TULIACHANA NA ZORAN KWA SABABU ALIKATAA BAADHI YA WACHEZAJI WETU...